Author: EFM

  • Wabunge Kenya watofautiana kuhusu matamshi ya ‘chuki’ ya Charles Kanyi ‘Jaguar’

    Wabunge Kenya watofautiana kuhusu matamshi ya ‘chuki’ ya Charles Kanyi ‘Jaguar’

    Matamshi ya mbunge wa Starehe nchini Kenya Charles ‘Jaguar’ Kanyi kuhusu kuwatishia raia wa kigeni wanaofanya kazi nchini Kenya yaliwasilishwa mbele ya kikao cha bunge ili kujadiliwa.

    Hatua hiyo inajiri huku Mbunge huyo akizuiliwa katika kituo cha polisi usiku kucha ambapo anasubiri kuwasilishwa mahakamani siku ya Alhamisi.

    Kulingana na mtandao wa runinga ya Citizen nchini Kenya, licha ya wabunge wengi kushutumu jinsi ambavyo bwana Jaguar alitoa hoja yake , baadhi yao walikubaliana kwamba kuna swala tata kuhusiana na raia wa kigeni ambalo lilihitaji kuangaziwa.

    Kulingana na mtandao huo swala hilo liliwasilishwa na mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Uhusiano wa kigeni Katoo Ole Metito katika taarifa yake, akithibitisha kwamba raia wa kigeni hususan kutoka Jumuiya ya Afrika mashariki wana uhuru wa kufanya biashara nchini Kenya.

    ”Tunashutumu sana matamshi yoyote ya chuki yanayokiuka msimamo huu unaotuleta sisi pamoja kama taifa na kuthibitisha sera ya kuwakaribisha raia wote wa kigeni”, alisema mbunge huyo wa Kajiado kusini.

    Matamshi yake yaliungwa mkono na mbunge wa Suba Kaskazini John Mbadi ambaye aliwarai wabunge wenzake kutotoa matamshi mbele ya umma kwa lengo la kujitafutia umaarufu na badala yake kuchukua tahadhari.

    ”Kama bara, tunahitaji kukuza uwiano katika mipaka yetu ili kutafuta ajira; Wakenya wako huru kwenda Tanzania kufanya biashara iwapo biashara hiyo ni halali”, alisema Mbadi.

    Hatahivyo kiongozi wa walio wengi bungeni Aden Duale, ambaye pia alishutumu matamshi hayo ya mbunge huyo wa Starehe alisema kwamba Kenya sio jaa la raia wa kigeni na bidhaa zao, kulingana na mtandao wa Citizen kenya.

    Kulingana na mbunge huyo wa Garissa mjini, Bunge pamoja na serikali zinafaa kuwalinda wananchi wa kawaida kutopoteza kazi kwa idadi kubwa ya raia wa kigeni waliomo nchini.

    Mbunge huyo alitaja mfano ambapo wataalam kutoka Kenya kama vile afisa wa kampuni ya Safaricom Sylvia Mulinge alinyimwa fursa ya kufanya kazi katika taifa jirani la Tanzania, akiongezea kuwa Kenya pia inafaa kutokubali maswala mengine.

    “Lazima ukweli usemwe; Unapoona biashara ya uchuuzi ikichukuliwa na raia wa taifa jingine tuna jukumu la kuwalinda watu wetu. Hawa wabunge hawafai kusahau kwamba kuku wetu walichomwa Tanzania , ng’ombe wetu walipigwa mnada Tanzania”, alisema Duale.

    ”Leo chini ya utawala uliopo Tanzania Wakenya hawawezi kufanya biashara, kwa nini bidhaa zetu haziingi Tanzania? Kwa sababu wametuwekea kodi ya juu”.

    Duale aliwataka wabunge kutolichukulia swala hilo na hisia, bali kuchukua tahadhari wanapochukua jukumu lao la kuwalinda raia wa kawaida.

    ”Kama bunge ni lazima tuamue na kuleta sheria zitakazolinda biashara zetu. Munaweza kumshutumu Jaguar, lakini leo ndiye mbunge maarufu zaidi katika eneo bunge lake”, aliongezea Duale.

    Nae mbunge wa Ugenya David Ochieng, kwa upande wake aliilaumu idadi kuu ya raia wa kigeni wanaofanya biashara nchini Kenya kwa kushindwa kwa serikali kuidhinisha sera yake.

