Author: E-FM CO LTD

  • Watu 49 wauawa katika shambulio kwenye misikiti New Zealand

    Watu 49 wauawa katika shambulio kwenye misikiti New Zealand

    Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern anasema watu 49 wameuawa na wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa vibaya baada ya kuzuka mashambulio katika misikiti miwili katika mji wa Christchurch, huko New Zealand.

    Waziri mkuu huyo amelitaja shambulio hilo kuwa mojawapo lililotanda ‘kiza kikubwa’ siku ya leo nchini humo.

    Wanaume watatu na mwanamke mmoja wamekamatwa, kamishna wa polisi Mike Bush anasema, lakini ameonya kwamba huenda washukiwa zaidi wapo.

    Inaarifiwa kwamba washambuliaji hao hawakuwa kwenye orodha ya magaidi wanaosakwa lakini ni wazi kwamba wana itikadi kali.

    Waziri mkuu wa Australia Scott Morrison amesema mojawapo ya waliokamatwa ni raia wa Australia.

    Amemtaja mshukiwa wa shambulio hilo kuwa “gaidi mwenye itikadi kali za mrengo wa kulia”.

    Walioshuhudia mkasa huo wameambia vyombo vya habari kwamba walilazimika kutoroka kuokoa maisha yao na waliona watu walioanguka chini wanaovuja damu nje ya mskiti wa Al Noor.

    Polisi inasisitiza kwamba hali bado haijaimarika na wamethibitisha pia kwamba “vilipuzi kadhaa vilivyofungwa kwenye gari vimeharibiwa”.

    Maafisa wameshauri misikiti yote katika mji huo ifungwe mpaka ilani itakapotolea, wakieleza kwamba hili lilikuwa shambulio la vurugu ambalo halikutarajiwa.

    Mohan Ibrahim, ambaye alikuwa katika eneo hilo la msikiti wa Al Noor ameliambia gazeti la Herald: “Awali tuliona ni hitilafu za umeme lakini mara tu, watu wote wakaanza kutoroka.

    “Bado rafiki zangu wamo ndani. Nahofia usalama wa maisha ya rafiki zangu.”

    Nini kilichofanyika katika mskiti?

    Bado haijulikani wazi nini kilichofanyika ndani ya misikti hiyo, taarifa mpaka sasa zimetoka kwa walioshuhudia mkasa na waliozungumza na vyombo vya habari.

    Mashahidi wametaja kuona watu wakiwa wameanguka chini wanavuja damu.

    Inaarifiwa mshambuliaji alilenga sehemu ya maombi ya wanaume, na baadaye kuelekea katika sehemu ya wanawake.

    Watu wamehamishwa pia kutoka msikiti wa pili katika kitongoji cha Linwood na kamishna wa polisi amesema “watu kadhaa wameuawa ” katika maeneo mawili.

     

  • shika ndinga 2019

    shika ndinga 2019

    SWALI: Kama kwa siku anaingiza kiasi cha 30,000/=Tsh ambayo kwa mwezi ni sawa na 900,000/=Tsh Je kwa mwaka atakuwa ametengeneza kiasi gani cha pesa?

    Huyu ni Michael Peter Mshiriki na mshindi wa #ShikaNdinga2017 Kwa mtaji wa sikio tu wiki hii mkazi wa DSM yaweza kuwa zamu yako.

  • Tshisekedi na Kabila watangaza serikali ya Muungano

    Tshisekedi na Kabila watangaza serikali ya Muungano

    Kiongozi mpya katika Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo, Felix Tshisekedi na mtangulizi wake Joseph Kabila wamesema wameamua kuunda serikali ya muungano kufuatia mazungumzo, shirika la habari la AFP linaripoti.

    Licha ya ushindi wa rais Tshisekedi — kiongozi huyo amejikuta akilazimika kugawanya uongozi tangu uchaguzi huo wa urais.

    Mpaka sasa hajafanikiwa kumteua waziri mkuu kutokana na kwamba muungano wa Kabila – Common Front for Congo (FCC) una uwingi katika bunge la taifa.

    Mkwamo huo umeweka kizuizi kwa maazimio ya Tshisekedi kuigeuza nchi hiyo inayogubikwa kwa rushwa na tuhuma za ukiukaji wa haki za binaadamu.

