Category: Local News

  • Wajasiriamali wahofia usimamizi wa jeshi katika sakata la korosho

    Wajasiriamali wahofia usimamizi wa jeshi katika sakata la korosho

    Wanawake wajasiriamali wanaoshughulika na kubangua korosho nchini wamelalamikia mpango mpya uliotangazwa na rais Magufuli ambapo sasa jeshi la nchi litasimamia biashara shughuli hiyo.
    Wanawake hao wanasema kuwa hatua hiyo itawanyima fursa ya ununuzi wa kiwango cha kawaida kwa lengo la biashara ndogo ndogo kwani, wana wasiwasi kwamba huenda jeshi likabadili kabisa mfumo wa uuzaji korosho tofauti na walivyo zoea.
    Hapo jana ikiwa ni kabla ya muda uliowekwa kwa wafanyabiashara kujiorodhesha ili wanunue korosho ya wakulima mkoani Mtwara, rais alibadili mawazo yake na kuamua kwamba wafanya biashara hao hawatanunua tena korosho hiyo, akihoji kwamba walikuwa wapi.

    “Yani huu mpango ambao rais ameuweka katika uuzaji wa korosho Mtwara kusimamiwa na jeshi, sisi wafanyabiashara wadogo kiukweli wametuangusha”, amedai mmoja wa wanawake ambaye ni maarufu kwa biashara hiyo.

    “Mimi ni mjasiriamali mdogo ambaye nnanunua gunia moja au mbili katika kipindi cha msimu wa korosho , nabangua na kuuza. Sasa wameweka usimamizi wa jeshi , nitanunua wapi? Nina miaka 15 ninafanya hii shughuli nnaendesha maisha na nnasomesha watoto”… amelalamika mjasiriamali mwingine mwanamke.

    Leo ni siku ya pili Baada ya serikali kukabidhi Jeshi la nchi hiyo, kuratibu shughuli za ununuzi wa korosho katika mkoa ulioko Kusini mwa nchi hiyo, Mtwara.

    Hali imepoa kidogo leo Mtwara hakuna kazi

    Hatua hiyo inafuatia Rais John Magufuli kusitisha mpango wa makampuni kununua zao hilo kwa kile alichodai wamekuwa na bei hazina tija kwa wakulima .

    “Kiukweli nimevurugwa kwa msimamo huu uliowekwa, kwa sababu sisi ni wajasiriamali wadogo ambao hatuna uwezo wa kununua tani moja, tani mbili ..tunajikwamua tu kidogo kidogo.

    Wanasaidiwa wakulima lakini sisi wajasiriamali wadogo wadogo tutaishije?”

    Kwa sasa korosho zinauzwa kwa gharama ya shilingi 3,300 badala ya shilingi 3000 za kitanzania ambayo ni sawa na dola 1.43.

    Rais amesema anataka kuhakikisha maelfu ya wakulima wanapata faida kwa mazao yao na kuhakikisha kipato kutokana na usafirishaji wa korosho katika mataifa ya nje.

    Lakini wakosoaji wanasema huenda ni hatua ya kujaribu kutafuta uungwaji mkono katika eneo la Mtwara, eneo lililo ngome ya upinzani.

    Mwansiasa wa upinzani Zitto Kabwe amesema serikali inastahili kupata ridhaa ya bunge kununua korosho hizo.

    Kadhalika rais Magufuli ameivunjilia mbali bodi ya usimamizi wa zao la korosho Tanzania na kutegua uteuzi wa mwenyekiti wake, Anna Abdallah.

  • Serikali ‘yakaza buti’ mzozo wa korosho

    Serikali ‘yakaza buti’ mzozo wa korosho

    Rais John Magufuli

    Rais John Magufuli amesema kwamba kuanzia Jumatatu wanunuzi wa korosho hawaruhusiwi tena kununua bidhaa hiyo kutoka kwa wakulima.

    Serikali sasa iko tayari kununua korosho hizo kwa gharama ya shilingi 3,300 badala ya shilingi 3000 za kitanzania ambayo ni sawa na dola 1.4.

    Na kukabidhi rasmi kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuzichukua korosho hizo.

    Mzozo huu wa korosho umekuwa gumzo kubwa kwasababu korosho zina umuhimu mkubwa kutokana na kuwa usafirishaji wake katika nchi za nje ndio mojawapo ya kitega uchumi nchini.

    Pamoja na uamuzi huo, rais Magufuli ametangaza kukitaifisha kiwanda kimoja cha korosho kilichokuwa kiamilikiwa na mtu binafsi kinachofaamika kama ‘Bucco’ na kuwakabidhi wanajeshi.

    Amesema kiwanda hicho kina uwezo kwa kutengeneza korosho mpaka kilo 20 elfu kwa mwaka hivyo hizo tani hizo 70 elfu ni kidogo sana kazi za wanajeshi.

    “Na kuanzia leo wanajeshi inabidi wakakizingire na wakishindwa na kupewa watu wengine” Rais Magufuli amesisitiza.

    Soko la Korosho Kimataifa

    Rais Magufuli ameongeza kwa kusisitiza kuwa ameangalia soko la korosho na korosho za Tanzania ni za kiwango cha juu.’

    Kwa upande wao wakulima,bbc ilizungumza na mmoja wa mfanyabiashara na mkulima wa zao la korosho ambaye alisifu umuhimu wa korosho katika uchumi wa mkoa wa Mtwara.

    Alibainisha kwamba korosho inatoa ajira za muda katika mkoa huo lakini mfumo uliokuepo ulikuwa unarudisha nyuma mauzo na kuwafanya wakulima kushindwa kupata faida.