    ”Katika uchumi wa leo , ni rahisi kununua bidhaa kutoka mataifa jirani kama vile Tanzania na Uganda na kuleta Kenya. Sio kwamba hatuna sheria, ni swala la utekelezwaji na ufisadi. Tunwaruhusu watu kuingia nchini na kuanza kuuza vitu barabarani. Huwezi kuwalaumu Watanzania kwa kufanya hivyo ni kwa sababu ya mfumo wetu ambao ni dhaifu”, alisema Ochieng’.

    ”Hatuwakagui watu wanaoingia nchini. Watanzania wanafanya kazi yao, ndio sababu wanaweza kujua kwamba Mulinge hakuhitimu kufanya kazi Tanzania.

    Hatahivyo Mbunge huyo alishutumu matamshi ya Jaguar , huku akilitaka bunge hilo kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wabunge wanaoharibu jina la taifa hilo katika ulingo wa kimataifa.

    Tayari ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai kupitia ukurasa wake wa Twitter imesema mbunge huyo anashikiliwa kwa tuhuma za kuchochea ghasia.

    Katika kanda ya video iliosambazwa pakubwa nchini Kenya na katika nchi jirani Tanzania, mbunge huyo alisema hawatokubali watu wa nje waje kuendesha biashara nchini humo.

  • Mambo muhimu ya kuhakikisha usalama wako mvua inaponyesha

    Mambo muhimu ya kuhakikisha usalama wako mvua inaponyesha

    Mvua kubwa imekuwa ikinyesha maeneo mengi Afrika Mashariki na kusababisha uharibifu wa mali na vifo.

    Nchini Kenya, watu zaidi ya 10 wamefariki baada ya kusombwa na maji ya mafuriko

    Wengi wao wamefariki wakisafiri kuelekea nyumbani au wakiwa kwenye magari wakijaribu kupitia maeneo yaliyofurika

    Je, unaweza kujikinga vipi hasa ukiwa safarini?

    Maafisa wa Mamlaka ya Taifa ya Usalama Barabarani (NTSA) pamoja na Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya wametoa ushauri ambao unaweza kukufaa sana wakati huu wa mvua.

    Fahamu kwamba wakati wa kiangazi, vumbi, mchanga na taka za aina mbalimbali hurundikana barabarani. Mvua inaponyesha, husababisha barabara kuwa telezi na kwa hivyo ukiwa na gari ni muhimu kutoendesha gari lako kwa mwendo wa kasi kupindukia kwani gari likiteleza utashindwa kulidhibiti gari lako kwa urahisi.

    Kwa sababu ya maji, huwa vigumu sana kupiga breki wakati wa mvua na hivyo hatari ya mwenye gari kumgonga anayetembea barabarani huwa juu. Unashauriwa kutoendesha gari kwa mwendo wa kasi.

    Kwa sababu ya mvua, wapita njia mara nyingi hutembea wakiwa wameinamisha vichwa chini na huenda wasilione gari linapokaribia. Wenye magari wanashauriwa kuwa makini zaidi wanapofika kwenye vivuko barabarani au wanapomuona mtu akivuka barabara. Kwa wanaotembea kwa miguu, wanashauriwa kutumia vivuko vilivyotengwa na kuchukua tahadhari zaidi pia.

    Kwa wenye magari, iwapo barabara imefurika maji, ni vyema kutafuta barabara nyingine ya kupitia badala ya kujaribu kupitia ndani ya maji. Huwa vigumu kukadiria kina cha maji barabara inapofurika.

    Wakati mvua inaponyesha, wenye magari wanatakiwa kuwasha taa kuwawezesha kuona mbele na pia kutokaribia sana magari yaliyo mbele yao. Maji yanayorushwa na gari lililo mbele yanaweza kutatiza mwenye gari iwapo atakuwa karibu sana. Ushauriwa kufuata kanuni ya sekunde 3, hicho ndicho kipindi kinachochukuliwa na binadamu kuona jambo na kuchukua hatua. Usipofanya hivi, kufikia wakati unapoona aliye mbele yako amesimama na kuchukua hatua utakuwa tayari umesababisha ajali.