    Katika taarifa ya pamoja hapo jana Jumatano, Tshisekedi na Kabila wamesema kwamba licha ya “FCC kuwa na uwingi mkubwa bungeni” katika kuidhinisha matakwa yalioelezewa na wapiga kura, FCC na CACH wanaonesha uwajibikaji “wa malengo yao ya pamoja kuongoza pamoja kama sehemu ya serikali ya muungano” linaripoti AFP.

    Taarifa hiyo inafuata ziara ya Tshisekedi nchini Namibia wiki iliyopita ambapo alielezea kukasirishwa kwake kwa kutoweza kuwa na uwingi kuunga mkono chaguo lake la wadhifa wa waziri mkuu.

    Kwa miaka 18 iliyopita, taifa lenye utajiri wa madini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo limeongozwa na mtu mmoja: Joseph Kabila.

    Kwa muda ilionekana kana kwamba Tshishekedi, jina lake halingekuwa kwenye karatasi za kura.

    Kuongezea hilo, wakosoaji wake pia walikuwa wakisema Tshisekedi hajawahi kushikilia wadhifa wowote wa juu au kuwa na uzoefu wa usimamizi.

    Lakini kadri muda ulivyosogea amefanikiwa kupanda cheo, kuanzia mwaka 2008 ambapo alikuwa katibu wa taifa aliyeangazia masuala ya uhusiano wa nje.

    Tshisekedi, ingawa hana uungwaji mkono mkubwa kama wa babake, mwaka jana alisema kwamba akishinda urais ataunda tume ya ukweli, haki na maridhiano na kumuwajibisha Bw Kabila. Lakini alisema atamruhusu kusalia nchini DR Congo.

    Changamoto kubwa ni kuangalia vipi Tchisekedi anaweza kuleta amani na maridhiano kwa taifa hilo hususan eneo la mashariki ambako kumeshuhudia ghasia na umwagikaji damu mkubwa wa raia, na uwepo wa wanamgambo waliojihami wanaotekeleza mashambulio.

    Ni wazi kwamba ni wakati wa kihistoria kwa upinzani wa nchi hiyo, ambao umekuwa kando kando katika siasa za nchi kwa miongo kadhaa.

    Lakini swali kubwa sasa ni je makubaliano haya ya kuunda serikali ya muungano yana uzito kiasi gani katika ushawishi wa kiongozi huyu mkuu, na inaweka wapi matumaini ya raia wa Congo katika swala la mageuzi nchini?

    cc;BBCswahili

  • Auawa na simba aliyemfuga nyumbani kwake

    Auawa na simba aliyemfuga nyumbani kwake

    Mwanamume mmoja ameshambuliwa na simba aliyemfuga nyumbani kwake mashariki mwa Jamhuri ya Czech

    Michal Prasek alimmiliki simba huyo mwenye miaka 9 na simba jike aliyemfuga kwa ajili ya kuzalisha , hatua inayoarifiwa kuzusha wasiwasi kutoka kwa wakaazi.

    Babake Prasek aliupata mwili wake ndani ya kizuizi cha simba huyo na kuambia vyombo vya habari kwamba kilikuwa kimefungwa kwa ndani.

    Wanyama hao waliokuwa wanaishi katika vizuizi tofuati, walipigwa risasi na kuuawa na polisi walioitwa katika eneo hilo.

    Msemaji wa polisi amewaambia waandishi habari kwamba ilikuwa muhimu kwa simba hao kuuliwa ili kumfikia marehemu.

    Prasek, mwenye umri wa miaka 33, alimnunua simba huyo mnamo 2016 na simba jike huyo mwaka jana, na aliwaweka wote katika vizuizi alivyovitengeneza katika ua lake katika kijiji cha Zdechov.

    Awali alikatazwa ruhusa ya kujenga vizuizi hivyo, na alitozwa faini kwa kufuga wanyama hao kinyume na sheria.

    Lakini mvutano wake na maafisa wa utawala ulifikia mkwamo baada ya kukataa kuruhusu mtu yoyote kuingia kwake.

    Ukosefu wa vituo mbadala katika Jamhuri hiyo ya Czech, imemaanisha kwamba haingewezekana wanyama hao kuondolewa kwa lazima.

    Prasek aligonga vichwa vya habari mwaka jana baada ya mwendesha baiskeli kupambana na simba hao wakati Prasek alipokuwa akiwatembeza huku akiwa amewafunga kwenye nyororo.

