Mkurugenzi na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas amesema kuwa Serikali inaendelea na majadiliano kuhusu kuendelea na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo Mkoani Pwani ili kuona kama inaweza kuwa na tija kiuchumi kwa upande wa Tanzania.
Mkurugenzi na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas
Amesema kuwa Serikali ina uwezo wa kujenga bandari nyingi na kwa kuwa Tanzania ina ukanda mkubwa wa ufukwe wa bahari na kwamba bado majadiliano yenye tija kwa Taifa yanaendelea kufanywa baina ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji wa mradi huo.
“Serikali haijasema kuwa Mradi wa Bandari ya Bagamoyo ni hatari, tunaendelea na majadiliano ya utekelezaji wa mradi huo, nchi yetu imejaliwa ukanda mkubwa wa ufukwe wa bahari kwa hiyo tuna uwezo wa kujenga Bandari nyingi tu, hii ya Bagamoyo si kweli kuwa imeachwa kuna mambo ya msingi tunayajadili na tusipofikia maamuzi tutaachana nayo,”amesema Dkt. Abbas
Aidha, kuhusu uhuru wa habari na kufungia magazeti yasiyofuata sheria za uchapishaji Msemaji huyo wa Serikali amesema kuwa ofisi yake haikurupuki kufungia magazeti, na kusema kuwa ni magazeti matatu tu yalifungiwa kati ya 266 yaliyosajiliwa nchini na kuwataka wamiliki wa magazeti hayo kufuata sheria.
Hata hivyo, kuhusu malamiko ya wafanyabiashara kwenye maeneo mbalimbali nchini ya kufunga biashara hizo kwa kisingizio cha kodi na tozo mbalimbali, amesema kuwa ni muhimu wakaelewa kwamba kwa sasa Serikali inapita katika kipindi cha mabadiliko na hakuna siku serikali haitadai kodi huku akieleza kuwa kodi nyingi zimepunguzwa hususani kwenye sekta za Kilimo, Mifugo na uvuvi.
“kwanza tukubali tunapita kwenye kipindi cha mabadiliko, hakuna siku serikali haitadai kodi kwa sababu ndio msingi wa maendeleo ya nchi hii, kuna dhana ilijengeka kuwa unaweza kufanya biashara bila kulipa kodi hiyo sasa haipo, lazima tuangalie changamoto ambazo zinakumba sekta mbalimbali mfano sekta ya kilimo, miufgo na uvubvi kulikuwa na kodi zaidi ya 150, serikali imefuta zaidi ya kodi 80 hadi 100” alisema Dkt Abbas
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewashukia vikali wanasiasa nane wa Kata ya Kitwai Wilayani Simanjiro wanaorudisha nyuma maendeleo kwa kukataza wanafunzi wasisome kwenye madarasa ya shule ya msingi Kitwai B yaliyojengwa na mdau wa maendeleo hivyo kuyasusia.
Ametoa onyo hilo mkoani humo wakati akizindua madarasa matatu mapya ya shule hiyo, ambapo amesema kuwa wanasiasa hao atawachukulia hatua kali wanaoshawishi wananchi kususia maendeleo.
Amesema kuwa hatakubali kuona watu wachache wanaopinga maendeleo, hivyo serikali itamuunga mkono mdau huyo wa maendeleo, Sanare Mollel ambaye pia ana mpango wa kumalizia majengo ya Zahanati ya kijiji hicho.
“Wanasiasa hao wanampinga mdau huyo kwa sababu ni mfugaji mkubwa ambaye amefuata taratibu na kanuni zote za kuingia ndani ya kijiji hicho lakini hajavunja sheria kwani Mtanzania anaruhusiwa kuishi popote,”amesema Mnyeti.
Aidha, amesema kuwa haiwezekani mdau wa maendeleo ajitolee kujenga madarasa matatu kisha baadhi ya wanasiasa wanawaambia wananchi wasisomeshe watoto katika shule hiyo.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo, Nyika Shawishi amesema kuwa wapinzani wake wa kisiasa ndiyo wanaosababisha hali hiyo kwani wanaona maendeleo yakifanyika sifa zitakuwa kwake.
Naye ofisa elimu ya msingi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Silvanus Tairo amesema kuwa shule hiyo imegharimu sh. 47.3 milioni ambapo mdau wa maendeleo alijitolea sh30 milioni na nguvu za wananchi zimegharimu sh.12.3 milioni.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema kuwa utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi wa mwaka 2016/17 unaonyesha kwamba kiwango cha maambukizi ya VVU yamepungua kwa asilimia moja kutoka asilimia 5.1 mwaka 2011/2012 mpaka asilimia 5.0 kwa mwaka 2016/17.