    Breki za gari huathiriwa na maji, kwa hivyo unapoendesha gari eneo lenye maji, ni vyema kuendesha gari kwa mwendo wa polepole. Hii itaziwezesha breki kukauka.

    Madereva wanashauriwa pia kutumia mikono yao miwili kudhibiti mwelekeo wa gari kuhakikisha wanadhibiti vyema gari.

    Wapita njia, waendesha baiskeli na waendeshaji pikipiki wanashauriwa kuvalia mavazi yanayoweza kuonekana vyema au mavazi yanayoweza kuakisi mwanga. Haya yatamuwezesha mtu kuonekana na madereva na kumpungushia mtu hatari ya kugongwa.

    Usiendeshe gari lako ndani ya maji yanayosonga, yawe kwenye mifereji au kwenye mto. Huwa vigumu sana kukadiria nguvu ya maji. Magari mengi husombwa na maji madereva wakijaribu kuvuka mito au wakitumia madaraja yaliyofurika maji. Mvua pia hudhoofisha madaraja, jambo ambalo huenda usifahamu. Daraja linaweza kubomolewa bila ufahamu wake wewe nawe ukaingia mtoni ukitarajia daraja bado lipo. Maji ya kina ya futi moja yanaweza kusomba gari lako. Kwa binadamu anayetembea, inchi sita za maji zinaweza kukusomba.

    Ukiwa na gari lako, hakikisha vipangusia kioo vya gari lako vinafanya kazi. Hili litakuwezesha kupangusa kioo na kuona mbele unapokuwa barabarani.

    Iwapo una gari na limeanza kuteleza, achilia mafuta na kulielekeza gari upande ambao unateleza. Ukianfanikiwa kudhibiti gari, anza kulainisha magurudumu tena na kurejea barabarani. Hakikisha kwamba unabaki kuwa tulivu na usichukue hatua yoyote ghafla.

    Usiende kwa mwendo wa kasi. Iwapo una safari ya mbali, anza mapema kuhakikisha kwamba haukumbwi na shinikizo la kutaka kwenda kwa kasi ndipo ufike.

    Unapokuwa unaendesha gari, usishawishike kutumia simu yako au kufanya jambo lolote ambalo litakuzuia kuwa makini ukiliendesha gari.

    Iwapo utakuwa safarini, usiegeshe gari lako au kuanza kufanya shughuli zako karibu na mto wakati wa mvua.

    Ni vyema kusikiliza vituo vya redio na runinga kujifahamisha kuhusu yanayojiri na ni wapi mvua kubwaimenyesha au mafuriko kutokea.

    Usitembee kwenye maji au maeneo yenye matope ambayo kuna uwezekano kwamba kuna nyaya za umeme ambazo zimeanguka. Nyumba yako ikifurika maji pia, hakikisha umezima stima.

    Iwapo unatembea kwa miguu, tumia fimbo au kijiti kukadiria kina cha maji.

    Mafuriko yakitokea eneo ulipo, mara moja kimbilia maeneo yaliyo juu na salama.

     

  • SASA SUGU HURU !

    SASA SUGU HURU !

    Mbeya. Viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti, Freeman Mbowe waliokwenda Gereza Kuu la Ruanda mkoani Mbeya kuwalaki Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga wamepigwa butwaa baada ya kuelezwa na askari magereza kwamba wameshatoka.
    Wakiwa nje ya gereza leo Mei 10, 2018, viongozi hao walifuatwa na askari na kuelezwa kwamba wawili hao wameshatoka.
    Magari mawili ya polisi yaliyokuwa yameimarisha ulinzi gerezani hapo nayo yaliondoka.
    Happiness Msonge, mkewe Sugu akizungumza na MCL Digital amesema walipigiwa simu na kuelezwa kwamba wameshatoka na wako njiani wakielekea nyumbani.
    Baadhi ya viongozi waliokuwepo ni mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda, Meya wa Jiji la Mbeya, Mchungaji David Mwashilindi na madiwani.
    Viongozi hao walianza kufika gerezani leo Mei 10, 2018 saa 12:45 asubuhi na kuingia ndani ya uzio wa gereza ambako askari waliwaondoa.
    Sugu na Masonga walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano jela Februari 26 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli kwenye mkutano wa hadhara walioufanya Desemba 30 mwaka jana eneo la Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.
    Wawili hao wameshatumikia adhabu hiyo kwa siku 73 ikiwa ni zaidi ya robo ya kifungo chao

  • Tetesi za soka Ulaya Alhamisi 10.05.2018

    Tetesi za soka Ulaya Alhamisi 10.05.2018

    Mshambuliaji wa Paris St-Germain , 26, alifanya mazungumzo ya siri na Real Madrid mnamo mwezi Machi. Mchezaji huyo wa Brazil amedaiwa kutaka kuondoka mjiini Paris(AS, via Express).

