Category: Local News

  • Afrika yaongoza kwa rasilimali ya maji baridi

    Afrika yaongoza kwa rasilimali ya maji baridi

    Zaidi ya asilimia 30 ya maji baridi Duniani yapo katika ukanda wa Afrika, hayo yamebainishwa na Meneja wa mamlaka ya udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kanda ya kati, Mhandisi Norbet kayonza katika semina ya siku moja ya wakandarasi wa umeme wa manispaa ya singida.

    Mhandisi Kayonza ametahadharisha kuwa licha ya mahitaji ya maji kuongezeka lakini vyanzo vya maji vinapungua kwani idadi ya watumiaji inaongezeka siku hadi siku, nakusisitiza “rasilimali ya maji duniani inapungua huo ni ukweli ambao haupingiki, lakini siyotu inapungua bali watumiaji wa maji ikiwa na maana ya idadi ya watu inaongezeka sasa ‘balance’ itatoka wapi”

    Kwamujibu wa meneja huyo ameeleza kuwa uwepo wa maji baridi Duniani ni maeneo machache yaliyo bahatika huku ukanda wa Afrika mashariki ukiwa na kiwango kikubwa kwa asilimia 30 ya majiyote baridi ulimwenguni.

    Hivyo amesisitiza wannchi kujitahidi kutunza vyanzo vya maji asilia kwa kuokoa kizazi kijacho, na kwa wakandarasi waliopo na wanafunzi kuendelea kuvumbua njia mbadala za kupata umeme kwa matumizi machache ya maji.

  • Umoja wa wabangua Korosho wampongeza JPM

    Umoja wa wabangua Korosho wampongeza JPM

    Uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kununua korosho za wakulima na kuzibangua nchini umepongezwa na Umoja wa Wabanguaji Wadogo wa Korosho Tanzania (UWWKT).

    Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa umoja huo, Tumpale Magehema ambapo amesema kuwa uamuzi wa Rais Magufuli una nia ya kuwapa ajira wanachama wake wapatao 2881, jambo ambalo ni la kupongezwa.

    Amesema kuwa uamuzi huo wa kijasiri uliofanywa na Rais Magufuli utaongeza ari ya kufanya kazi na kuchochea ukuaji wa uchumi hasa kwenye mikoa inayolima korosho kwa wingi.

    Kwa upade wake Katibu wa umoja huo, Audax Mkongi, amesema kuwa umoja huo ni asasi mwamvuli ya kitaifa ya wabanguaji wadogo yenye jumla ya vikundi 183 kutoka wilaya tisa za mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Morogoro. baadhi ya wilaya hizo ni Ulanga, Tandahimba, Kisarawe, Liwale na Ruangwa.

    Aidha, naye mgeni rasmi kwenye hafla hiyo iliyofanyika mkoani Lindi, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya ameupongeza umoja huo kwa ari na nia ya kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano ya uchumi wa viwanda.

    Manyanya pia amewahakikishia ushirikiano kutoka wizara yake na kwa kuanza serikali inaandaa utaratibu wa kuutumia ili kuingia nao mikataba ya kubangua korosho iliyonunuliwa na serikali msimu huu.

     

  • Vigogo watano wa WETCU watupwa jela

    Vigogo watano wa WETCU watupwa jela

    Vigogo watano wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka minne kila mmoja, baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili likiwemo la kukisababishia chama hicho hasara ya zaidi sh. milioni 109.

    Vigogo hao ambao walitiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Tabora, mbele ya Hakimu Mkazi, Tengwa Chiganga na kupewa adhabu hiyo, watatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani kutokana na adhabu za kifungo.

    Waliotiwa hatiani na kupewa adhabu hiyo ni  pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Mkandala Mkandala, Kaimu Meneja Mkuu, John Kusanja, Mhasibu mkuu, Prosper Mbacho, Francis Mpeta na  Makamu Mwenyekiti, Msafiri Ngassa ambao walipelekwa katika gereza la Uyui kuanza kutumikia adhabu ya kifungo.

    Aidha, mahakama hiyo iliwaachia huru washitakiwa wawili katika kesi hiyo, Hamza Kapela na mfanyabiashara, Faraz Abbas ama Faraz Yaseen Abbasi, kutokana na upande wa jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.

    Hata hivyo, washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka manne ambayo ni kula njama ya kutenda kosa, kughushi, matumizi mabaya ya madaraka kwa kununua gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 bila kupata kibali kutoka kwa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini na kukisababishia chama hicho hasara ya sh. 109,010,000 kutokana na kununua gari  hilo.

