Author: EFM

  • Mwanaharakati wa Rwanda awa mmoja kati ya wanawake 10 mashuhuri duniani

    Mwanaharakati wa Rwanda awa mmoja kati ya wanawake 10 mashuhuri duniani

    Wanawake hao wanajifunza kukubali yaliyawatokea wakati wa vita vya kimbari

    Mwanaharakati wa maswala ya wanawake nchini Rwanda Godelive Mukasarasi amewekwa kwenye orodha ya wanawake 10 mashuhuri duniani.
    Tuzo aliyopewa na Marekani Bi Godelive Mukasarasi inatokana na juhudi za shirika aliloanzisha nchini Rwanda la SEVOTA kusaidia wakinamama walionusurika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
    Amewekwa kwenye orodha hiyo na nchi ya Marekani ambao hivi karibuni walitunukiwa tuzo ijulikanayo kwa jina”International women of Courage ” kutokana na shughuli za shirika lake la SEVOTA ambalo husaidia wanawake waliobakwa wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda pamoja na watoto waliozaliwa kutokana na kitendo hicho.
    Shirika hilo limekuwa likisaidia wakinamama hao kujijenga kimaisha, kupokea yaliyowapata na kuwapa upendo watoto waliozaa kwa namna hiyo.

    Shirika hilo aliloanzisha limeweza kukusanya watu wasiopungua elfu 10 ambao ni wanawake wajane wa mauaji ya kimbari na watoto yatima.
    Kadhalika tuzo aliyopewa ni baada ya kile kilichotajwa kuwa juhudi zake kupigania kosa la ubakaji kuwa miongoni mwa makosa ya uhalifu wa kivita.

    “Ni kweli kwamba mwaka 96 Rwanda ilipotunga sheria ya kuadhibu waliofanya mauaji ya kimbari,tulipaaza sauti wanaharakati wote wa akinamama pia kwa msaada wa wabunge wanawake wote walisimama kwa kauli moja kwamba waliofanya makosa ya ubakaji lazima wawekwe katika ngazi ya kwanza ya wauwaji wanaohukumiwa adhabu kali” alieleza Mukasarasi
    Wakinamama hao husaidiwa kujikimu kimaisha wakifanya kazi katika mashirika mbali mbali, lakini kubwa zaidi ni ushauri nasaha wa jinsi ya kukabiliana na matatizo yaliyowapata wakati wa mauaji ya kimbari na kuwaonesha upendo watoto wao waliozaa wakati wa kubakwa.

     

     

  • Zuckerberg akiri kosa lake na kuomba radhi

    Zuckerberg akiri kosa lake na kuomba radhi

    Mkurugenzi Mtendaji wa Facebook Mark Zuckerberg ametoa maelezo katika Bunge la Marekani- Congress kwa mara ya kwanza Jumanne, akijibu wasiwasi ulioelezwa na wabunge juu ya kushindwa kwa mtandao wa jamii maarufu kulinda taarifa zao.
    Taarifa hizo za siri za watumiaji wanaofikia milioni 87 ulimwenguni zilizotumiwa na kampuni yenye kujishughulisha na siasa- Cambridge Analytica iliyokuwa na mafungamano na Trump.

    Mahojiano hayo yanaendelea Jumatano wakati Zuckerberg atakapokutana katika raundi ya pili kujibu maswali mbele ya jopo la Wabunge wa Marekani.

    Mkurugenzi huyo Mark Zuckerberg amekiri kuwa :”Hilo lilikuwa kosa kubwa na ni kosa langu mimi mwenyewe na naomba radhi. Nilianzisha matandao wa Facebook, niliusimamia na nina wajibika kwa kitu chochote kinachotokea.”

    Wachambuzi wanasema ni kosa ambalo liliruhusu kampuni ya kisiasa ya Cambridge Analytica kupata taarifa kwa kupitia programu iliyotengenezwa na kampuni nyingine, ambayo ili ingilia taarifa binafsi za mamilioni ya wanaotumia Facebook duniani.

    Marc Rotenberg wa kituo cha kutunza taarifa za siri za kielektroniki amesema: “Ni suala nyeti kwa Facebook kwa njia nyingi. Kuhakikisha bei ya hisa zao zinanyanyuka, watu wana wasiwasi mkubwa juu ya mustakbali wa kampuni hiyo. Lakini nafikiri vipi Facebook itaweza kuendelea kufanya shughuli zake kama ilivyo kwani ni suala la wazi. Nafikiri mjini Washington na maeneo mengine, utashuhudia shinikizo la kuwepo mabadiliko ya kweli.