    Na kwa upande wao wanunuzi wa zao hilo walishindwa kufikia bei ambayo wangeweza hata kuuuza mwaka jana.

    Mnamo mwezi Juni mjadala mkali ulizuka nchini Tanzania kuhusu mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2018 /2019 katika zao la korosho. Mapendekezo hayo ni pamoja na kuondolewa kwa ruzuku ya asilimia 65 iliyokuwa inaenda kwenye Mfuko wa Maendeleo wa Korosho na badala yake, iende kwenye mfuko mkuu wa serikali.

    Chama cha ushirika kilibainisha tatizo lililopo la teknolojia ya kunyunyizia na utegemezi wa pembejeo kutoka nje.

    Kwa takribani miaka 10, korosho imekuwa zao lililoleta matokeo chanya ambapo tangu mwaka 2007/08 bei ilikuwa shilingi 250 mpaka 500 kwa kilo ila sasa hivi wastani ni shilingi 3000 mpaka 5000 kwa kilo.

    Msimamo wa serikali kuhusu bei ya korosho

    Ingawa mwezi Oktoba tarehe 28, 2018 baada ya serikali ya Tanzania kufanya mazungumzo na wanunuzi wa zao la korosho, Serikali ililazimika kuchukua hatua ya kuwalazimisha wanunuzi kununua korosho hizo na hata kutishia kuwafutia leseni wafanyabiashara hao.

    Katika mazungumzo hayo Serikali iliungana na msimamo wa wakulima wa korosho wa kukataa bei ya kati ya shilingi 1,900 hadi 2,700 kwa kilo, na hivyo kukubaliana kuwa korosho zitanunuliwa kwa bei isiyopungua shilingi 3,000 kwa kilo.

    Na mtaalamu wa uchumi na biashara nchini Tanzania, Johakim Bonaventure anasema serikali imeamua kutekeleza sera ya kuweza kuhodhi ile kodi ya kuuza nje, mwanzoni ilikuwa inahozi kwa asilimia 35 ya kipato hicho lakini sasa hivi imechukua na ile asilimia 65.

    ‘Ni jambo jema lakini kiuchumi kuna mambo kadhaa ambayo yanaweza kuwa yameandamana nayo na mojawapo ni kupunguza uwezo wa vyombo vinavyosimamia mazao sio korosho pekee yanayolimwa katika baadhi ya maeneo.’

    Mtaalamu huyo amesema kama zao la korosho likiweza kuathirika basi pato linaweza kuathirika pia.Bado kuna uwezekano wa kukaa chini kuangalia faida na hasara.

    Mwaka jana zao la korosho limeweza kuleta mapato makubwa katika taifa na sasa linatangazwa kuanzishwa katika maeneo mengine 17.

    cc;BBCswahili

  • Serikali yatishia kufuta leseni za wafanyabiashara wa korosho

    Serikali yatishia kufuta leseni za wafanyabiashara wa korosho

    Sakata la korosho nchini  lianendelea kufukuta na sasa serikali ya nchi hiyo imewapa wafanyabiashara siku nne za mwisho kununua zao hilo.

    Kikao cha Rais Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kati) na Waziri wa Kilimo Charles Tizeba pamoja na wafanyabiashara Septemba 28 kilitazamiwa kumaliza sakata la ununuzi

    Siku 11 zilizopita, Rais John Magufuli pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa walikutana na wanunuzi wa zao hilo baada ya kutokea mgomo wa wakulima kuuza korosho zao kwa wanunuzi hao.

    Mwaka jana zao hilo liliuzwa kwa wastani wa Shilingi 4,000 kwa kilo lakini mwaka huu bei ikaporomoka mpaka wastani wa Sh1,900 mpaka Sh2,700 kwa kilo.

    Mgomo wa wakulima hao uliungwa mkono na Serikali ambapo tarehe 28 Septemba kwenye kikao baina yao na Magufuli na Majaliwa wafanyabiashara hao walikubali kununua zao hilo kwa bei isiyopungua Sh3,000 kwa kilo.

    Serikali pia ilikubali kwa upande wake kuondosha baadhi ya tozo na vikwazo vilivyopelekea wafanyabiashara kushusha bei.

    Hata hivyo, wafanyabiashara hao wanaounda kampuni 35 wanaripotiwa kutonunua korosho hiyo kama ilivyotarajiwa na hali hiyo imechukuliwa na serikali kama mgomo baridi.

    Leo hii Waziri Mkuu Majaliwa amekuja na onyo la mwisho; waseme ndani ya siku nne zijazo watanuanua tani ngapi na lini ama wafutiwe leseni zao za biashara.

    “Hivyo wanunuzi waliojiandikisha wakiwemo na wale wote ambao wamekuwa wananunua kwenye minada lakini kwa kiasi kidodo, wahakikishe ndani ya siku hizo nne kuanzia leo Ijumaa hadi Jumatatu saa 10 alasiri wawe wameleta barua na ofisi yangu ipo wazi saa 24,” amesema Majaliwa.

    “Mwenye nia ahakikishe katika siku hizo nne iwe ndio mwisho wa kununua korosho na waandike barua wakionesha kiwango wanachokihitaji. Zaidi ya hapo serikali haitoruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena.”

    Katika kikao cha Septemba 28, Rais Magufuli alinda mbali kwa kuwaambia wafanyabiashara hao kuwa serikali yake ipo radhi kuzinunua korosho zote kwa bei inayowafaa wakulima na kuziuza katika masoko ya kimataifa nchini Marekani na Uchina.

    Rais Magufuli amesema yupo tayari kutumia jeshi kununua korosho kwa bei ambayo inakubalika na wakulima.