     

  • BANDARI TANGA KUHUDUMIA SHEHENA YA NCHI SABA KWA KUTUMIA MPAKA MMOJA

    BANDARI TANGA KUHUDUMIA SHEHENA YA NCHI SABA KWA KUTUMIA MPAKA MMOJA

    Bandari ya Tanga inaelezwa kuwa bandari ya kipekee na ya aina yake barani Afrika inayoweza kuhudumia nchi saba kwa kutumia mpaka mmoja.

    Hayo yameelezwa na Meneja wa bandari hiyo, Percival Salama, ofisini kwake jijini Tanga wakati akizungunza na waandishi wa habari kuhusu maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika kuhakikisha wanaongeza ufanisi wa bandari hiyo.

    Meneja wa bandari hiyo, Percival Salama,akizungumza na Waandishi wa habari juu ya mipango ya kuboresha bandari ya Tanga na mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitatu ya Rais Magufuli.

    Amesema mbali na kuwa na uwezo wa kuhudumia nchi saba bandari ya Tanga kijografia ina sifa ya kuwa bandari pekee ya asili kutokana na kuwa na kina cha maji cha asili cha kuanzia mita tano hadi 30 huku ikizungukwa na visiwa vya asili ambavyo husaidia kupunguza nguvu ya mawimbi.

    “Serikali ya awamu ya tano kwa kuona upekee wa bandari ya Tanga iliamua kutoa fedha za kuwekeza katika miradi ya uboreshaji ili kuongeza ufanisi,” amesema.

    Salama alifafanua kuwa maboresho makubwa ya bandari hiyo ambayo kwa sasa inaongoza kuwa bandari inayohudumia mizigo kwa kasi Afrika Mashariki, yamefanyika katika nyanja ya ukatabati na ununuzi wa mitambo mipya, ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhia mizigo, na uboreshaji wa mifumo ya teknolojka ya habari na maaasiliano.

    Amesema kwa upande wa mitambo tayari imeshaanza kuwasili ambapo kati ya mitambo 20 iliyonunuliwa mitano imeshawasili bandarini hapo na wanatarajia kupikea mingine miwili siku chache zijazo na kwamba hadi kufikia Julai mwakani mitambo yote
    itakuwa imewasili.

    Alitaja mitambo iliyowasili kuwa ni mashine mbili za kupakia na kushusha makontena yenye uwezo wa kubeba tani 45 kila moja, mashine moja ya kupakia na kushusha mizigo kwenye majahazi na yadi ya uwezo wa tani 30, Fork lift moja ya tani 16 pamoja boti moja ya doria.

    Aliongeza kuwa katika uboreshaji wa  miundombinu ya kuhifadhia mizigo Disemba 3 mwaka huu wameanza mradi wa uboreshaji wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia shehena yenye mita za mraba 13,000, mnara wa kuongozea meli, uwekaji sakafu na sehemu ya kulia chakula na kwamba utakamilika Machi 2020.

    Aidha alisema serikali kwa kupitia TPA imenunua mdaki unaotembea (mobile scanner) ambao umerahisisha zoezi la uondoshaji mizigo bandarini ambao unaweza kuhudumia makasha 80 hadi 100 kwa saa.

    “Kutokana na kuwa na mdaki huu sasa hivi mzigo ukitoka kwenye meli unaingizwa moja kwa moja kwenye mdaki kukaguliwa na kisha unaenda kuhifadhiwa tayari kwa mteja kuja kuchukua baada tu ya kukamilisha nyaraka zake za uondoshaji,” amesema Salama.

    Amesema kutokana na maboresho hayo ufanisi umeongezeka kwa kiasi kikubwa ambapo wamefanikiwa kuongeza shehena za mizigo baada ya kuvutia wateja waliokimbia baada ya kutetereka.

    “Mfano ni kampuni ya A to Z ya Arusha ambayo tulipotetereka walituhama lakini sasa wamerudi na inapitisha mizigo yake hapa takribani tani 91 kwa mwezi na tuna hakika hadi kufikia 2020/21 tutakuwa tumewarudisha wateja wote waliohama,” amesema Salama.

    Alisema Bandari ya Tanga ambayo ina lango kubwa kuliko bandari yeyote Afrika Mashariki la mita 1200, inatarajia kuhudumia shehena ya mizigo tani 1,267,000 kwa mwaka 2018/2019 ikilinganishwa na tani 646,718 za mwaka 2017/2018.

    “Mteja anakuja anakaa siku tano anatoa mzigo, kesho hawezi kuja tena lakini sisi hapa mtu akija kuchukua mzigo anaondoka siku hiyo hiyo na meli ikija hapa haisubirishwi kwenye eneo la bahari kama kwenye bandari zingine bali inaingia moja kwa moja kushusha au kupakia mzigo,” alisema Salama.