    Mabingwa wapya wa ligi ya mabingwa Wolvehampton ambao wamepandishwa daraja katika ligi kuu ya Uingereza ni miongoni mwa wanaopigiwa upatu kumsaini mshambuliaji wa Everton Wayne Rooney, 32, mwisho wa msimu huu(Birmingham Mail)

    Lakini Rooney hatatoa uamuzi wa iwapo atasalia katika uwanja wa Goodison Park hadi pale hatma ya mkufunzi Sam Allardyce itakapoamuliwa(Star).

    Klabu ya ligi ya Marekani ya DC United ina matumaini kwamba inaweza kumshawishi mfungaji huyo wa mabao mengi nchini Uingereza kujiunga nao(Washington Post)

    Arsenal imempatia kiungo wa kati Jack Wilshere, 26, mkataba mpya wa miaka mitatu ikiwemo kuongeza mkataba huo kwa miezi 12 na hivyobasi kumzuia mchezaji huyo katika uwanja wa Emirates hadi 2022. (Mirror)

    The Gunners wameanza mazungumzo ya kumsajili kipa wa Bayer Leverkusen Bernd Leno, 26, kuchukua mahala pake Petr Cech. (Bild, via Express)

  • Malaysia yapata kiongozi mkongwe zaidi duniani aliyechaguliwa

    Malaysia yapata kiongozi mkongwe zaidi duniani aliyechaguliwa

    Dr.Mahathir Mohamad aibuka mshindi akiwa na miaka 92

    Waziri mkuu wa zamani wa Malaysia Dr.Mahathir Mohamad amepata ushindi wa kihistoria katika uchaguzi mkuu uliofanyika katika hilo. Kiongozi huyo ameweza kukiangusha chama ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 1957 ambacho kimekuwa kikidaiwa kujihusisha na nasuala ya rushwa na ufisadi.

    Dr.Mahathir ameshinda kwa idadi ya uwingi kura,na kukibwaga chama cha Barisan Nasional kilichotawala kwa zaidi ya miaka 60.

    Akiwa na umri wa miaka 92 Mhathir ameachana na kuitwa mstaafu na amerejea tena kuchukua nafasi ya mfuasi wake huyo wa zamani yaani Najib Razak ambaye utawala wake umekuwa na shutma kadhaa za rushwa.

    Ibrahim Suffian, ni mtafiti wa masuala ya uchaguzi wa kujitegemea wa mjini Kuala Lumpur,anasema matokea haya yameleta mmshituko mkubwa.

    “Tupo hapa tumekumbwa na mshangao kutokana na matokeo haya,ni jamba ambalo halikutarajiwa na ilikuwa vigumu sana kuweza kujua nani atabiri nani mshindi kwa kadri kura zilivyokuwa zikiendelea kuhesabiwa.”Ibrahim

    Malaysia katika utawala uliopita imeshuhudia kupanda kwa gharama za maisha na ongezeko la visa vya utengano wa kikabila,jambo ambalo Ibrahim Suffian anasema Dr Mahatir aliweza kuleta ushawishi mkubwa kwamaba anaweza kuleta mageuzi.

    “Nafikiri jambo hili,na kufanikiwa kutekeleza mambo kadhaa yanayoonekana kuwa kikwazo.Jambo la kwanza ataunda muungano unaoshirikisha vyama vingine vya upinzani,na mbili nafikiri amewezakuwa na ushiwishi mkubwa kubainisha matatizo ya kisiasa ambayo yamekuwa yakiikabili Malaysia kwa takribani miaka 60 iliyopita,kama masuala ya kodi na mikasa ya rushwa ambayo ilimhusisha hata waziri mkuu pia.”