    “…nipo tayari hata kutumia majeshi yetu kununua korosho na tutatafuta masoko ya uhakika ili tuuze kwa bei nzuri” amesisitiza Rais Magufuli.

    Jana Alhamisi Majaliwa alitangaza bungeni kuwa serikali pia inajadiliana na wanunuzi kutoka nje ya nchi ili kuwavutia kununua zo hilo ambalo ndilo mhimili mkuu wa kiuchumi kwa wakaazi wa mikoa ya kusini mwa.

    Wafanyabiashara wa korosho wakimsikiliza Rais Magufuli Septemba 28

    Mapema mwezi Mwezi Juni mwaka huu kulikuwa na mnyukano bungeni ambapo wabunge bila kujali tofauti zao za kisiasa walikuwa wakiyapinga mapendekezo ya serikali katika Sheria ya Fedha wa mwaka 2018 kwa kuchukua asilimia 100 ya tozo za mauzo ya korosho nje ya nchi (Export levy) kupelekwa mfuko mkuu wa fedha za serikali.

    Awali, asilimia 65 ya tozo hiyo ilikuwa ianenda kwenye mfuko wa zao hilo na baadae kurejeshwa kwa wakulima kupitia pembejeo. Hoja ya wabunge wakiongozwa na kamati ya bajeti ilikuwa, hatua ya kuchukua fedha zote ingeleta athari kubwa kwa maendeleo ya zao hilo na wakulima wake.

    Mjadala ukawa mkali lakini hoja ya serikali ikapita. Baadae, Rai John Magufuli akasema hakupendezwa na namna ya wabunge wa CCM hususani wa mikoa ya kusini kwa namna walivyolijadili suala hilo, na akatishia kuwa laiti wangeliandamana basi angetuma askari wawaadhibu.

    Msimu wa mwaka jana, serikali iliingiza kiasi cha dola 209 milioni za Marekani kutokana na zao la korosho.

  • CPJ yapatwa na hofu ya wafanyakazi wake kukamatwa

    CPJ yapatwa na hofu ya wafanyakazi wake kukamatwa

    Kamati ya Kimataifa ya Kuwalinda Waandishi wa Habari CPJ imezitaka Mamlaka nchini Tanzania kuwaachia huru wawakilishi wake wawili barani Afrika, Mratibu wa progam barani Afrika Angela Quintal na Muthoki Mumo mwakilishi wa CPJ kusini mwa jangwa la Sahara ambao wanadaiwa kukamatwa na Idara ya Uhamiaji nchini.

    Muthoki Mumo
    Angela Quintal

    Kwa mujibu wa Taaarifa iliyotolewa na kuchapishwa kwenye tovuti ya CPJ, Afisa mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa Idara ya Uhamiaji aliwakamata wafanyakazi hao wawili wa CPJ Angela Quintal na Muthoki Mumo, katika hotel waliyofikia jijini Dar es Salaam ambapo walikagua vitu walivyokuwa navyo na baadae kuchukua pasi zao za kusafiria.

    Taarifa hiyo inadai Wafanyakazi hao ambao wamekuja nchini kwa masuala ya kikazi, inaelezwa kuwa waliondolewa hotelini na kupelekwa sehemu wasioijua.

    Mkurugenzi mtendaji wa CPJ Joel Simon amesema wana wasiwasi na usalama wa wafanyakazi wao huku wakidai kuwa waliingia Tanzania ki uhalali.

    Ametoa wito kwa mamlaka nchini kuwaachia na kuwarejeshea pia pasi zao hizo za kusafiria.

    “Ni jambo la kutia wasi wasi mkubwa kuwa huenda simu ya Angela Quintal imetumiwa bila idhini yake. Hatujawasiliana na Angela Quintal au Muthoki Mumo tangua wakamatwe na tunaamini kuwa wote wanazuiliwa na mamlaka za Tanzani,” Joel Simon aliandika kwenye Twitter.

    Hata hivyo akizungumza kwa njia ya simu Afisa Habari wa Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania Ali Mtanda amesema hana habari kuhusiana na taarifa hiyo na kwamba bado hazijafika makao makuu na kutaka kupewa muda, ili kuweza kuthibitisha.

    Hata hivyo taarifa ambazo bado hazijathibitisha zilizotufikia muda huu ni kwamba wafanyakazi hao wa CPJ hao wameachiliwa huru.

    cc; BBCswahili

  • Mashoga wapo salama

    Mashoga wapo salama

    Waziri wa Mambo ya Ndani nchi Kangi Lugola amesema kuwa wapenzi wa jinsia moja hawapo hatarini nchini humo.

    Lugola amesema japo ushoga ni kosa la jinai nchini, wanaojihusha na vitendo hivyo hawatishiwi maisha na wala hawaikimbii nchi.

    Akizungumza na gazeti la serikali la Habari Leo, Lugola amekanusha kuwa wapenzi wa jinsia moja wapo hatarini.

    “Ninachosema ni kuwa Tanzania ni salama na hakuna mtu yeyote anayeweza kusema kuwa sio salama bila ya kuwa na vigezo husika, kama mtu yeyyote anahatarishiwa maisha yake, basi napaswa kwenda polisi na mimi sijapata taarifa zozote kutoka polisi zinazoeleza kuwapo kwa mazingira hatarishi ya watu hao,” Lugola amenukuliwa akisema.

    Hata hivyo, wakati Lugola akitoa hakikisho la usalama kwa mashoga, watu 10 wamekamatwa na polisi Zanzibar kwa tuhuma za kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

    Shirika la kutetea Haki za Binaadamu la Amnesty International limeripoti kuwa wanaume hao 10 wamekamatwa Jumamosi iliyopita katika fukwe ya Pongwe walipokuwa katika harusi ya mashoga. Wengine sita walifanikiwa kuwatoroka polisi.