    Alifafanua kuwa ucheleweshaji wa meli bandarini ni moja ya vikwazo kwa wenye meli kwani anapochelewa anapigwa penati ambapo kwa siku moja ni dola 20,000 hivyo anaongeza gharama za uendeshaji.

    “Sisi hapa mara nyingi tunawahisha meli kabla hata ya muda wa makubaliano ambapo tumekuwa tukipata zawadi mara kwa mara,” aliongeza.

    Awali meli ya tani 40,000 ilikuwa ikihudumiwa kati ya siku sita hadi nane lakini kutokana na maboresho yaliyofanywa bandarini hapo hivi sasa inahudumiwa kwa siku mbili.

    “Bandari chakula chake ni mzigo hivyo, jitihada zetu ni kupunguza muda wa kuhudumia na wateja wanaangalia ubora wa huduma na kazi kubwa iliyofanyika katika bandari yetu ni kuboresha eneo la vifaa kwa sababu shida kubwa ilikuwa kwenye mitambo
    iliyosababisha uondoshwaji wa mizigo kuchukua muda mrefu,” alisema.

    Kuhusu mapato alisema kwa mwaka 2018/2019 bandari hiyo imepangiwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 25 hivyo wameweka nguvu kubwa kuboresha miundombinu na kununua mitambo ya kisasa kufanikisha malengo hayo.

    Akizungumzia kuhusu miradi mikubwa iliyopangwa kufanyika Salama alisema tayari wameanza kufanyia kazi agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuchimba na kuongeza kina cha bandari hiyo hadi kufikia kina cha mita 15.

    Alisema tayari wamefanya utafiti wa aina ya udongo uliopo ambapo kazi oliyofanywa na kampuni ya BIKO ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

    “Tumegundua kuwa taarifa zilizokuwepo kwa miaka mingi kuwa kuna jiwe si za kweli na kwamba kilichopo ni mchanga na udongo aina ya mfinyanzi na sasa tunatarajia kufanya usanifu na kumtafuta mhandisi mshauri ili tuanze kuchimba,” alisema.

    Mradi mwingine ni wa ujenzi wa matanki ya kuhifadhia mafuta kutokana na kuwepo kwa mradi wa bomba la maguta kutoka Ohima Uganda hadi bandarini hapo eneo la Chongoleani litajengwa gati ya mafuta itakayowezesha meli kubwa za kubeba tani 100,000 hadi 250,000.

    “Kwa kuweza kupokea meli za aina hii bandari ya Tanga itakua ndio yenye uwezo wa kupokea meli kubwa kuliko bandari yeyote Afrika na huku ni kuelekea kuwa Hub ya ukanda wa Mashariki na kati,” alisema Salama.

    Alisema bandari ya Tanga ina fursa kubwa ya kufanyiwa upanuzi kutokana na kuwa na ghuba nne zenye eneo la maji la mita za mraba milioni 35.

    “Eneo hili ni sawa na bandari 12 za nchi jirani hivyo unaweza kuona fursa iliyopo kwenye bandari yetu ya Tanga,” aliongeza.

    Akizungumza kuhusu changamoto katika bandari hiyo alisema ni uwepo wa bandari bubu ambazokwa mujibu wa tathmini wamebaini uwepo wa bandari bubu 48 kwenye wilaya nne, 12 zikiwa wilaya ya Mkinga, 20 Tanga mjini, moja Muheza, na 15 wilaya ya Pangani.

    Alisema uwepo wa bandari bubu unaikosesha mapato serikali pamkna na kuhatarisha usalama wa nchi.

    “Bandari ni mipaka ya nchi hivyo kuwepo kwa uingizaji na uondoshaji wa mizigo usiosimamiwa ni kuhatarisha usalama wa nchi kwasababu wanaweza kuingiza bidhaa zisizo ruhusiwa ikiwemo silaha,” alisema.

    Hata hivyo alisema wamefanikiwa kwa kiasi fulani kudhibiti bandari hizo baada ya kutoa elimu kwa wananchi na kufanya doria za mara kwa mara kwa kutumia boti yetu ambayo ni mpya.

    Alisema tayari wameanza kuona mafanikio ya udhibiti wa bandari bubu ambapo mapato yanayotokana na majahazi yameongezeka kutoka Sh
    milioni 26 kwa mwezi hadi Sh milioni 63 kwa bandari ya Tanga na kutoka Sh milioni 2.5 hadi Sh milioni 8 hadi 9 kwa bandari ya Pangani huku lengo likiwa ni kufikia Sh milioni 12.