    Najib Razak kashindwa na mengi kwani pia anahusishwa na kashfa ya kudaiwa kujipatia kiasi cha dola 700 kutoka taasisi moja ya maendelea ya Malaysia na mamlaka zinaendelea kuchunguza kashfa hiyo.

    Kufuatia ushindi wa Dr Mahathir, serikali imetangaza mapumnziko ya siku mbili ya kitaifa kwa siku ya Alhamis na Ijumaa.

     

  • Marekani yajiondoa katika mpango wa nyuklia wa Iran

    Marekani yajiondoa katika mpango wa nyuklia wa Iran

    Viongozi wa mataifa ya magharibi wanasema kuwa wataendelea kuuunga mkono makubaliano ya kinyuklia ya Iran muda mfupi baada ya Marekani kutangaza kuwa inajiondoa katika makubaliano hayo.
    Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zinasema kuwa watafanya kazi pamoja na matiafa yote yaliosalia katika mkataba huo huku ikiitaka Marekani kutovuruga utekelezwaji wake.
    Mataifa mengine yalioweka mkataba huo wa 2015- Urusi na China pia yamesema yataendelea kuunga mkono makubaliano hayo.

    Iran imesema kuwa inafanya kazi kunusuru makubaliano hayo bila ya ushirikiano wa Marekani.
    ”Mataifa yetu yataendelea kuunga mkono makubaliano hayo na yatafanya kazi na mataifa yanaoendelea kuunga mkono mkataba huo”, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa zilisema katika taarifa ya pamoja.
    Siku ya Jumanne rais wa Iran Hassan Rouhani alisema: “Nimeagiza wizara ya maswala ya kigeni kujadiliana na mataifa ya Ulaya ,China na Urusi katika majuma yajayo”.
    ”Iwapo tutaafikia malengo ya makubaliano haya kwa ushirikikiano wa wanachama wengine basi makubaliano hayo yataendelea kuheshimiwa”.
    Mkakati wa pamoja uliizuia Iran kuendelea na mpango wake wa kinyuklia huku Umoja wa mataifa ukikubali kuiondolea vikwazo Iran vilivyowekwa pamoja na, Marekani na bara Ulaya.

    Katika taarifa katika runinga ya taifa siku ya Jumanne , rais alisema kuwa Marekani itajiondoa katika mkakati huo wa pamoja JCPOA.
    Aliutaja kuwa mkataba mbaya unaopendelea upande mmoja ambao haungewahi kuafikiwa.

  • SIRRO CUP KUANZA KUTIMUA KIBITI

    SIRRO CUP KUANZA KUTIMUA KIBITI

    Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akimkabidhi mpira mmoja wa Viongozi wa timu zinazoshiriki mashindano ya Sirro Kibiti mwaka 2018 katika uwanja wa Samora Kibiti wakati wa uzinduzi wa michezo hiyo uliofanyika jana. Mashindano hayo yanashirikisha timu 16 kutoka Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji.
    Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akisalimiana na wachezaji wa timu ya mpira wa miguu ya Migomba kutoka Wilayani Rufiji wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Sirro Kibiti mwaka 2018 katika uwanja wa Samora Kibiti. Mashindano hayo yanashirikisha timu 16 kutoka Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji.
    Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akiwasalimu wakazi wa Kibiti wakati wa Sherehe za ufunguzi wa mashindano ya Sirro Kibiti mwaka 2018 katika uwanja wa Samora Kibiti. Mashindano yanayoshirikisha timu 16 kutoka Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji.

     

     

     

     

  • Serikali ya muungano wa vyama yashindikana Italia

    Serikali ya muungano wa vyama yashindikana Italia

    Mazungumzo ya muungano wa vyama nchini Italia yameshindikana,hivyo kuiacha nchi ikitakiwa kufanya uchaguzi mpya ama kuwa na serikali ya mpito hadi mwishoni mwa mwaka huu.
    Rais Sergio Mattarella amesema mazungumzo hayo ilikuwa ndiyo tegemeo la kulifikisha taifa hilo kwenye makubaliano kufuatia vyama vyote vilivyoshiriki uchaguzi mkuu mwezi machi kutofanikiwa kupata ushindi. Hakuna chama chochote binafsi kilichopata kura za kukiwezesha ushindi kama chama.
    Hata hivyo vyama viwili maarufu vya Five Star na The League,ndivyo vinavyochuana kwa karibu.
    Mazungumzo hayo yaliyoshindikana yalikuwa na lengo kuunda serikali ya muungano,japo kuwa chama kikuu cha kilipinga hatua hiyo ya ama kuungana na chama chama cha mrengo wa kulia ama ule wa kushoto.