    “Polisi walifika eneo la tukio baada kupewa taarifa na wananchi kuwa kuna harusi ya mashoga inaendelea…Watu hao wanashikiliwa katika kituo cha polisis Chwaka na mpaka sasa hakuna mashtaka yoyote yaliyofunguliwa,” inasema ripoti ya Amnesty.

    Sababu hawajakamatwa wakiwa wanafanya ngono, Naibu Mkurugenzi wa Amnesty kwa kanda ya Afrika Mashariki Seif Magongo anahofu kuwa watalazimishwa kufanyiwa vipimo.

    Serikali imejitenga na kampeni ya Paul Makonda dhidi ya ushoga

    Wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alitangaza kuanza kampeni dhidi ya ushoga kwa kuunda kamati ya watu 17.

    Makonda alisema haki za mashoga hazitambuliki kama haki za binaadamu nchini Tanzania na kuzitaka nchi zinazotetea vitendo hivyo kuwachukua mashoga wa Tanzania.

    Baada ya kauli hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Tazania ilitoa taarifa kuwa huo si msimamo wa serkali bali mawazo ya Makonda pekee.

    Taarifa hiyo ilisema Tanzania itaendelea kuheshimu haki zote za binaadamu kama inavyotakikana na katiba ya nchi pamoja na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeisaini na kuiidhinisha.

     

  • Abdul Nondo ashinda kesi ya ‘kujiteka’

    Abdul Nondo ashinda kesi ya ‘kujiteka’

    Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imemuachia huru Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi  (TSNP), Abdul Nondo.

    Nondo ameshinda kesi aliyofunguliwa na upande wa jamuhuri toka mwezi Machi mwaka huu.

    Katika kesi hiyo, Nondo alikuwa anakabiliwa na mashtaka mawili, la kwanza kutoa taarifa ya uongo kwa ofisa wa polisi wa kituo Mafinga akidai alitekwa na watu wasiojulikana.

    Katika shtaka la pili, Nondo alidaiwa kutoa taarifa za uongo mtandaoni kuwa yupo katika hatari.

    Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu Liad Chamchama na Nondo aliwasilisha utetezi wake Septemba 18 na 19.

    Akizungumza na BBC wakili wa Nondo Jebra Kambole amesema upande wa utetezi wamepokea hukumu hiyo kwa mikono miwili na kuishukuru mahakama kwa kusimama katika haki.

    “Mahakama imetenda haki katika kipindi hiki kigumu sana, hili limetufanya kuendelea kuwa na Imani thabiti juu ya taasisi ya mahakama,” amesema Jebra.

    Nondo ambaye ni mwanafunzi wa Sayansi ya Siasa na Utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisimamishwa masomo toka alipofunguliwa kesi hiyo, huku uongozi wa chuo ukisema angeendelea na masomo baada ya kumalizika kwa kesi yake.

    “Tunashukuru kesi imeisha kwa ushindi kwetu, sasa mwananfunzi (Nondo) arejee shule amalize masomo yake,” amesema Jebra.

    Hakimu Chamchama katika maelezo yake amesema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha pasi na shaka tuhuma zilizokuwa zinamkabili Nondo.

    Mwezi Machi mwaka huu, Nondo ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali juu ya maslahi ya wanafunzi alituma ujumbe mfupi kwa watu wake wa karibu akisema kuwa yupo hatarini.

    Baada ya kutoweka, uongozi wa TSNP ikatoa taaaarifa ya chama hicho cha wanafunzi inasema Bw Nondo amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana.

    Wakati mmoja, anadaiwa kukamatwa na askari wa jeshi la polisi eneo la Milimani City na kutuhumiwa kwamba “analeta uchochezi wa baadhi ya wanafunzi waliokosa mikopo ya elimu ya juu kuandamana.”

    “Mara kadhaa kumekwua na makundi ya watu asiowatambua na wenye nguo za kiraia wakijitambulisha kama watu wa usalama ambao wamekuwa wakimfuatilia na kumpa vitisho hivyo,” taarifa hiyo ilisema.

    Baada ya siku moja alipatikana akiwa hajitambui wilayani Mafinga mkoani Iringa na kudai kuwa alitekwa na kutelekezwa na watu wasiojulikana.

    Hata hivyo, madai hao yalipingwa vikali na polisi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo Mwigulu Nchemba amabye alidai mwanafunzi huyo “alijiteka”. Baada ya kushikiliwa kwa siku kadhaa mjini Iringa na jijini Dar es Salaam, hatimaye alifunguliwa mashtaka ambayo ameyashinda hii leo.

  • Biashara ya ngono na ushoga vita vikali na rc makonda

    Biashara ya ngono na ushoga vita vikali na rc makonda

    Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda ameunda kamati maalum ya watu 17 ili kuhakikisha kuwa watu wanaofanya biashara chafu za ngono wanachukuliwa hatua za kisheria.

    Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam

    Kamati hiyo ambayo imejumuisha watu kutoka bodi ya filamu, Mamlaka ya mawasiliano Tanzania TCRA, polisi kutoka kitengo cha kuzuia uhalifu wa mitandao,madaktari na wanasaikolojia.