Waziri Mhagama amesema hayo wakati akizindua utafiti huo ambapo ameeleza kuwa unaonyesha kwamba kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15-64 umepungua kwa asilimia moja kutoka asilimia 5.1 mwaka 2011/2012 na kufikia asilimia 5.0 kwa mwaka 2016-2017 ambapo wanawake ni asilimia 6.5 na wanaume ni asilimia 3.5.
Amesema asilimia 60.9 ya watu wanaoishi na VVU ndio wanaofahamu hali zao ikiwa ni chini ya kiwango cha lengo ambapo amedai wamaofahamu hali zao asilimia 93.6 ndio wanaopatiwa dawa za kufubaza makali ya VVU (ARV) ambao miongoni mwao asilimia 87.0 virusi vyao vimefubazwa.
Ameongeza kuwa utafiti huo unaonesha zaidi ya nusu milioni ya watu wanaoishi na VVU Tanzania hawajui hali yao ya maambukizi.
“Juhudi za pamoja za wenye wigo mpana zinahitajika kuwafikia watu wanaishi na VVU ambao bado hawajapima na kujua hali zao nakuanza dawa,” alisema.
Amesema takribani watu 72,000 wanapata maambukizi mapya huku kiwango cha wanaume kujua maambukizi kikiwa kipo chini kuliko wanawake.
Aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Yanga Samwel Lukumay na aliyekuwa mjumbe wa kamati ya utendaji, akishikilia nyadhifa za Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano na Mwenyekiti wa Kamati ya usajili, Hussein Nyika, wamejiuzulu nafasi zao leo Machi 27, 2019.
Nyika na Lukumay wametangaza hilo, kwenye makao makuu ya klabu hiyo ambapo wamesema kuwa wamefanya hivyo ili kupisha uchaguzi utaowezesha klabu hiyo kupata viongozi wapya.
Aidha, viongozi hao ndio waliokuwa wamebaki kwenye uongozi wa Yanga ambao uliingia madarakani mwaka 2016 baada ya wengine kujizulu, hivyo sasa timu hiyo inabaki bila uongozi mpaka pale uchaguzi mkuu utakapofanyika.
”Ninajiuzulu nafasi zangu zote nikiwa kama Mjumbe wa kamati ya utendaji lakini pia Mwenyekiti wa kamati ya usajili na kamati ya mashindano na niombe msamaha kwa wale niliowakosea katika utekelezaji wangu wa majukumu,” amesema Nyika.
Kwa upande wake Lukumay amesema kuwa wameamua kufanya hivyo ili kutoa nafasi kwa uchaguzi mkuu kupata viongozi wote tofauti na awali ambavyo ilikuwa ni uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi.
Hata hivyo, siku za hivi karibuni Baraza la wadhamini la Yanga liliweka wazi kuwa, badala ya kufanya uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizowazi ikiwemo ile ya Mwenyekiti, utafanyika uchaguzi mkuu kwaajili ya kupata viongozi.
Mzee mmoja aliyetambulika kwa jina la Visu Urembo (80) amefariki dunia baada ya kuchomwa mkuki sehemu ya ubavuni mwa mwili wake, katika mgogoro wa wakulima na wafugaji uliotokea Lukenge, Tarafa ya Ruvu, Kibaha Vijijini mkoani Pwani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, ACP Wankyo Nyigesa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo amesema tukio hilo limetokea machi 26 mwaka huu baada ya kutokea tafrani kati ya wakulima na wafugaji.
Amesema kuwa mzee Urembo kabla ya kufikwa na umauti alikimbizwa kituo cha afya Mlandizi, ambapo baadaye alikimbizwa katika hospital ya Tumbi kwa matibabu zaidi lakini kabla ya kupatiwa matibabu madaktari waligundua kuwa tayari ameshafariki.
Aidha, Wankyo amesema kuwa wafugaji hao waliingiza mifugo yao (Ng’ombe) kwenye bwawa linalotumika katika shughuli za kibinadamu ikiwemo kunywa, kufulia, kupikia, kwa kuona hivyo wakulima walienda na mihemko kuwazuia wafugaji hao, ndipo wafugaji hao walipoanza kurusha mikuki na vitu vyenye ncha kali na kusababisha kifo cha mzee huyo na wengine watatu kujeruhiwa vibaya.
“Polisi tulifika eneo la tukio alfajiri Machi 27 mwaka huu ,na kutuliza tafrani hiyo na sasa hali ni shwarii,”amesema kamanda Wankyo
Hata hivyo, amewataja waliojeruhiwa kuwa ni pamoja na John Kisukari Urembo (50) ambaye ni mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Lukenge. Maximilian Evarist (34) mtendaji wa kijiji cha Lukenge na Adam Onesha ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maji kijijini hapo .