    Akizungumza siku ya jumatatu kwa njia ya televisheni rais Mattarella alitoa rai kwa viongozi wa vyama kunga mkono serikali huru isiyoegemea upande wowote na hasa baada ya kushindikana kuundwa kwa serikali ya muungano wa vyama na kusisitiza kwamba hawawawezi kuendelea kusubiria bila ya kuwa na serikali.

    Mattarella ameongeza kuwa serikali hiyo hiyo isiyofungamana na upande wowote wa vyama,ndiyo iwe na jukumu la kuandaa bajeti yam waka 2019 ili kuliepusha taifa hilo kushuka kiuchumi.
    Serikali hiyo ya mpito itaendesha taifa hilo hadi mwishoni mwa mwaka,na kisha baadaye kufikia ukomo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2019.
    Hadi sasa si chama cha Five Star movement ama The League ambacho kimeonyesha uungaji mkono mawazo.

  • Kero la uhaba wa maji kwa wakaazi Nairobi licha ya mvua kubwa.

    Kero la uhaba wa maji kwa wakaazi Nairobi licha ya mvua kubwa.

    Mji wa Nairobi umekumbwa na ukosefu mkubwa wa maji. Wakaazi wengi wa jiji hulazimika kununua maji kwa bei ghali kutoka kwa wachuuzi. Hali hii inaendelea licha ya mvua kubwa inayoendea kunyesha.
    Katika eneo la Rongai nje kidogo ya mji mkuu Nairobi, mmoja wa wakaazi wa eneo hili anaeleza jinsi imekuwa vigumu kapata maji.
    ”Nimeishi mtaa huu tangu miaka ya 80 na mpaka sasa, hatujawahi kuona tatizo kubwa la maji kama hili. Shida ya maji ni kubwa kiasi kwamba kutoka mwezi Januari mwaka huu, hutajapata hata tone la maji kutoka kwenye mabomba ya kampuni ya Nairobi water. Sasa imetubidi kutegemea wauzaji wenye visima kutuletea maji.”

    Bwawa la Ndakaini eneo la Murang’a katikati mwa Kenya lina ukubwa wa ekari 600.
    Kiwango cha maji kimepunngua katika bwawa hili kufuatia msimu mrefu wa kiangazi katika miaka michache iliyopita na hata mvua kubwa inayoendela kunyesha nchini haijabadili hali kwenye bwawa na hili limewaacha wengi na maswali.
    Mvua hiyo imewaacha karibu watu nusu milioni kupoteza makaazi yao nchini.

    Licha ya hayo kampuni ya kusambaza maji mjini Nairobi inadai kuwa eneo la sehemu ya chemichemi ya Aberdare haina maji ya kutosha, Meneja wa Mawasiliano wa kampuni hiyo akidai imewabidi kuanzisha mradi wa ugavi wa maji kukithi mahitaji.

    Mbaruku Vyakweli ni meneja wa mawasiliano, Nairobi Water, anasema, ”Kwa bahati mbaya viwango vya maji vimekuwa vikipungua.Vimekuwa vikipungua kwa mwaka mmoja sasa.
    Tulibuni mpango wa ugavi wa maji. Mradi huo unahakikisha kuwa tunasambaza maji yaliyoko kwa wateja wetu wote kwa usawa jijini Nairobi. Hatujakuwa na mvua ya kutosha.”

    Tunaamua kwenda juu zaidi mlimani ili kutafuta majibu. Bwawa la ndakaini hupokea maji kutoka mito mitatu ambayo chanzo chake ni milima Abadare .
    Kiwango cha maji kimepungua. Kipimo kilichowekwa kando ya mto huu kikiashiria upungufu huo.
    Lakini kilomita chache tu kutoka Ndakaine hali ni tofauti kabisa. Katika mto Chania ambao pia chanzo chake ni milima Abadare , maji yanatiririka kwa kasi na viwango kuongezeka maradufu.
    Lakini Gavana wa County hii ya Murang’a hakubaliani na maelezo ya kampuni ya kusambaza maji ya Nairobi.