    Makonda amesema kuwa kamati hiyo aliyoiunda itafanya kazi katika makundi manne;

    • Kamati itakayoshughulika na mashoga wanaojitangaza na wasiojitangaza lakini wanajulikana kuwa mashoga.
    • Kamati itakawashughulikia wale wote wanaotengeneza picha au video za ngono ambapo mpaka sasa tayari ana udhibitisho wa taarifa za nyumba 24 ambazo zinashughulika na kazi hiyo.
    • Kundi ambalo litaangazia watu wote wanaotangaza biashara ya ngono kwa njia ya mtandao ya kijamii kama instagram,whatsapp na facebook.
    • Kundi la mwisho ni kundi la watu wanaofanya utapeli kwa njia ya mtandao kwa kutumia majina ya watu wengine vibaya ili kujipatia fedha.

    Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es salaam amesisitiza pia ifikapo jumatatu tarehe 5 Novemba, kila mtu ahakikishe kuwa hana picha chafu ya ngono katika simu yake kwa sababu zoezi hilo litaanza rasmi siku hiyo.

    Aidha nyumba zote zinazofanya biashara ya madanguro na kuchua (massage) wahakikishe kuwa wamesajiliwa na wanatumia wataalamu na kama hawafuati utaratibu basi watajulikana kuwa wanafanya biashara ya ngono.

    Makonda ameshukuru pia tangu atoe namba ya simu hapo jana ili watu watoe taarifa juu ya watu wanaojishughulisha na biashara hiyo tayari ana ujumbe 18,972 ambapo wote wanalaani vitendo hivyo.

    Hata hivyo Makonda amezionya na kutoa angalizo kwa mashirika ya haki za binadamu kuwa Tanzania ina tamaduni zake na ushoga ni kesi ya jinai kwa mujibu wa kifungu cha 154 ambacho kinasema mtu yeyote ambaye anamuingilia mtu yeyote kinyume cha maumbile au, anamuingilia mnyama kimwili au anamruhusu mwanaume kumuingilia yeye mwanaume au mwanamke kinyume cha maumbile,atakuwa ametenda kosa, na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha na wakati mwingine kifungo kisichopungua miaka thelathini .

    “Tayari nimepokea majina kadhaa ya watu maarufu katika biashara hiyo na kuna wengine ambao wameeleza kuwa walianza bila kutaka na wanataka kuacha ushoga,”

    na kuna ambao wanafanya biashara hiyo kwa hiari na kuna wale wanaowekewa vilevi na kufanyishwa biashara hiyo ambao wote watashughulikiwa”, Makonda aeleza.

    Na mwisho amesisitiza kuwa mapambano haya dhidi ya ushoga na biashara ya ngono sio yake peke yake bali ni ya watu wote .

  • Rais Magufuli atema cheche anguko la bei ya korosho

    Rais Magufuli atema cheche anguko la bei ya korosho

    Panda shuka za zao la korosho nchini  zimemvuta Rais John Pombe Magufuli na sasa ametishia tena kuchukua hatua kali.

    Siku chache zilizopita msimu mpya wa mauzo ya zao la korosho ulifunguliwa huku bei ya zao hilo zikishuka maradufu.

    Korosho ndio chanzo kikuu cha fedha na tegemeo la kiuchumi kwa wakazi wa mikoa ya kusini.

    Wakaazi hao kutokana na unyeti wa sekta hiyo waligomea bei mpya kati ya Sh1,900 mpaka Sh2,700 kwa kilo ikiwa ni anguko la kutoka wastani wa Sh4,000 kwa kilo msimu uliopita.

    Kutokana na hali hiyo, mbunge wa upinzani na kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo ambaye amekuwa mwiba kwa serikali ya Magufuli amewaambia waandishi kuwa serikali haiwezi kukwepa lawama.

    “Badala ya Serikali kulichukulia zao la korosho kama la kimkakati imekuwa haisikii, haielewi, na sasa imeharibu kuku anayetaga mayai ya dhahabu katika nchi yetu,” amesema.

    Jana hiyo hiyo Rais Magufuli alifanya kikao na wanunuzi wakuu wa zao hilo na kuwaeleza kuwa serikali inaunga mkono msimamo wa wakulima.

    Magufuli alienda mbali kwa kusema serikali yake ipo radhi kuzinunua korosho zote kwa bei inayowafaa wakulima na kuziuza katika masoko ya kimataifa nchini Marekani na Uchina.

    “…nipo tayari hata kutumia majeshi yetu kununua korosho na tutatafuta masoko ya uhakika ili tuuze kwa bei nzuri” amesisitiza Rais Magufuli.

    Hata hivyo, wafanyabiashara hao wamekubali kununua korosho kwa bei isiyopungua shilingi 3,000. Serikali pia imekubali kwa upande wake kuondosha baadhi ya tozo na vikwazo vilivyopelekea wafanyabiashara kushusha bei.

    Awali ilikuwa marufuku kwa korosho kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi kusafirishwa kupitia bandari nyengine isipokuwa ya Mtwara lakini serikali sasa imeruhusu kutumika kwa bandari ya Dar es Salaam pia.

    Kutoka bandari ya Dar, korosho husafirishwa kwa Sh47 kwa kilo kwa kutumia meli ambazo zimeleta mizigo mingine ikilinganishwa na bandari ya Mtwara ambako kilo moja inasafirishwa kwa shilingi 203/- kwa kutumia meli zinazokodiwa kwa ajili ya kubeba korosho tu.

    Mapema mwezi Mwezi Juni mwaka huu kulikuwa na mnyukano bungeni ambapo wabunge bila kujali tofauti zao za kisiasa walikuwa wakiyapinga mapendekezo ya serikali katika Sheria ya Fedha wa mwaka 2018 kwa kuchukua asilimia 100 ya tozo za mauzo ya korosho nje ya nchi (Export levy) kupelekwa mfuko mkuu wa fedha za serikali.