Kwa upande wake, mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama ameyataka makundi hayo yaheshimiane na kujenga upendo badala ya kujiona kundi moja ni zaidi ya kundi jingine.
Wadau wa sekta ya Afya wameazimisha siku ya Muungano wa Utepe mweupe wa uzazi salama katika mkoa wa Kagera kwa kuhimiza jamii kuzuia ukatili wa kijinsia kwa wanawake na wasichana
Maazimisho hayo yamefanyika katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera yakiwa na kauli mbiu ‘komesha unyanyasaji kwa wanawake na wasichana, okoa maisha wakati wa uzazi’.
Meneja Mawasiliano wa Muungano wa Utepe mweupe wa uzazi salama, Anna sawaki amesema kuwa lengo la kufanya maazimisho ni kuweza kupunguza vifo kwa wanawake wakati wa kujifungua.
Amesema kuwa takwimu zinaonyesha vifo vitokanavyo na uzazi vinaongezeka badala ya kupungua kutokana na unyanyasaji wanaoupata akina mama pindi wawapo wajawazito na wakati wa kujifungua.
Kwa upande wake mratibu wa taifa wa muungano wa utepe mweupe wa uzazi salama, Rose Mlayi ameiomba jamii kukomesha ukatili kwa wanawake na wasichana, ili kuokoa maisha yao wakati wa uzazi.
Katika hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo amesisitiza kuwa serikali kupitia idara zake inaendelea kukomesha vitendo hivyo, ikiwemo kuendelea na mikakati yake ya kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi pingamizi.
Waziri ummy ameongeza kuwa wizara yake inaendelea kuboresha sekta ya afya hasa upande wa vituo vya afya pamoja na vifaa tiba ambapo pia ameeleza mkakati wa kuanzisha vituo vya huduma jumuishi kwa kila kituo cha afya.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amewataka wajasiliamali wa Wilaya ya Nkasi kuhakikisha fedha za mkopo walizopewa na halmashauri hawazitumii katika matumizi binafsi bali wazielekeze katika biashara ili ziweze kuwapatia faida na kuwainua kiuchumi na hatimae kupata fedha za kujikimu kimaisha.
Ameyasema hayo alipokuwa akikabidhi mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 53 ikiwa ni asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani ya halmashauri kwa vikundi 15 vya halmashauri ya wilaya ya Nkasi ikiwa ni utekelezaji wa kisheria chini ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) lililoanzishwa Mwaka 2005 chini ya sheria na 16 ya mwaka 2004 yenye adhima ya kuwainua wananchi kiuchumi ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
“Kwenye vikundi vyenu mna malengo mahususi na ili haya malengo mahususi yaweze kutimia kwenye biashara hakuna kingine zaidi ya kuwa bahili lazima muwe mabahili, lazima muwe watu ambao hamkubali kutoa fedha hovyo hovyo, uskibali kutoa fedha ambayo haina mpango, leo unaambiwa kuna msiba pale wewe unachukua fedha ya mkopo unapeleka, huu sio ubahili, weka fedha yako vizuri, kama kuna shida tafuta hela nyingine,na ukichukua fedha inayotokana na hapo labda ni faida,”amesema Wangabo
Mbunge wa jimbo la Nkasi Kaskazini, Ally Kessy alisema kuwa pesa hizo ni kodi za wananchi ambazo halmashauri inapita kuzikusanya nahatimae asilimia 10 ya mapato hayo kuyagawa kama mikopo kwa wajasiliamali wanawake, vijana na walemavu na kusisitiza kuwa fedha hiyo irudishwa kadiri inavyotakiwa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Emanuel Sekwao amesema kuwa Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Jumla ya vikundi 15 viliomba mikopo ya Tshs. 68,292,000.00. lakini baada ya Kamati ya Mikopo kukaa na kupitia maombi ya mikopo jumla ya kiasi cha Tshs 53,000,000 kiliidhinishwa.
Naye mkuu wa wilaya hiyo, Said Mtanda amemuhakikishia mkuu wa mkoa kuwa watajitahidi kuhakikisha wanakusanya mapato ya halmashauri kwa asilimia 100 na kutoa mikopo hiyo kwa vijana na kuwapa fursa ya kujiajiri lakini pia kuongeza viwanda vidogovidogo kutokana na shughuli mbalimbali za uzalishaji wanazojihusisha nazo wajasiliamali hao.
