Rais Kikwete Kukutana Na Ukawa Hivi Karibuni

Rais Kikwete Kukutana Na Ukawa Hivi Karibuni

Like
388
0
Wednesday, 27 August 2014
Local News

Jakaya-Kikwete

Rais Jakaya Kikwete anatarajia kukutana na viongozi wa Vyama vya Siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ili kuzungumzia mchakato wa Katiba wakati wowote wiki hii.
Katika mkutano huo, ambao unasubiriwa kwa hamu, Rais Kikwete atakutaka na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao unaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na CUF.
Aprili 16, mwaka huu wajumbe wa Ukawa na baadhi kutoka Kundi la 201, walisusia vikao vya Bunge hilo wakitaka msingi wa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba usibadilishwe, wakipinga uamuzi wa CCM kutaka kuingiza mfumo wa serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa katika Rasimu.
TCD inaundwa na vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni ambavyo ni CCM, CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi, UDP na TLP, huku vyama visivyo na uwakilishi bungeni vikiwakilishwa na UPDP kinachoongozwa na Fahmi Dovutwa.
Jana, kwa nyakati tofauti wenyeviti wenza wa Ukawa, Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR Mageuzi), walisema wako tayari kukutana na Rais, ila msimamo wao wa kutaka ijadiliwe rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kimekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa Ukawa kuomba wakutane na Rais Kikwete kwa ajili ya kujadiliana namna bora ya kuendesha mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari bungeni Dodoma jana, Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo alisema Rais atafanya kikao hicho wakati wowote ndani ya wiki hii na kwamba viongozi wa vyama wakiwamo wa Ukawa, wamethibitisha kushiriki.
Cheyo alisema, katika kikao walichokutana Dar es Salaam Agosti 23, wanachama wa TCD walikubaliana kwamba upo umuhimu wa kukutana na Rais Kikwete kwa mazungumzo na maridhiano.
Kukutana kwa viongozi hao, kunakuja huku wajumbe wa Bunge Maalumu wakiwa wamemaliza kujadili sura zote 15 zilizokuwa zimesalia na tayari baadhi ya kamati zimemaliza kupiga kura wakisubiri kuingia bungeni Septemba 2 kwa kazi ya kupigia kura sura kwa sura.
Kuhusu viongozi wa Ukawa, alisema wanazo taarifa na baadhi yao walikuwapo katika kikao cha kujadili kukutana na kiongozi huyo wa nchi, hivyo akasema lazima watashiriki wakati wowote wakiitwa.
Lipumba
Akizungumzia mkutano huo na Rais, Profesa Lipumba alisema: “Tunakutana na Rais Kikwete kwa sababu sisi ni wanachama wa TCD.” Alipoulizwa juu ya msimamo wa Ukawa, alisema lengo ni kutafuta mwafaka ili mchakato wa kupata Katiba Mpya uendeshwe kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
“Kikubwa tunachokitaka ni maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Warioba kuheshimiwa na siyo kuchukuliwa maoni mengine kama inavyofanyika sasa huko bungeni,” alisema Profesa Lipumba.

Mbowe
Mbowe alisema Katiba Mpya ni kwa masilahi ya Watanzania wote na Taifa lao, hivyo inapotokea mikutano kama hiyo na kwa hali ilivyo sasa, hakuna mtu mwenye nia njema atakayekataa kushiriki. Kikubwa ni kwamba hatuwezi kubadili msimamo wetu na huo ndiyo ukweli,” alisema.
Kuhusu Bunge hilo kupokea maoni ya makundi mbalimbali wakati tayari ukusanyaji wa maoni umeshafanywa na Tume ya Jaji Warioba, Mbowe alisema, “Ndiyo maana tulisusia vikao vya Bunge la Katiba, nadhani sasa Watanzania wamejua kwa nini tulitoka nje.”
Mbowe alisema kuwa mchakato wa Katiba unaendeshwa kwa mujibu wa sheria, lakini hivi sasa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samwel Sitta analiendesha Bunge hilo kinyume na sheria hiyo… “Ukusanyaji wa maoni unaofanyika sasa ni fedheha kwa CCM na Serikali, ni utoto na aibu wa CCM. Kwa sasa Ukawa tumetulia tunatazama hali inavyokwenda na tuna mipango yetu ambayo tunapanga. Kama hali ikiendelea kuwa hivi tutachukua uamuzi mgumu ili dunia nzima ijue.”

James Mbatia
Alisema wako tayari kukutana na Rais Kikwete kwa ushauriano kwa sababu suala la maridhiano ni la msingi na viongozi wote wa TCD walikubaliana Agosti 23.
“Mwaliko tumeupata na tutashiriki. Bunge linaweza kuendelea kwa taratibu zake za kisheria, lakini suala la mashauriano, lazima tukae tuangalie ni jinsi gani Taifa letu linaweza likavuka kwa maridhiano kwa amani na utulivu,” alisema.
Kauli ya Ikulu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu alisema Rais Kikwete yuko tayari kukutana na viongozi wa vyama vya siasa muda wowote… “Wao wafuate utaratibu tu, Rais hawezi kukataa kukutana nao na hilo amekuwa akilisema mara nyingi tu.”

 

 

Comments are closed.