    Awali, asilimia 65 ya tozo hiyo ilikuwa ianenda kwenye mfuko wa zao hilo na baadae kurejeshwa kwa wakulima kupitia pembejeo. Hoja ya wabunge wakiongozwa na kamati ya bajeti ilikuwa, hatua ya kuchukua fedha zote ingeleta athari kubwa kwa maendeleo ya zao hilo na wakulima wake.

    Mjadala ukawa mkali lakini hoja ya serikali ikapita. Baadae, Rai John Magufuli akasema hakupendezwa na namna ya wabunge wa CCM hususani wa mikoa ya kusini kwa namna walivyolijadili suala hilo, na akatishia kuwa laiti wangeliandamana basi angetuma askari wawaadhibu.

    Baadhi ya wakosoaji akiwemo Zitto wanahusianisha kinachoendelea kwenye anguko la bei na hatua ya serikali ya kuchukua fedha zote za tozo za mauzo ya korosho nje ya nchi.

    “Mnaweza kuona fedha za kigeni tunazoenda kupoteza kwa uamuzi wa Serikali kuchukua fedha zote za export levy (ushuru wa forodha) badala ya kupeleka zinakostahili,” amesema Zitto.

    Msimu wa mwaka jana, serikali iliingiza kiasi cha dola 209 milioni za Marekani kutokana na zao la korosho.

     

    cc;bbc

  • Mizizi na asili ya nguli wa muziki duniani na visiwa vya Zanzibar

    Mizizi na asili ya nguli wa muziki duniani na visiwa vya Zanzibar

    Freddie Mercury

    Filamu mpya imeingia sokoni kuhusu bendi ya mziki ya Queen kutoka Uingereza, na macho yameelekezwa tena juu ya maisha ya muimbaji kinara wa bendi hiyo Freddie Mercury.

    Ushawishi wake jukwaani, mavazi, mizizi yake na kifo chake kutoana na maradhi yanayohusiana na ugonjwa wa ukimwi akiwa na umri wa miaka 45 mwaka 1991 ni kumbukumbu tosha za mwanamuziki huyo wa miondoko ya rock kuanzia miaka ya sabini na themanini.

    Kile ambacho wengi hawakifahamu na hakizungumziwi sana katika filamu ni kuwa alizaliwa katika visiwa vya karafuu vya Zanzibar kwenye familia ambayo asili yake ni India na Uajemi.

    Filamu hiyo mpya yajulikana kama Bohemian Rhapsody, the biography of Mercury.

    Haya ni mambo mambo unastahili kuyafahamu kuhusu Freddie Mercury na Zanzibar.

    Alizaliwa kama Farrokh Bulsara

    Mercury alizaliwa katika hospitali ya serikali huko Zanzibar tarehe 5 Septemba mwaka 1946. Wazazi wake Bomi na Jer Bulasara wana mizizi yao huko Uajemi lakini walikuwa pia wameishi nchini India.

    Nyumba familia ya Freddie Mercury walikuwa wanaishi Zanzibar

    Boni Bulsara alitokea huko Bulsar Gujarat (ndio maana familia ina jina hilo) na kuhamia Zanzibar kufanya kazi kwenye mahakama kuu kama karani wa serikali ya Uingerezea.

    Alimuoa Jer huko India na kumleta Zanzibar. Farrokh mtoto wao kifungua mimba alifuatwa miaka sita baadaye na binti yao, Karishma.

    Mercury mara nyingi hakuongeza hadharani kuhusu malezi yake huko Zanzibar.

    Waliishi kwenye nyumba nzuri iliyokuwa ikiangalia baharini kwenye mji wa Stone Town ambayo ni sehemu ya kihistoria ya mji wa Zanzibar.

    Leo hii mashabiki wake wanaweza kutembea sehemu alizokulia ikiwemo nyumbani kwake na mahakama ambapo baba yake alifanya kazi. Pia kuna mgahawa uitwao Mercury’s.

    Nyumba ya familia ya Freddie Mercury huko Stone Town
    Farrokh Bulsara alikulia kwenye mitaa ya Stone Town

    Suala tata kwa Wazinzibari wengi na wafuasi wa dini ya Zoroastria ambayo Mercury alikuwa mfuasi ni kuwa mwanamuziki huyo alikuwa ni shoga. Uislam ndio dini yenye wafuasi wengi Zanzibar na ngono ya jinsia moja iliharamishwa kisheria na kufanywa kosa la jinai mwaka 2004.

    Mwaka 2006, kundi moja la Wiaslamu lilizua tafrani baada ya kuenea kwa fununu kuwa kundi la watalii mashoga lilipanga kuzuru Zanzibar kusherehekea miaka 60 ya kuzaliwa kwa nguli huyo.

    Aligundua muziki akiwa mdogo

    Miaka ya kwanza ya masomo ya Mercury ni katika shule ya Wamishenari huko Zanzibar ambapo alifunzwa wa watawa wa Kianglikana. Lakini akiwa na umri wa miaka minane wazazi wake waliamua kumpleka shuleni huko India.

    Freddie Mercury (wa pili kushoto) na bendi ya Queen mwanzo wa miaka ya sabini

    Alisomea shule ya St Peter’s Church of England huko Panchgani kusini mashariki mwa mji wa Bombay (sasa Mumbai).

    Wakati akiishi na shangazi na mababu zake huko Bombay ndipo akagundua kuwa aliupenda muziki. Pia aliunda bendi yake ya kwanza ya Hectics.