    Baada ya polisi kuingilia kati, tukio hilo lilitazamwa kama ajali ya trafiki.

    “Tukio la leo huenda likasaidia hatimaye kutatua tatizo hili la muda mrefu,” amesema meya wa Zdechov , Tomas Kocourek.

     

  • Wajasiliamali watakiwa kuwa wabahili

    Wajasiliamali watakiwa kuwa wabahili

    Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amewataka wajasiliamali wa Wilaya ya Nkasi kuhakikisha fedha za mkopo walizopewa na halmashauri hawazitumii katika matumizi binafsi bali wazielekeze katika biashara ili ziweze kuwapatia faida na kuwainua kiuchumi na hatimae kupata fedha za kujikimu kimaisha.

    Ameyasema hayo alipokuwa akikabidhi mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 53 ikiwa ni asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani ya halmashauri kwa vikundi 15 vya halmashauri ya wilaya ya Nkasi ikiwa ni utekelezaji wa kisheria chini ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) lililoanzishwa Mwaka 2005 chini ya sheria na 16 ya mwaka 2004 yenye adhima ya kuwainua wananchi kiuchumi ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

    “Kwenye vikundi vyenu mna malengo mahususi na ili haya malengo mahususi yaweze kutimia kwenye biashara hakuna kingine zaidi ya kuwa bahili lazima muwe mabahili, lazima muwe watu ambao hamkubali kutoa fedha hovyo hovyo, uskibali kutoa fedha ambayo haina mpango, leo unaambiwa kuna msiba pale wewe unachukua fedha ya mkopo unapeleka, huu sio ubahili, weka fedha yako vizuri, kama kuna shida tafuta hela nyingine,na ukichukua fedha inayotokana na hapo labda ni faida,”amesema Wangabo

    Mbunge wa jimbo la Nkasi Kaskazini, Ally Kessy alisema kuwa pesa hizo ni kodi za wananchi ambazo halmashauri inapita kuzikusanya nahatimae asilimia 10 ya mapato hayo kuyagawa kama mikopo kwa wajasiliamali wanawake, vijana na walemavu na kusisitiza kuwa fedha hiyo irudishwa kadiri inavyotakiwa.

    Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Emanuel Sekwao amesema kuwa Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Jumla ya vikundi 15 viliomba mikopo ya Tshs. 68,292,000.00. lakini baada ya Kamati ya Mikopo kukaa na kupitia maombi ya mikopo jumla ya kiasi cha Tshs 53,000,000 kiliidhinishwa.

    Naye mkuu wa wilaya hiyo, Said Mtanda amemuhakikishia mkuu wa mkoa kuwa watajitahidi kuhakikisha wanakusanya mapato ya halmashauri kwa asilimia 100 na kutoa mikopo hiyo kwa vijana na kuwapa fursa ya kujiajiri lakini pia kuongeza viwanda vidogovidogo kutokana na shughuli mbalimbali za uzalishaji wanazojihusisha nazo wajasiliamali hao.

  • Rubani wa naibu rais William Ruto afariki baada ya helikopta kuanguka Kenya

    Rubani wa naibu rais William Ruto afariki baada ya helikopta kuanguka Kenya

    Rubani wa naibu rais William Ruto amefariki katika jali ya ndege baada ya helikopta aliyokuwemo kuanguka nchini Kenya.

    Taarifa katika vyombo vya habari nchini zinaeleza kwamba ndege hiyo ilianguka Jumapili mwendo wa saa mbili usiku katika eneo la Turkana.

    Inaarifiwa kwamba Kapteni Mario Magonga amefariki pamoja na abiria wengine wanne.

    Polisi inasema helikopta hiyo imeanguka katika eneo la Labolo, kisiwa chenye milima ya volcano katikakati ya ziwa Turkana – Central Island National Park kaskazini magharibi mwa Kenya.

    “Taarifa zilizopo zinaashiria kwamba ndege mbili zilitua mapema katika kambi ya Lobolo katika kisiwa hicho kilichopo kwenye mbuga ya kitaifa, hatahivyo moja ndio iliyofanikiwa kutua salama katika eneo hilo,” idara ya polisi imesema katika taarifa yake rasmi.

    Inaarifiwa kwamba vikosi vya usalama vimetumwa katika eneo hilo katika kusaidia kwenye jitihada za kuondosha miili na masalio ya ndege hiyo.