    Mabadiliko yaliyoanza katika mahojiano yasiyo ya kawaida kabisa yakiendeshwa na nusu ya Baraza la Seneti ya Marekani.

    Seneta Richard Durbin (Mdemokrati) alimuuliza Zuckerberg: “Je, uko radhi kutuambia jina la hoteli uliofikia jana usiku?” “Um, uh, hapana,” alijibu Zuckerberg.

    Seneta Durbin : “Kama ulituma ujumbe kwa mtu yoyote wiki hii, unaweza kutujulisha majina ya watu hao uliowasiliana nao?’

    “Seneta, hapana, pengine sitopendelea kufanya hivyo hadharani hapa,” alijibu mkurugenzi huyo wa Facebook.

    “Nafikiri pengine hilo ndio suala zima. Haki yako ya kutoingiliwa maisha yako binafsi.”

    Hata hivyo Zuckerberg ameahidi mabadiliko. Amesema iwapo tutagundua kuwa mtu yoyote alitumia taarifa za watu kinyume cha utaratibu, tuta wafungia kutumia Facebook na kumfahamisha kila aliyeathirika.”

    Baadhi ya maseneta wamesema kuwa kuongeza uwazi katika mitandao ya jamii lazima iwe ni hatua ya pili baada ya hapa.

    “Mmarekani wa hali ya kati hajui chochote pale mitandao inapowapeleka, umeona misamiati na masharti yaliyopo Facebook, mimi ni wakili, lakini sikuweza hata kufahamu maelezo ya ibara ya kwanza.”

    Pamoja na kuwa baadhi ya maseneta wanatambua Facebook inahitaji kuwa na mfumo wa kibiashara unaoingiza kipato kwa kutumia taarifa za watu binafsi kwa ajili ya kuwavutia watangazaji.

    “Hakuna kitu kilichokuwa bure katika maisha, kila kitu kinahusisha biashara, iwapo unafikiri unataka kitu bila ya kulipia.”

    Mahojiano ya Zuckerberg na Bunge la Marekani limeibua mazungumzo.

    “Je, utawafiki sheria ambayo itakutaka uwafahamishe watumiaji wa mitandao ya jamii kunapotokea uvunjifu wa sheria katika kipindi cha saa 72,” aliuliza Seneta Amy Klobuchar (Mdemokrati). Zuckerberg amejibu kuwa jambo hilo linafaa.

  • Marekani inapima hatua za kujibu shambulio ‘kemikali nchini Syria

    Marekani inapima hatua za kujibu shambulio ‘kemikali nchini Syria

    Marekani inasema kuwa “tayari ana maamuzi mengi” za kujibu shambulio linaloshukiwa kuwa la kikemikali nchini Syria, huku viongozi wa magharibi wakiendelea kupima hatua za kijeshi.
    Msemaji wa Ikulu ya White House Sarah Sanders amewaambia wandishi wa habari kuwa hakuna ushahidi wa mwisho uliokwisha chukuliwa juu ya mashambulio ya kijeshi.
    Lakini amesema Marekani inaziwajibisha Urusi na Syria kwa tukio hilo.

    Baraza la Kitaifa la Usalama la Marekani litakutana Alhamisi, huku waziri mkuu wa Uingereza PM Theresa May akiitisha mkutano wa baraza la mawaziri kujadili tukio hilo la Syria.
    Wanaharakati, wahudumu wa uokozi na madaktari wanasema makumi ya watu walikufa katika mji unaodhibitiwa na waasi wa Douma Jumamosi.

  • Mfanyabiashara na Mmiliki wa mabasi ya HBS, Sultan Hemed amejiua kwa kujipiga risasi asubuhi ya leo Aprili 11, 2018 nyumbani kwake Sikonge mkoani Tabora.

    Mfanyabiashara na Mmiliki wa mabasi ya HBS, Sultan Hemed amejiua kwa kujipiga risasi asubuhi ya leo Aprili 11, 2018 nyumbani kwake Sikonge mkoani Tabora.