    ”Ukitazama mto wa Chania kwa mfano,ni ushahidi wa kutosha kuwa mvua inanyehsa katika chemichemi ya Abardare.Kwa hivyo ni wao watueleze nini kinaendelea.Je inawezekana kuwa kuna mtu ambaye hachungi bwawa inavyofaa na labda inavuja?Mimi si mtaalama but nashuku tu.” anasema Gavana Mwangi Wairia.

  • Barcelona yatoshana nguvu na Madrid El Clasico

    Barcelona yatoshana nguvu na Madrid El Clasico

    Mchezo wa pili wa El Clasico kati ya mahasimu Fc Barcelona na Real Madrid kwa msimu wa La Liga wa 2017/2018 uliopigwa katika dimba la Camp Nou ulimalizika kwa sare ya kufungana magoli 2-2.
    Mshambuliaji wa Barcelona Luis Suarez, ndio alianza kuipatia timu yake goli la kuongoza katika dakika ya kumi, ya mchezo, iliwachukua dakika nne kwa Madrid kusawazisha goli hilo kupitia kwa nyota wake Cristiano Ronaldo.
    katika dakika ya 52, mshambuliaji Lionel Messi, aliipatia klabu yake goli la pili baada ya kuihada ngome ya ulinzi ya Real Madrid, Nyota toka Wales, Gareth Bale, alifunga goli la kusawazisha katika dakika ya 72 ya mchezo.

    Barcelona walicheza pungufu ya mchezaji mmoja katika mchezo huo baada ya Sergi Roberto, kutolewa kwa kadi nyekundu, na klabu hiyo imendeleza rekodi yake nzuri ya kutopoteza mchezo hata mmoja katika msimu huu.

    Lionel Messi anaongoza kwa ufungaji katika la Liga akiwa katupia kambani magoli 33 mpaka sasaHaki miliki ya pichaREUTERS
    Image caption
    Lionel Messi anaongoza kwa ufungaji katika la Liga akiwa katupia kambani magoli 33 mpaka sasa
    Mchezo wa pili wa El Clasico kati ya mahasimu Fc Barcelona na Real Madrid kwa msimu wa La Liga wa 2017/2018 uliopigwa katika dimba la Camp Nou ulimalizika kwa sare ya kufungana magoli 2-2.
    Mshambuliaji wa Barcelona Luis Suarez, ndio alianza kuipatia timu yake goli la kuongoza katika dakika ya kumi, ya mchezo, iliwachukua dakika nne kwa Madrid kusawazisha goli hilo kupitia kwa nyota wake Cristiano Ronaldo.
    katika dakika ya 52, mshambuliaji Lionel Messi, aliipatia klabu yake goli la pili baada ya kuihada ngome ya ulinzi ya Real Madrid, Nyota toka Wales, Gareth Bale, alifunga goli la kusawazisha katika dakika ya 72 ya mchezo.

    Barcelona walicheza pungufu ya mchezaji mmoja katika mchezo huo baada ya Sergi Roberto, kutolewa kwa kadi nyekundu, na klabu hiyo imendeleza rekodi yake nzuri ya kutopoteza mchezo hata mmoja katika msimu huu.

    Tayari Barcelona, ni mabingwa wa La Liga msimu huu wakiwa na alama 87, na wanasaliwa na michezo mitatu huku Madrid, wakiwa na alama 72 katika nafasi ya tatu na wakisaliwa na michezo miwili kabla ya ligi kumalizika.
    Atletico Madrid walioko nafasi ya pili wakiwa na alama 75, wakicheza katika uwanja wao wa Wanda Metropolitano, walikubali kichapo cha magoli 2-0 Espanyol.
    katika michezo mingine Las Palmas, walifungwa nyumbani na Getafe, kwa goli 1-0 na Alaves wakawatambia Malaga, kwa kuwachapa kwa magoli 3-0.