    Kufikia sasa, chanzo cha ajali bado hakijajulikana.

    Kapteni Magonga ni nani?

    Alikuwa rubani wake naibu rais wa Kenya William Samoei Ruto.

    Aliwahi kuwa rubani katika jeshi la Kenya.

    Ni mzawa wa Nyamataro, Kitutu Chache kusini, kaunti ya Kisii – kusini magharibi mwa Kenya.

    Babake ni mwanajeshi mstaafu; Brigedia (rtd) Magonga.

    Alikuwa rubani mkuu wa helikopta za kampuni ya KIDL helicopters – inayotoa huduma za usafiri binafsi katika eneo zima la Afrika mashariki.

    Alikuwa mkufunzi aliyehitimu wa helikopta.

    Alipokea mafunzo kutoka kikosi cha ulinzi Kenya KDF.

    Ana uzoefu wa kuendesha ndege kwa zaidi ya saa 5500 kwenye ndege za injini moja na injini zaidi ya moja.

    Kwa waliofahamu, wanamueleza kuwa rubani aliye na taaluma na uzoefu mkubwa, na aliheshimika pakubwa.

  • Wanawake walio na maumbo makubwa  nchini Uganda wamewasilisha  malalamiko yao kwa  spika wa Bunge

    Wanawake walio na maumbo makubwa nchini Uganda wamewasilisha malalamiko yao kwa spika wa Bunge

    Waandalizi wa shindano la wanawake walio na maumbo makubwa nchini Uganda wamewasilisha malalamiko yao kwa spika wa bunge kufafanua madhumuni yao.

    Wamesema kuwa lengo lao sio kutumia shindano la ‘Miss Curvy Uganda” kuvutia watalii kuja nchini humo.

    ”Haya ni mashindano ya urembo wa wanawake wanene”alisema Annie Mungoma, mkurugenzi mkuu wa mashindano hayo.

    Bi. Mugoma aliongeza kuwa mtazamo wao itaondosha fikra za kimagharibi kuwa urembo unamaanisha mtu kuwa mwembamba.

    ”Tunataka kuwapatia motisha wanawake wenye maumbo makubwa kujiamini kwamba wao pia ni warembo”.

    Siku mbili zilizopita spika wa bunge Rebecca Kadaga aliyepinga vikali mashindano hayo amebadili msimamo wake baada ya kupokea ufafanuzi huo.

    Ameahidi mkono juhudi zao na kutoa ufafanuzi kwa bunge ili kuondoa fikra kwamba mashindano hayo ni ya aibu kwa jinsia ya mwanamke.

    Tangu shindano shindano hilo lilipozinduliwa mapema mwezi huu, wanasiasa,wanaharakati wa haki za wanawake na viongozi wa kidini wamejitokeza na kulishtumu vikali.

    Waziri wa utalii nchini Uganda Godfrey Kiwanda alipendekeza kuwe na onyesho la wanawake wenye maumbo makubwa ili kuvutia wageni zaidi wanaoitembelea nchi hiyo.

    Akizungumza katika uzinduzi wa shindano hilo , waziri huyo alisema kuwa itakuwa “tukio la kipekee ambalo litawaonesha mabanati wakionesha maumbo yao mazuri yaliyo nona”

    Kauli hiyo ilizua mjadala mkali hasa katika mitandao ya kijamii huku baadhi ya watu wakimshutumu bwana Kiwanda kwa kuzungumza juu ya wanawake wanene kama wananyama huku mwanamke mmoja akihoji kama ingewezekana basi wawekwe bustanini ili watazamwe kama wanayama watendewavyo “.

    Licha ya mjadala huo kufikia sasa washiriki 200 kutoka sehemu mbalimbali za Uganda pamoja na nchi jirani ya Rwanda wamejisajili kushiriki shindano la Miss Curvy Uganda linalotarajiwa kufanyika mwezi wa June mwaka huu.

    cc.BBCswahili

  • Ajali ya Treni yaua 20 Misri

    Ajali ya Treni yaua 20 Misri

    Watu 20 wamekufa na wengine 40 kujeruhiwa baada ya kutokea ajali ya treni katika njia kuu ya treni nchini humo.

    Tukio hilo limetokea baada ya treni hiyo kugonga kizuizi cha kupunguza kasi, katika kituo kimoja cha treni katikati ya mji.