    Akithibitisha taarifa hizo mbele ya waandishi wa habari, Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa amesema kuwa marehemu amejipiga risasi mdomoni na kutokea nyuma ya kichwa.

    “Tumepokea taarifa za kifo cha mfanyabiashara ambaye ni mkazi wa wilaya ya Sikonge, ambaye anaitwa Sultan Hemed mmiliki wa mabasi ya HBS leo asubuhi majira ya saa tatu amejipiga risasi nyumbani kwake. Risasi ambayo imeingilia mdomoni na kutokea nyuma ya kichwani,“amesema Kamanda Mutafungwa.

    Hata hivyo, Kamanda Mutafungwa amesema kuwa jeshi la polisi limefika eneo la tukio kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa zaidi baadae.

  • Naibu waziri, Juliana shonza aeleza mkakati wa serikali kuinua soka la Tanzania

    Naibu waziri, Juliana shonza aeleza mkakati wa serikali kuinua soka la Tanzania

    Serikali kupitia kwa Naibu Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza imesema kuwa inatambua katika kuhakikisha michezo ikiwepo soka inaimarika nchini, imeendelea kundesha mashindano mbalimbali ya michezo mashuleni kitaifa ikiwepo umiseta na umitashunta.

    Waziri Shonza ameyasema hayo bungeni akiwa anajibu swali la Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini Mussa Ramadhani Sima aliyetaka kufahamu mikakati ya Serikali juu kuinua soka la Tanzania.

  • 36 wahukumiwa kifo Misri kwa kushambulia makanisa ya Coptic

    36 wahukumiwa kifo Misri kwa kushambulia makanisa ya Coptic


    Mahakama ya kijeshi huko Misri imewahukumu watu thelathini na sita adhabu ya kifo kutokana na makosa ya mashambulizi dhidi ya makanisa ya Coptic.
    Watu sabini walikufa kutokana na shambulizi la bomu katika kanisa kuu la ki Coptic mjini Cairo mwishoni mwa mwaka 2016, na makanisa ya Alexandria na Tanta yaliripuliwa siku kama hiyo mwezi wa nne mwaka uliofuata.
    Tayari kundi la wanamgambo wa kiislamu wenye msiamamo mkali wamekiri kuhusika na mashambulizi hayo matatu. Wameendelea kukiri kuwa kazi yao kubwa ilikuwa kuwashambulia wakristo wachache, pamoja na mamlaka ya kijeshi.

  • Trump aapa ”kutumia nguvu” kujibu shambulio ”la kemikali” Syria

    Trump aapa ”kutumia nguvu” kujibu shambulio ”la kemikali” Syria

     

    Rais wa Marekani Donald Trump ameahidi ” kutumia nguvu ” kujibu madai ya shambulio la kemikali nchini Syria, huku mataifa ya magharibi yakitafakari hatua watakayoichukua.

    “Tuna njia nyingi za kijeshi,”aliwambia waandishi wa habari.

    Aliongeza kuwa hatua ya kujibu shambulio hilo itaamuliwa katika kipindi cha “muda mfupi”.

    Bwana Trump alisema kuwa Marekani inapata ”msaada mzuri” juu ya nani aliyehusika na shambulio la Douma Jumamosi.

    Duru za kitabibu zinasema makumi kadhaa ya watu waliawa katika shambulio hilo, lakini idadi kamili haijathibitishwa.

    Bw Trump pia alijadili tukio hilo la rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Jumatatu jioni, na viongozi wote walielezea utashi wao wa “kujibu kikamilifu”.

    Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema kuwa “analaani vikali” kitendo cha “ukatili” kinachodaiwa kuwa ni shambulio la kemikali na akatoa wito kwa wanaomuunga mkono rais Bashar al-Assad kuwajibishwa.

    Kauli za viongozi wa kimagharibi za kulaani shambulio hilo zimefuatia kikao cha malumbano katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo Marekani na Urusi walitupia na maneno makali kuhusiana na tukio la Douma.

    Muwakilishi wa Urusi kwenye baraza hilo Vassily Nebenzia alisema shambulio linalodaiwa lilipangwa na akaonya kwamba hatua za kijeshi za Marekani zinazolenga kujibu tukio hilo “litakuwa na athari mbaya”.