Wakati Tanzania ikiwa kwenye majonzi ya kuondokewa na mdau mkubwa wa tasnia ya burudani na habari, Ruge Mutahaba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba amemuandikia barua yenye mguso wa moyo ambayo imesambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii.
Mkurugenzi huyo wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group Ruge Mutahaba Renzi za uhai wake
Makamba ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Mkurugenzi huyo wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, ameeleza mengi kuhusu ukaribu wao, mipango yao na usiri waliokuwa wakiushea pamoja.
“Ndugu yangu Ruge, najua ndio umewasili huko upande wa pili na si ajabu una mambo mengi na bado unasalimiana na jamaa zetu wengi waliotangulia. Lakini naomba uchukue muda wako kidogo kunisikiliza. Nimeumia sana na nimelia peke yangu kwamba umetuacha namna hii. Sawa, umeitwa kwa wakati wako na sisi hatuna kauli kwenye suala la wakati wa kuitwa lakini nilitegemea, na sikuwa na shaka kabisa, kwamba tutakamilisha yale mawazo yako mengi mazuri uliyoniambia. Sikuwa na shaka kwasababu nilishuhudia pale Hospitali ya Kairuki kabla hujaenda India, ulivyorudi kutoka India, na siku nimekuona Afrika Kusini, ulivyokuwa unapigana kupona – hadi madaktari wa Afrika Kusini wakakupa jina “Ruge, The Fighter”. Jina sahihi kabisa lililotafsiri harakati za maisha yako.
Unajua nini? Nilikuwa nangoja urudi Dar nikwambie nilichogundua mara ya mwisho nilivyokuona hospitali. Lakini ngoja tu nikwambie kabla sijaja huko uliko. Ile kiu kubwa ya kupona niliyoiona kwenye macho yako haikuwa kwa ajili yako wewe, bali kwa ajili ya kutoiangusha familia yako nzima iliyosimamisha kila kitu kukuuguza na Watanzania wote waliokuwa wanakuombea. Ulipigana kupona, sio kwa ajili yako, bali kwa ajili yetu. Hukuamka kitandani lakini hukushindwa mapambano kwasababu umeamkia ndani ya mioyo ya Watanzania. Huku tuliko karibu watu wote tunakumbuka ulivyotugusa. Jamaa yangu, tunakuomboleza wakati huu, halafu tutabaki tunafurahia nuru yako katika maisha ya wengi kwa urefu wa uhai wetu. Umekimbia mbio njema, umemaliza safari yako vyema.
Majonzi yangu ni kwamba umeondoka kabla sijalipa kwa ukamilifu deni langu kwako. Deni la upendo na urafiki wa kweli. Ulinipa heshima kubwa ya kuwa msiri wako – kwa kuniamini na kunielezea wasiwasi wako, ndoto zako, matumaini yako, harakati zako, mipango yako. Ulinipa heshima ya kunipa fursa ya kubishana nawe kuhusu mawazo na fikra zako.
Majonzi yangu ni kwamba kuna vitu fulani vikubwa na vizuri tulivipanga – mimi na marafiki na wadogo zako, kwa ajili yako, kwa staili yako – mapema mwezi Machi, ambavyo naamini vingekupa tabasamu. Kama unaweza, hapo ulipolala, tupe ishara tufanyeje.
Nafarijika kidogo kwamba nilipata nafasi ya kukukumbatia kwa mara ya mwisho. Sikujua kwamba tunaagana. Ulinishika mkono kwa nguvu, hukutaka kuuachia, na ulitabasamu niliposema nakungoja Dar tukae pale THT, kama kawaida yetu, kujadili mawazo na mipango yako mingi.
Ingawa umeshawasili huko upande wa pili, familia yako na watu wengi watauaga mwili wako kwa heshima kubwa. Utajengewa kaburi. Nadhani litawekwa marumaru. Lakini tukitaka kukusalimia tena hatutakutafuta kaburini kwako. Tutakutafuta kwenye nyoyo za watu uliowagusa na kuwasaidia. Na ni wengi kweli. Kumbukumbu yako itabaki kwenye nyoyo zao na kwenye mafanikio yao. Watoto wako hawapo peke yao. Watalia sana, lakini ni kwa muda tu; kwasababu watafunikwa kwa upendo wetu sote na watafarijika, na watakuwa na fahari, kwa jinsi unavyosemwa na unavyokumbukwa.
Ndugu yangu, nisikuchoshe. Mengine tutaongea tutakapokutana tena kwasababu kwa hakika sisi sote, mmoja mmoja na kwa wakati wetu, kwa kadri ya mipango yay eye aliyetuumba, tutakufuata huko. Miaka yote nimekujua, sijawahi kukuona umepumzika. Pumzika kwa amani kwa sasa – na milele.