    Ajali hiyo imesababishwa na kulipuka kwa tanki la mafuta la treni hiyo, hali iliyosababisha majengo ya jirani pia kuungua.

    chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana, lakini saa chache baadaye, Waziri anayeshughulika na usafiri Hisham Arafat alijiuzulu.

    Watu walioshuhudia ajali hiyo wamesema wameona miili kadhaa katika janga baya kukumba nchi hiyo katika siku za hivi karibuni, hususan kwa usafiri wa treni.

    Mmoja wa mashuhuda, Ahmed Mahmoud ameliambia shirika la Habari la AFP, kuwa alitoa miili ya watu 20 na kuiweka kwenye gari la wagonjwa, yote ikiwa imechomeka.

    Aidha amesema kawaida treni likikaribia kituoni huja kwa mwendo wa taratibu, lakini siku hiyo lilikuwa katika kasi.

    Awali vyombo vya habari vya nchi hiyo viliripoti kwamba watu waliofariki ni 25 huku wengine 50 wakiwa wamejeruhiwa.

    Waziri mkuu wa nchi hiyo Mostafa Madbouli ameapa kutoa adhabu kali kwa yeyote yule atakayehusika kupanga ajali hiyo.

    Kwa upande wake, Rais wa nchi hiyo Abdul Fattah al Sisi ametuma salamu za rambirambi kwa familia za marehemu na kusisitiza kuwa watu wote waliojeruhiwa watapata msaada wowote watakaohitaji.

     

  • Wakili wa zamani wa Trump aliambia bunge kuwa rais huyo wa Marekani alipanga uongo

    Wakili wa zamani wa Trump aliambia bunge kuwa rais huyo wa Marekani alipanga uongo

    Wakili wa zamani wa rais wa Marekani Donald Trump, Michael Cohen amedai kwamba kiongozi huyo alimtaka adanganye kuhusu mpango biashara kuhusu biashara ya ujenzi wa jengo mjini Moscow wakati wa kampeni ya uchaguzi wake.

    Katika ushahidi alioutoa bungeni, Cohen amesema Trump aliratibu mipango ya siri kwa ujenzi wa jengo kubwa, hata wakati alikana kuhusika na biashara yoyote Urusi.

    Ameeleza pia kwamba Trump alifahamu kuhusu kufichuliwa kwa barua pepe zilizodukuliwa za chama cha Democrat na amemuita kiongozi huyo “mbaguzi”, “tapeli” na “muongo”.

    Trump alijibu: “Anadanganya ili kupunguza kifungo chake gerezani.”

    Rais wa Marekani alichukua muda katika kujitayarisha kukutana na kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong-un huko Hanoi, Vietnam, siku ya Jumatano kumjibu kupitia ujumbe wa Twitter wakili wake huyo wa zamani.

    Cohen amesema nini kuhusu mradi wa Moscow?

    Katika ushahidi wake wa wazi katika kamati ya bunge la wawakilishi Jumatano, amesema Trump “alifahamu na aliratibu” mipango ya ujenzi wa jengo ‘Trump Tower’ mjini Moscow, huku akikiri wazi kwamba hana biashara yoyote na Urusi.

    “Wakati huo huo nilikuwa nashauriana na kujadiliana na Urusi kwa niaba yake,” Cohen ameeleza katika ushahidi wake, “angeniangalia machoni na aniambie hakuna bishara yoyote Urusi na alafu atoke aende kuwadanganya raia wa Marekani kwa kusema hilo hilo. Kwanamna yake, alikuwa akiniambia nidanganye..”

    “Alitaka nidanganye,” aliongeza.

    Hatahivyo, Cohen ameshtakiwa kwa kulidnagnya bunge alipotoa ushahidi mnamo 2017 kwambajitihada za kujenga jengo refu la Trump huko Moscow zilisitishwa kufikia Januari 2016.

    tangu hapo amekiri kwamba kumekuwepo majadiliano yalioendelea hadi Juni 2016 wakati wa kampeni ya uchaguzi, licha ya kwamba ujenzi wa mradi huo haukuendelea.

    Cohen ameomba msamaha kwa kauli yake ya awali bungeni, ambayo anatuhumu kwamba ‘ilikaguliwa na kuhaririwa’ na mawakili wa Trump.

    Cohen amewaambia wabunge kwamba Trump ni mbaguzi wa rangi.