  • Putin kuapaishwa kwa muhula wa nne kama rais wa Urusi

    Putin kuapaishwa kwa muhula wa nne kama rais wa Urusi

    Vladimir Putin anatarajiwa kuapishwa kwa muhula wa nne kama rais wa Urusi leo Jumatatu baada ya kushinda uchaguzi mnamo Machi.
    Amekuwa madarakani kwa miaka 18 kama rais na hata waziri mkuu, na wapinzani wameufananisha muda wake wa uongozi kama utawala wa mfalme.
    Polisi wa kupambana na fujo walikabiliana na waandamanaji wanaopinga utawala wake mjini Moscow na katika miji mingine Jumamosi.
    Kumekuwa na hofu kwamba huenda kutazuka ghasia tena leo Jumatau wakati anapoapishwa.
    Sherehe hiyo ya kuapishwa kwake itafanyika Kremlin mjini Moscow na huedna ikawa na ya watu wa karibu tu ikilinganishwa na ile ya mwaka 2012, shirika la habari la AFP Linaripoti.
    Putin anatarajiwa kukutana na watu waliojitolea kushughulika wakati wa kampeni yake peke, shirika hilo la habari linasema.

    Rais wa kwanza aliyechaguliwa mnamo mwaka 2000, Putin aliwania tena muhula mwingine mnamo mwaka 2004 kabla ya kujiuzulu 2008 ili kuhudumu kama waziri mkuu chini ya mshirika wake Dmitry Medvedev, kwa sababu kisheria, anaruhusiwa kuhudumu kwa mihula miwili pekee mtawalia.
    Ilikuwa wazi ni nani aliye na udhibiti na mwaka 2012 Putin alirudi kama rais, kwa mara hii kwa muhula wa miaka sita.
    Iwapo na atakapofika mwisho wa muhula wake wa nne mwaka 2024, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 65 atakuwa amehudumu kwa takriban robo karne madarakani.

    1952: Alizaliwa Octoba 7 huko Leningrad mji wa pili kwa ukubwa Urusi, akasomea Sheria na kujiunga na Polisi ya KGB akiwa jasusi katika Ujerumani mashariki iliyokuwa na Ukomyunisti
    1997: Baada ya kuhudumu kama msaidizi mkuu wa meya wa St Petersburg, akaingia ikulu chini ya Boris Yeltsin akateuliwa kuwa mkuu wa kitengo cha polisi FSB
    1999: Alichaguliwa kuwa waziri mkuu , na kuwa kaimu rais baada ya Yeltsin kujiuzulu.
    2000: Alichaguliwa Rais na kuhudumu mihula miwili ya miaka minne.
    2008: Alizuiwa kuhudumu kwa muhula wa tatu mtawalia, akawashangaza wachambuzi kwa kurudi katika wadhifa wa waziri mkuu huku mshirika wake Dmitry Medvedev akiwa rais
    2012: Achaguliwa tena rais na kwa muhula wa miaka sita, chini ya sheria mpya
    2018: Achaguliwa kwa muhula wa nne

    Warusi wa kawaida wamekaribisha utulivu unaotajwa kutokana na miaka ya kwanza ya uongozi wa Puti wakati mfumko wa bei ulidhibitiwa na idara msingi za serikali zilipofufuliwa.
    Ghasia za kutaka kujitenga zilizogubika utawala wa kiongozi aliyemtangulia Putin, Boris Yeltsin, hatimaye zilisitishwa kwa umwagikaji damu mkubwa.

    Umairi wake uliozidi ,uliochochewa na ushuru kutoka kwa mafuta gafi na gesi , Bw Putin aliongeza umairi wake uongozini na kusababisha vituo vya habari kurudia nyakati za kale pia uhuru wa kisiasa.
    Uamuzi wake wa kuihamisha rasi ya annex Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014 ulizua mgogoro mkubwa tangu vita baridi , na kusababisha vikwazo vinavyoendelea kutoka Magharibi hadi sasa.
    Urusi inadaiwa kuingililia kati uchanguzi wa urais wa Marekani 2016 uliozua utata katika mahusiano ya kimataifa.
    Mwaka huu Bw Putin aliitupiwa kidole cha lawama na Uingereza kwa shambulio la kemikali kwa jasusi wake – madai ambayo aliyapinga Moscow.