    Mjumbe wa Marekani Nikki Haley alisema kuwa-wanaounga mkono jeshi la Syrian – wana “damu ya watoto wa Syria ” mikononi mwao na akambandika jina rais Assad kama “zimwi “.

    Bi Haley alitoa wito wa kupigwa kura juu ya muswada wa maazimio ya kubuniwa kwa tume ya uchunguzi juu ya matumizi ya silaha za kemiikali nchini Syria siku ya Jumanne.

    Lakini Urusi inasema haiwezi kuunga mkono pendekezo hilo kwasababu lina “vipengele visivyokubalika”.

    Shirika la matibabu la Marekani na Syria linasema kuwa watu zaidi ya 500 waliletwa kwenye kituo cha matibabu katika mji wa Douma, uliopo katika jimbo la mashariki la Ghouta , karibu na mji mkuu Damascus, wakiwa na dalili “zinazoonesha kuwa walishambuliwa na kemikali”.

    Shirika hilo linasema dalili walizaokuwa nazo ni pamoja na ugumu wa kupumua, ngozi ya samawati , kutokwa na povu mdomoni , kuungua kwa mboni na “walikuwa na harufu kama ya kemikali ya chlorine”.

    Idadi kamili ya vifo ya na ni nini hasa kilichotokea haviwezi kuthibitishwa kwasababu eneo hilo halina mawasiliano.

    Makadirio ya idadi ya watu waliouawa katika shambulio linaloshukiwa kuwa la kemikali ni kuanzia watu 42 hadi zaidi 60, lakini makundi ya kitabibu yanasema idadi hiyo inaweza kuongezeka baada ya wahudumu wa uokoaji kuweza kufika kwenye sehemu za chini za majengo ambako mamia ya familia walikuwa wamekimbilia kuepuka mashambulio ya mabomu.

    Muwakilishi wa Ufaransa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amesema gesi ya sumu ilitumiwa kwa makusudi kwasababu inaweza kusambaa hadi sehemu za chini za majengo hadi.

    Marekani ,ufaransa na Uingereza wameongoza kampeni ya kimataifa ya kulaani shambulio hilo linalodaiwa kuwa la kemikali, huku serikali ya Syria na waungaji mkono wao Urusi wakikana kuwajibika kwao kokote na tukio hilo.

  • Huyo Kamusoko Anataka Mashabiki Tu

    Huyo Kamusoko Anataka Mashabiki Tu

    Kiungo wa Yanga thabani kamusoko anataka nguvu ya mashabiki wa timu yao siku ya Jumamosi wakati Yanga itakapokuwa inacheza nyumbani dhidi ya Wolaitta Dicha mchezo wa mtoano kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya kombe la shirikisho Afrika.

    Kamusoko amesema kipindi hiki ambacho timu ipo kwenye wakati mgumu wachezaji wanahitaji zaidi sapoti ya mashabiki kuliko kitu kingine.

    “Timu inapokuwa haifanyi viruri ndiyo inahitaji sapoti kubwa ya mashabiki kwa hiyo nawaomba mashabiki waje kwa wingi kuisapoti timu yao kwa sababu bila wao inakuwa ngumu kwa wachezaji. Kwa sasa timu ipo katika kipindi kigumu na ndiyo hali ya mpira, timu haiwezi ikawa inashinda kila siku”-Thabani Kamusoko amezungumza na Yahaya Mohamed ‘Mkazuzu’ mjini Morogoro.

    Mchezaji huyo raia wa Zimbabwe amesema mchezo wa jumamosi utakuwa mgumu hivyo wanahitaji kuwaheshimu wapinzani wao kwa hatua waliyofika.

    Mashindano ya Caf magumu kwa sababu ukiona timu imefika hatua ambayo ikicheza mechi mbili ikishinda inaweza kuingia hatua ya makundi sio ya kuichukulia poa, Caf ni mashindano makubwa sana. Sisi tumejiandaa vizuri, tunajua timu tunayokutana nayo iko vipi tumefanya mazoezi kwa ajili ya mechi ya Jumamosi ili tuingie tena hatua ya makundi.

    Amesema pia kwa sasa anapambana kuhakikisha anarejea kwenye kiwango chake baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha.

    “Majeraha sio mazuri, ukikaa muda mrefu bila kucheza mpira huwezi kurudi mara moja kwa hiyo unarudi taratibu hadi ifike kipindi wewe mwenyewe unaona umekaa sawa. Nimerejea lakini najitahidi nirudi kwenye kiwango changu naamini taratibu nitakuwa poa.”