    Amesema: “Aliwahi kuniuliza nitaje jina la nchi moja ambayo inaongozwa na mtu mweusi ambayo sio ‘shithole’ kwa maana ya shimo la choo.

    “Huu ulikuwa wakati ambapo Barack Obama ndiye alikuwa rais wa Marekani.

    “Tulipokuwa tumo ndani ya gari tukipita mtaa duni huko Chicago, alitamka kwamba ni watu weusi tu wanaoweza kusihi katika hali kama hiyo.

    “Na aliniambia kwamba watu weusi hawawezi kumpigia kura kwasababu ni wapumbavu. Lakini bado niliendelea kufanya kazi naye.”

    Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchni Tanzania, said Msonga ambaye ameifuatilia sakata hii, ametathmini kwamba katika maelezo ambayo bwana Cohen ameyatoa bungeni, ‘unaona moja kwa moja amejaribu kushambulia baadhi ya hoja za rais Donald Trump ambazo amekuwa akizisimamia kwa muda mrefu.

    ‘Kwa mfano amekuwa akishughulika na masuala ya vyombo vya habari, familia pamoja na masuala ya ule ukuta wa Mexico na urafiki wake na viongozi ambao wao walikuwa wanafikiria ni maadui wa Marekani’.

    Kwa jumla, Msonga anasema ni mambo ambayo yanaweza yakaibua hoja na hisia ambazo zinaweza zikampatia bwana Trump kipindi kigumu wakati wa uchaguzi wa mwaka 2020 pale atakapowania nafasi ya kuiongoza tena Marekani.

  • Makamba amwaga wino mzito kuhusu Ruge, ‘msiri wako’

    Makamba amwaga wino mzito kuhusu Ruge, ‘msiri wako’

    Wakati Tanzania ikiwa kwenye majonzi ya kuondokewa na mdau mkubwa wa tasnia ya burudani na habari, Ruge Mutahaba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba amemuandikia barua yenye mguso wa moyo ambayo imesambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii.

    Mkurugenzi huyo wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group Ruge Mutahaba Renzi za uhai wake

    Makamba ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Mkurugenzi huyo wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, ameeleza mengi kuhusu ukaribu wao, mipango yao na usiri waliokuwa wakiushea pamoja.

    “Ndugu yangu Ruge, najua ndio umewasili huko upande wa pili na si ajabu una mambo mengi na bado unasalimiana na jamaa zetu wengi waliotangulia. Lakini naomba uchukue muda wako kidogo kunisikiliza. Nimeumia sana na nimelia peke yangu kwamba umetuacha namna hii. Sawa, umeitwa kwa wakati wako na sisi hatuna kauli kwenye suala la wakati wa kuitwa lakini nilitegemea, na sikuwa na shaka kabisa, kwamba tutakamilisha yale mawazo yako mengi mazuri uliyoniambia. Sikuwa na shaka kwasababu nilishuhudia pale Hospitali ya Kairuki kabla hujaenda India, ulivyorudi kutoka India, na siku nimekuona Afrika Kusini, ulivyokuwa unapigana kupona –  hadi madaktari wa Afrika Kusini wakakupa jina “Ruge, The Fighter”. Jina sahihi kabisa lililotafsiri harakati za maisha yako. 

     Unajua nini? Nilikuwa nangoja urudi Dar nikwambie nilichogundua mara ya mwisho nilivyokuona hospitali. Lakini ngoja tu nikwambie kabla sijaja huko uliko. Ile kiu kubwa ya kupona niliyoiona kwenye macho yako haikuwa kwa ajili yako wewe, bali kwa ajili ya kutoiangusha familia yako nzima iliyosimamisha kila kitu kukuuguza na Watanzania wote waliokuwa wanakuombea. Ulipigana kupona, sio kwa ajili yako, bali kwa ajili yetu. Hukuamka kitandani lakini hukushindwa mapambano kwasababu umeamkia ndani ya mioyo ya Watanzania. Huku tuliko karibu watu wote tunakumbuka ulivyotugusa. Jamaa yangu, tunakuomboleza wakati huu, halafu tutabaki tunafurahia nuru yako katika maisha ya wengi kwa urefu wa uhai wetu. Umekimbia mbio njema, umemaliza safari yako vyema.