    Familia yake ilikimbia mapinduzi

    Freddie alirejea kutoka Zanzibar 1963, mwaka ambao visiwa hivyo vilipata uhuru kutoka Uingereza na kumalizia masomo katika shule ya Kikatoliki ya St Joseph’s Convent School.

    Rafiki yake mmoja kutoka nyakati hizo anakumbuka jinsi walikuwa wakiogelea baharini baada ya kutoka shuleni na pia walivyokuwa wakiendesha baiskeli ufukweni sehemu za kusini.

    Ramani

    Lakini nyakati nzuri zilikuwa fupi. Mwaka 1964 mapinduzi yaliwatimua Waarabu waliokuwa wanatawala ambapo yakisiwa watu 17,000 waliuawa.

    Jamhuri ikaundwa na marais wa Zanzibar na Tanganyika, kwa kusaini mkataba wa umoja. Wakaunda Jamhuri ya Muungano Tanzania.

    Famialia ya Bulsara na wengine wengi wakakimbia visiwa hivyo.

  • Asa Mwaipopo na wakuu wa kampuni ya madini washtakiwa kwa uhalifu wa kiuchumi

    Asa Mwaipopo na wakuu wa kampuni ya madini washtakiwa kwa uhalifu wa kiuchumi

    Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya uchimbaji madini Tanzania Acacia Mining, Asa Mwaipopo amefikishwa mahakamani hii leo kwa mashtaka ya uhalifu wa kiuchumi.

    Mwaipopo mwenye umri wa miaka 55 alikamatwa hapo jana mjini Dar es salaam.

    Anajiunga na wengine sita ambao wanazuiwa tangu wiki iliyopita kwa makosa hayo akiwemo Deogratias Mwanyika aliyekuwa makamu wa rais wa kampuni ya Barrick Gold na mkurugenzi wa mawasiliano wa kampuni ya Bulyanhulu mine, na Alex lugendo mwenye umri wa miaka 41 ambao tayari wako rumande.

    Wanakabiliwa na mashtaka yakiwemo biashara haramu ya fedha, udanganyifu, na ukwepaji kulipa kodi.

    Mwaipopo alifikishwa mbele ya mahakama ya hakimu mkaazi ya Kisutu hii leo ambapo alishtakiwa kwa kupanga njama na maafisa wengine ndani na nje ya Tanzania na kughushi nyaraka kukwepa kulipa kodi.

    Acacia imekuwa katika mgogoro na serikali ya Tanzania, tangu serikali izuie usafirishwaji wa makinikia ya kampuni hiyo nje ya nchi.

    Serikali ya Tanzania pia imekuwa ikiishutumu kampuni ya Acacia kwa kukwepa kulipa kodi inayostahili, tuhuma ambazo kampuni hiyo mpaka sasa imekuwa ikizikanusha.

    Rais John Magufuli na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, Prof John Thornton katika mkutano wa nyuma

    Kwa mujibu wa Reuters, Acacia Mining ilithibitisha siku ya Jumatano wiki iliyopita kwamba mfanyakazi wao na aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni hiyo, walizuiliwa na taasisi ya kupambana rushwa Tanzania, ikiwa ni wiki moja baada ya kampuni hiyo kusema mfanyakazi mwingine ameachiwa kwa dhamana baada ya kushtakiwa kwa rushwa.

    Acacia, ambayo ni kampuni kubwa ya uchimbaji madini Tanzania imekuwa katika mzozo wa muda mrefu na serikali ambayo inaituhumu kampuni hiyo kwa kukwepa kulipa kodi. Acacia imekana kufanya makosa yoyote.

    Kampuni hiyo inamilikiwa na kampuni iliyopo Canada Barrick Gold.

    Mvutano wa Acacia Mining na serikali ?

    Serikali ya imeishutumu Acacia kwa kufanya kazi ya uchimbaji nchini Tanzania kinyume cha sheria na kusema kuwa makampuni ya uchimbaji madini yamekuwa yakikwepa kulipa kodi.

    Kutokana na tuhuma hizo kutoka kwa serikali, thamani ya hisa za kampuni ya Acacia ilishuka.

    Uchunguzi ulioamriwa kufanyika mwezi Machi mwaka jana ulibaini kuwa Kampuni ya uchimbaji Acacia imekuwa ikifanya kazi kinyume cha sheria.

    Mwenyekiti wa kamati ya wachumi na wanasheria Nehemiah Osoro iliyofanya uchunguzi huo alieleza.

    Kamati ilifanya uchunguzi kuhusu usafirishaji wa madini kwa kipindi cha miaka 19.

    Hisa za Kampuni ya Acacia ambayo inamilikiwa na Barrick Gold Corparation zilianguka kwa kiasi cha asilimia 15.

    Acacia imejitetea kuwa inafanya biashara zake kwa viwango vya juu na inafanya kazi kwa kufuata sheria za Tanzania ikiwemo kulipa kodi zote.

  • Jiwe lililotokana na ‘taa ya wachawi’

    Jiwe lililotokana na ‘taa ya wachawi’

    Kupiga picha kwenye kimondo cha Mbozi ni tukio la kipekee kwenye kivutio cha utalii kilichopo wilayani Mbozi, mkoa wa Songwe, Nyanda za Juu Kusini nchini Tanzania.

    “Wengi huwa wanafurahia kupiga picha kwa sababu ni kitu cha kipekee na tunaamini kuwa mtu akishapiga picha anakuwa balozi wa kimondo hiki kwa wengine,” anasimulia Beatus Bonabana, Mhifadhi, kivutio cha Kimondo Mbozi, anaongeza akisema.

    ‘Katika miaka ya nyuma, wenyeji wa eneo hilo walikuwa wanakitumia sehemu hiyo kwa ajili ya maombi ya kupata kitu, walifanya matambiko, ni jambo linaloendelea kufanyika mpaka leo.”