  • Uhamiaji -Tanzania Yambana Abdul Nondo Athibitishe Uraia Wake

    Uhamiaji -Tanzania Yambana Abdul Nondo Athibitishe Uraia Wake

    Mashtaka ya kujiteka nyara yanayomkabili kiongozi wa mtandao wa wanafunzi nchini Tanzania (TSNP), na mtetezi wa haki za binadamu Abdul Nondo, yanaonekana kuchukua sura mpya, baada ya maafisa wa uhamiaji kumlazimisha athibitishe ni raia wa Tanzania.
    Licha ya mwanafunzi huyo kutoka mkoa wa Kigoma kupata ufadhili wa masomo wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) kutoka serikalini, anahitajika kupeleka katika idara ya uhamiaji cheti chake cha kuzaliwa, cha baba yake, mama yake, cha bibi na babu mzaa baba na mzaa mama.

    Taarifa iliyotolewa na mwanasheria wa muungano wa wanafunzi Tanzania inaeleza kwamba Abdul Nondo, amefikishwa katika makao makuu ya ofisi za uhamiaji, na kutakiwa kuthibitisha uraia wake.

    Kati ya vyeti anayotakiwa kuwasilisha kwa maafisa wa uhamiaji ni pamoja na cheti chake cha kuzaliwa, cheti cha kuzaliwa cha baba yake, mama yake, cha bibi na babu mzaa baba na mzaa mama, na vyeti vya ndugu zake ifikapo Aprili 20 bila kukosa.

    Lakini mbunge wa Kigoma Mjini, anakotoka kijana huyo, Zitto Kabwe, anasema lazima atafuatilia kwa karibu uchunguzi huo.

    “Yeye atatoa wapi cheti cha kuzaliwa cha babu yake? Hata huyu ambaye amemwagiza hivi vitu, hawezi kupata cheti ya babu yake mwenyewe. Sasa mazingira kama haya ni kutaka kumtisha ili kumfanya aache shughuli zake za harakati” amesema mbunge Zitto Kabwe katika mahojiano ya simu na sauti ya Amerika.

    Maafisa wa uhamiaji wa mkoa wa Kigoma, wanasema kuwa sheria inawaruhusu kumhoji mtu yeyote wanaye mtilia mashaka uraia wake na kuwa wana mashaka na uraia wa Abdul Nondo, hivyo awathibitishie kuwa yeye ni Raia wa Tanzania. Lakini wakili wa kijana huyo, Reginald Martin, anasema hatua hiyo ina hila.

    “Unaweza tu ukapata mwelekeo ya kwamba nia yao ni nini kwa sababu Abdul Nondo ni mwanafunzi wa chuo, ana vigezo vyote kwa sababu ni miongoni mwa wanafunzi wanoapata ufadhili wa masomo kutoka serikalini. Serikali haiwezi kumdhamini mtu au kumlipia karo, mtu ambaye sio raia wa Tanzania,” ameeleza wakili wa Abdul Nondo, Regmald Matin.

    Uchunguzi wa uraia wa Abdul Nondo pia umezua hoja kwamba wakazi wa mkoa wa Kigoma, wanadhulumiwa na serikali. Mbunge Zitto Kabwe, amesema atafuatana na mwanafunzi huyo hadi katika ofisi za uhamiaji, akilalamika kwamba mara nyingi, raia wa Kigoma wanaendewa kinyume na serikali.

    “Imekuwa ni tabia sasa kwamba wanapojitokeza wanasiasa na wananchi wenye kuhoji utenda kazi wa serikali, ikitokea tu kwamba anatoka Kigoma au mikoa ya pembezoni, wanachukuliwa kama sio raia wa Tanzania. Ndio maana nimesema kwamba nitampeleka huyu Kijana Abdul Nondo katika ofisi za uhamiaji, na watuambie kama watu wa Kigoma sio watanzania”

    Mbunge huyo pia amewataka wakazi wa Kigoma kuandamana naye hadi ofisi za uhamiaji pindi atakapo msindikiza Abdul Nondo. Sauti ya Amerika ilipomuuliza kama hatua yake ya kutaka wakazi wa Kigoma kuandamana naye hadi katika ofisi za uhamiaji haitachukuliwa kama maandamano ambayo yamepigwa marufuku na serikali haitachukuliwa kama uvunjaji wa sharia, mbunge huyo amesema kwamba hatajali jinsi matamshi na vitendo vyake vitakavyotafsiriwa.