    Majonzi yangu ni kwamba umeondoka kabla sijalipa kwa ukamilifu deni langu kwako. Deni la upendo na urafiki wa kweli. Ulinipa heshima kubwa ya kuwa msiri wako – kwa kuniamini na kunielezea wasiwasi wako, ndoto zako, matumaini yako, harakati zako, mipango yako. Ulinipa heshima ya kunipa fursa ya kubishana nawe kuhusu mawazo na fikra zako.

     Majonzi yangu ni kwamba kuna vitu fulani vikubwa na vizuri tulivipanga – mimi na marafiki na wadogo zako, kwa ajili yako, kwa staili yako – mapema mwezi Machi, ambavyo naamini vingekupa tabasamu. Kama unaweza, hapo ulipolala, tupe ishara tufanyeje.

     Nafarijika kidogo kwamba nilipata nafasi ya kukukumbatia kwa mara ya mwisho. Sikujua kwamba tunaagana. Ulinishika mkono kwa nguvu, hukutaka kuuachia, na ulitabasamu niliposema nakungoja Dar tukae pale THT, kama kawaida yetu, kujadili mawazo na mipango yako mingi.

     Ingawa umeshawasili huko upande wa pili, familia yako na watu wengi watauaga mwili wako kwa heshima kubwa. Utajengewa kaburi. Nadhani litawekwa marumaru. Lakini tukitaka kukusalimia tena hatutakutafuta kaburini kwako. Tutakutafuta kwenye nyoyo za watu uliowagusa na kuwasaidia. Na ni wengi kweli. Kumbukumbu yako itabaki kwenye nyoyo zao na kwenye mafanikio yao. Watoto wako hawapo peke yao. Watalia sana, lakini ni kwa muda tu; kwasababu watafunikwa kwa upendo wetu sote na watafarijika, na watakuwa na fahari, kwa jinsi unavyosemwa na unavyokumbukwa.

     Ndugu yangu, nisikuchoshe. Mengine tutaongea tutakapokutana tena kwasababu kwa hakika sisi sote, mmoja mmoja na kwa wakati wetu, kwa kadri ya mipango yay eye aliyetuumba, tutakufuata huko. Miaka yote nimekujua, sijawahi kukuona umepumzika. Pumzika kwa amani kwa sasa – na milele.

     Ndimi, rafiki yako,

     January Makamba

    Ruge alipofariki dunia juzi akiwa hospitalini nchini Afrika Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu kutokana na kusumbuliwa na tatizo la figo. Mwili wake utawasili nchini kesho (Ijumaa) kwa ajili ya taratibu za mazishi.

    Mungu amrehemu.

  • Marekani yaeleza ilivyowachapa Al-Shabaab Jumapili

    Marekani yaeleza ilivyowachapa Al-Shabaab Jumapili

    Jeshi la Marekani jana lilisema kuwa limefanya mashambulizi ya anga nchini Somalia na kufanikiwa kuwaua wapiganaji 35 wa kundi la kigaidi la Al Shabaab.

    Marekani imekuwa ikifanya mashambulizi mara kadhaa dhidi ya Al Shabaab kwa lengo la kuviunga mkono vikosi vya Umoja wa Mataifa vinavyoendelea kuisaidia Serikali ya Somalia kupambana na Al Shabaab kwa miaka kadhaa sasa.

    Kupitia tamko lake, Kamandi ya Marekani nchini Afrika imeeleza kuwa ilifanya mashambulizi hayo Jumapili katika eneo lililo karibu na Beledweyne mkoani Hiran nchini Somalia.

    “Mashambulizi haya ya anga yalilenga wapiganaji wa Al Shabaab wenye silaha ambao walikuwa wanatawanywa kwenye maeneo mbalimbali katika vijiji,” imeeleza taarifa hiyo.

    Al Shabaab wanatekeleza mashambulizi ya kigaidi kwa lengo la kuipindua Serikali ya Somalia na kusimika utawala wa kidini wenye itikadi kali.

    Vikosi vya Umoja wa Mataifa vimeendelea kuiongezea nguvu Serikali dhidi ya kundi hilo, ingawa bado linaonekana kuwa na uthubutu wa kutekeleza mashambulizi katika maeneo mbalimbali.

    Januari mwaka huu, Al Shabaab ilivamia nchini Kenya na kufanya shambulizi la kigaidi katika eneo la Riverside.  Makumi ya watu walipoteza maisha kutokana na shambulizi hilo.