    Kimondo cha Mbozi kinakadiriwa kuwa na uzito wa tani 12 na ni cha nane kwa ukubwa duniani.

    Ni cha pili Afrika baada ya kimondo cha Hoba chenye tani 60. Kimondo cha Hoba kilichopo nchini Namibia ndicho kikubwa zaidi Afrika na duniani.

    Haijulikani ni lini hasa kimondo hiki cha Mbozi kilianguka, ila mtu wa kwanza kukiona katika miaka ya 1930 alijulikana kwa jina la Halele Simbaya, ambaye alikuwa mhunzi.

    Halele alipogundua kimondo hiki alitoa taarifa kijijini kwao, ndipo wenyeji wakaanza kuabudia katika shimo ambalo huwa linahifadhi maji ambayo wenyeji hunawa kupata baraka na wakalita jambo hilo kuwa ni kusafisha nyota.

    “Wenyeji walikuwa wanakatakata kimondo hicho, wakaita kipande cha nyota na hata sasa wenyeji wanakiita kimondo cha nyota. Watu walikata ili kusafisha nyota, ulinzi ulipowekwa ilisaidia,” Bonabana alieleza.

    Zamani kimondo hiki kilikuwa kinang’aa lakini sasa kimekuwa na rangi nyeusi baada ya kuathiriwa na hali ya hewa.

    Kimondo hiki hakifanani na chuma aina nyingine kutokana na ugumu wake na ukikipiga ni kama kuna uwazi ndani yake, unasikika mlio wa sauti ambao ni tofauti.

    Sauti inayoonesha kuwa ndani kuna uwazi na hii inatokana na madini ambayo yaliyokiumba.

    Imani kuhusu kimondo haipo miongoni mwa wenyeji hao wa Mbozi tu, bali sehemu mbali mbali duniani ambako vinapatikana.

    Wenyeji wake huhusisha zaidi na nguvu za Kimungu, hivyo kuyafanya maeneo vilipoangukia kuwa maeneo matakatifu kwa misingi ya imani zao.

    Mambo matatu kukihusu kimondo cha Mbozi

    • Kimondo cha Mbozi kinakadiriwa kuwa na uzito wa tani 12
    • Ni cha nane kwa ukubwa duniani
    • Cha pili Afrika baada ya kimondo cha Hoba chenye tani 60.
    • Inaaminika mtu wa kwanza kukiona katika miaka ya 1930 ni Halele Simbaya.
    • Hakipati joto la jua kali hata katika msimu wa kiangazi.

    Inaelezwa kuwa tangu zama za kale, vimondo viliaminika kuwa vitu vitakatifu na jamii mbali mbali za wakati huo duniani.

    Utaratibu wake wa kuanguka hapa duniani, ambapo huambatana na mwanga na sauti, kama vile nyota idondokayo, vumbi na kishindo imekuwa siku zote ikisababisha hofu kwa wale walioshuhudia.

    Sifa za kimondo cha Mbozi

    Kimondo hiki huwa ni baridi wakati wote, hata wakati wa msimu wa kiangazi ambapo jua huwa kali sana, lakini bado huwa cha baridi.

    Hiki ni kimondo kikongwe duniani kwa sababu hata hakijajulikana kilianza kuwepo hapo tangu lini tofauti na vimondo vingine duniani vinajulikana vilianguka lini (tarehe au mwaka) au kuonekana athari zilizosababishwa na kuanguka kwa kimondo hicho.

    Mfano kimondo kikianguka na kugongana na uso wa ardhi huwa kinaharibu makaazi ya watu au kama ni msituni miti pia huvunjika na kina tabia ya kujichimbia.

    Mfano kimondo kikubwa duniani ambacho kipo Namibia, kilipogonga uso wa ardhi kilijifukia.

    Sayansi na watafiti wanasema kimondo kikiwa na uzito wa zaidi ya tani 100 huwa kinalipuka na hufika duniani kikiwa vipande vipande.

    Kimondo cha Mbozi ndicho kikubwa kwa Tanzania, hata hivyo vipo vingine saba vidogo, hivi vinabebeka na vimehifadhiwa katika makumbsho ya taifa, Dar es salaam.

    Kwa nini Kimondo ni kivutio cha utalii?

    Kimondo ni kitu cha kipekee kwa sababu kimetoka nje ya anga ya dunia.

    Vitu hivi vimetokea sayari nyingine ya Mars na Jupita.

    Vitu hivi vimetokea katika mvuto wa jua na sayari zingine.

    ”Mfano mzuri wa kimondo ni vile tunavyoviona kama taa inayokimbia angani, vijijini huwa tunaita taa za wachawi wakati si kweli ni vimondo.

    Vile huwa ni vimondo vidogo vinavyoishia hewani na ndio mfano wa kimondo kama hiki,” anasimulia mhifadhi.

    Watalii wanaotembelea eneo hilo, ni wale tu wenye lengo la kukiangalia na kupiga picha, ambao hata hivyo sio wengi.

    Wadau wa utalii wanabainisha kuwa endapo eneo hilo litakuwa na kituo cha utafiti kuhusu masuala ya unajimu na makumbusho litakuwa eneo muhimu sana kwa watalii wa nje na ndani, hususani wanafunzi, hivyo kuwa kitovu cha elimu hiyo ya unajimu.

    Takwimu katika kituo hicho zinaonyesha kuwa wastani wa wageni wanaotembelea hapo ni kati ya 250 mpaka 350 kwa mwaka na wengi huwa ni wanafunzi.