    Abdul Nondo, mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam, anakabiliwa na mashtaka ya kutoa habari za uongo kwamba alitekwa nyara mnamo tarehe 6 mwezi machi mwaka huu, baada ya kutoweka katika mazingira tatanishi na baadae kuripoti polisi.

  • Magufuli Kuzindua Ukuta wa Machimbo ya Madini ya Tanzanite Leo

    Magufuli Kuzindua Ukuta wa Machimbo ya Madini ya Tanzanite Leo

    Rais John Magufuli wa Tanzania, leo anatarajiwa kuzindua ukuta wa machimbo ya madini ya Tanzanite,iliopo eneo la Mererani, kaskazini mwa nchini Tanzania
    Ukuta huo wenye urefu wa kilomita 24.5 na urefu wa mita tatu kwenda juu, umejengwa kufuatia agizo lililotolewa na Rais John Magufuli, kama jitihada za kudhibiti na kuzuia utoroshwaji wa madini hayo, ambayo yanapatikana nchini Tanzania pekee.

    Awali, Mwezi Februari, wakuu wa vyombo vya usalama, walitembelea eneo hilo, kuukagua ukuta huo uliojengwa kwa gharama za Kitanzania isiyozidi bilioni 6.
    Walisisitiza kuwa lengo la kujengwa kwake ni kuzuia uhalifu na si kuwazuia wachimbaji wakubwa na wadogo kupata riziki zao.

    Wakitoa taarifa kwa viongozi wa ulinzi, wataalamu waliojenga ukuta huo, walisema licha ya kufanikisha ujenzi huo, changamoto mbalimbali walikutana nazo ikiwemo hatari inayo ukabili ukuta huo, kutokana na wachimbaji kulipua baruti, karibu na ukuta, hivyo kusababisha hatari za kuharibika haraka.
    Ugumu wengine walioupata ni uchimbaji katika maeneo yenye miamba.

     

  • Spika Ndugai aizungumzia hoja ya Bashe kuhusu mauaji na utekaji

    Spika Ndugai aizungumzia hoja ya Bashe kuhusu mauaji na utekaji

    Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amezungumza kuhusu taarifa za Mbunge wa Nzega Mjini kwa tiketi ya CCM, Hussein Bashe aliyetangaza kuwasilisha hoja binafsi Bungeni kuhusu matukio ya kiusalama nchini.

    Katika mahojiano na kituo cha runinga cha Azam, Spika Ndugai amesema bado hawajapata taarifa rasmi kutoka kwa Bashe na kutoka kwa katibu wa wabunge wa CCM Bungeni kama kanuni zinavyoelekeza.

    “Niliona barua yake kwa Katibu wa Bunge akimtaharifu kuwa anayo nia ya kuleta hoja binafsi lakini hiyo hoja yenyewe sijasikia kama ameiwasilisha sasa inakuwa vigumu sana kusema chochote juu ya jambo ambalo halijawasilishwa rasmi alichofanya ni kuwasilisha taarifa,” amesema.

    Spika Ndugai ameongeza kuwa zipo kanuni za Bunge na zile za uendeshaji shughuli kwa wabunge wa CCM, vile kuna kanuni za kambi ya upinzani.

    “Kwa yeye kama mbunge wa CCM, kanuni zinamtaka hoja yake aipeleke kule kwanza kwenye chama chake ikajadiliwe kule ikikubaliwa kule ndio tuweze kuipokea, kwa hiyo bado Bashe hajatuletea hiyo taarifa lakini bado hatujapata taarifa kutoka kwa katibu wa wabunge wa CCM Bungeni,” amesema Spika Ndugai.

    Katika hatua nyingine Spika Ndugai amezungumza kuhusu hali yake ya kiafya ambapo hivi karibuni alirejea nchini kutoka kwenye matibabu.

    “Namshurukuru Mungu sasa hali yangu ni bora zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali, nichukue nafasi hii kuwashukuru sana madaktari na wasaidizi wao wote na Watanzania kwa kuniombea na kunitakiwa kila na kheri,” amesema.