Ndimi, rafiki yako,
January Makamba
Ruge alipofariki dunia juzi akiwa hospitalini nchini Afrika Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu kutokana na kusumbuliwa na tatizo la figo. Mwili wake utawasili nchini kesho (Ijumaa) kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuongeza ulinzi na doria katika maeneo ya mipaka kutokana na ongezeko la vitendo vya mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha na vitisho kwa wananchi.
Ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa wilayani Kibondo wakati akihitimisha ziara yake mkoani Kigoma.
Pia, Waziri Mkuu ameagiza wakimbizi wote watakaobainika kutoroka kwenye makambi wanayohifadhiwa na kuingia uraiani wakamatwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za Tanzania, kwani wanachokifanya ni ukiukwaji wa sheria.
Aidha, maeneo yaliyo katika hali mbaya ni Kibondo, Buhigwe, Kasulu, Ngara, Biharamulo, Uvinza, Kakonko na Kigoma Vijijini, ambako wananchi hususani wafanyabiashara wameingiwa na hofu kutokana na vitendo hivyo.
”Kulinda usalama wa nchi ni jukumu letu sote na si la vyombo vya ulinzi na usalama pekee, kila mmoja anapaswa kushiriki. Kwa upande wa majirani zetu wanaotaka kuja nchini ni lazima wafuate taratibu kwa kuomba vibali.”amesema Majaliwa
Hata hivyo, Majaliwa ameongeza kuwa watu wote wanaoingia bila ya kufuata sheria na taratibu ndio hao wanashiriki katika vitendo vya uhalifu yakiwemo mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, unyang’ani wa kutumia silaha za kivita pamoja na utekaji wa watoto.
Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu, Glory Mziray amefariki dunia jana majira ya mchana akiwa ofisini kwake jengo la Mpingo wakati akifanya mkutano na waandishi wa habari juu ya kupandishwa hadhi kwa misitu 7.
Meneja huyo alishikwa na umauti wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari yaliyotokana na kile alichokuwa akiwasilisha.
Hapa ndipo ule msemo usemao hakuna ajuaye siku wala saa unavyotimia kwa meneja huyu kijana, ambaye dakika chache zilizopita hakuwa mgonjwa wala hakuonesha kupata shida yeyote kwani alijiandaa vyema kuiwakilisha wizara yake.
Glory alikutwa na mauti mara baada ya mmoja ya mwandishi wa habari kumtaka ajitambulishe kwa majina na cheo chake kwani hakufanya hivyo mwanzoni wakati akitoa hotuba yake.
Ambapo dakika kadhaa baada ya kusimama kujibu swali hilo, Glory alianza kubadilika gafla na kuanza kupoteza sauti na kupoteza fahamu kabisa.
Wanahabari walimpa huduma ya kwanza bila mafanikio, ndipo wakaamua kumkimbiza hospitali ya TMJ chang’ombe ambapo madaktari walimfanyia uchunguzi na kubaini kuwa alipoteza maisha kabla ya kufika hospitali hapo.
Aidha, Daktari Chris Peterson ameeleza kuwa familia yake imesema Glory alikuwa na tatizo la Shinikizo la damu.
Wananchi takribani 285 wa Kijiji cha Utelingolo halmashari ya wa Mji wa Njombe mkoani humo wamesema kuwa hali ya uchumi itashuka kijijini hapo kwa sababu wamekuwa wakitumia muda mwingi kupeleka na kurudisha watoto shule badala ya kufanya shughuli za kuwapatia kipato.
Hali hiyo imepelekea serikali ya kijiji hicho kuweka utaratibu wa kuwa na daftari maalumu la kusaini pindi unapopeleka na kuchukua mtoto katika shule husika wanayo soma.
‘’Sisi wanawake ndo tunateseka, kama mimi nina watoto watatu wanasoma madarasa tofauti na muda wa kutoka hivyo sasa asilimia kubwa nashinda na kazi ya kwenda kuwachukua kwa hiyo muda wa kufanya maendeleo unakua hamna,’’ amesema Mary Mlawa.
‘Aidha, wananchi hao wameiomba serikali kusema kitu kwani sasa hivi wanashindwa kufanya maendeleo ya kujenga nchi kwa sababu hakuna anayeruhusiwa kuchukua mtoto wa mwenzake mpaka umfuate yeye mwenyewe.
Kwa upande wa Chris Msigwa amesema kuwa kila kitu kimesimama na kuna hatari kubwa hapo baadae kushindwa kusomesha watoto.