    Aidha alitoa wito kwa wananchi kutumia bandari rasmi ambazo ni Tanga na Pangani kwasababu ni gharama za chini kabisa kuliko bandari bubu ambazo wanaweza kukamatwa na mali zao kutaifishwa.

    Alisema katika mpango wa kutaka kurasimisha bandari hizo zipo bandari nne ambazo zinaweza kurasimishwa ambazo ni Mkwaja, Kipungwi, Kikombe na Moha.

    Bandari ya Tanga ikonekana kwa juu kama ilivyopigwa na Mpiga picha wetu alipotemblea Bandari hiyo
    Mdaki mpya wa kukagua mizigo uliopo katika Bandari ya Tanga
  • Uwekezaji katika sekta ya madini waongezeka

    Uwekezaji katika sekta ya madini waongezeka

    Waziri wa Madini, Angela Kairuki amesema kuwa uwekezaji katika sekta ya madini umeongezeka, hasa kwa wawekezaji wa nje kutoka katika kipindi cha miaka miwili iliyopita tangu sheria ya madini ya mwaka 2010 ifanyiwe marekebisho na kuanza kutumika mwaka 2017.

    Akizungumza mara baada ya kongamano la uwekezaji katika sekta ya madini kati ya Tanzania na China lililofanyika Beijing nchini China Jumatatu wiki hii, Kairuki alisema kasi ya uwekezaji katika sekta ya madini imeendelea kuongezeka baada ya kufanya marekebisho hayo ya sheria na hivyo kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa ujumla,..

    “Wizara yangu inafanya kila liwezekanalo katika kuvutia uwekezaji wa sekta ya madini,  kwa sasa tunalo ongezeko kubwa kwenye uwekezaji huo na hii inatokana na marekebisho ya baadhi ya sheria ambazo zilipitwa na wakati,” amesema Kairuki.

    Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Geoffrey Mwambe amesema kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, na akaeleza kwamba ofisi yake haijapokea ombi lolote la mwekezaji kutaka kufuta uwekezaji wake nchini kama inavyodaiwa na vyombo vya habari vya Magharibi.

    Akizungumza kwa niaba ya wawekezaji kutoka China, Mwenyekiti wa Kampuni ya SunShine iliyowekeza katika sekta mbalimbali nchini, Tony Sun amesema kuwa ameridhishwa na mapinduzi makubwa yanayofanywa na Serikali kwa sasa kwenye sekta ya madini, ambayo yamelenga kunufaisha wawekezaji pamoja na watanzania kwa ujumla.

    Kongamano la Uwekezaji katika sekta ya madini ambalo limeandaliwa na Wizara ya Madini Tanzania kwa ushirikiano na Kituo cha Uwekezaji nchini, pamoja na Ubalozi wa Tanzania nchini China, umekutanisha watendaji wa serikali na sekta binafsi kutoka China na Tanzania. Ujumbe wa China umeongozwa na Naibu Waziri wa Maliasili, Ling Yueming, kushirikiana na Kituo.

  • Mafuriko ya wasafiri, Wamiliki wa Mabasi waililia Serikali

    Mafuriko ya wasafiri, Wamiliki wa Mabasi waililia Serikali

    Kutokana na idadi kubwa ya abiria waliofurika katika vituo vya mabasi yaendayo mikoani kwa lengo la kusafiri katika msimu huu wa sikukuu za Christmas na Mwaka Mpya, wamiliki wa mabasi wameiomba Serikali kuzingatia ushauri wao ili kumudu hali iliyopo.

    Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), Enea Mrutu ameiomba Serikali kuruhusu mabasi ya abiria kusafiri usiku na mchana. Ameiomba Serikali kuongeza ulinzi kwa mabasi yanayotoka Dar es Salaam ili yasilale Shinyanga na badala yake yaruhusiwe kuingia Mwanza. Kadhalika, mabasi yanayotoka Mwanza kuelekea Dar es Salaam yasilale Morogoro kwa sababu ya usiku.

    “Kwa mfano kutoka Shinyanga kwenda Mwanza kinachotakiwa pale ni kuongeza ‘patrol’ (doria) na kuhakikisha maeneo yote ya mizani kunakuwa na mtu wa kupima uzito wa magari na madereva wa mabasi na maroli kama wanatumia vilevi,” Mtanzania wanamkariri Mrutu.

    Aidha, Mrutu aliitaka Serikali kuachana na mpango wake wa kusajili magari kwa ajili ya kuyaruhusu kusafirisha watu ili kuendana na mahitaji makubwa ya usafiri akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha matatizo zaidi kwani madereva wa magari hayo hawana uzoefu na magari yao hayajafungiwa ving’amuzi vya kudhibiti mwendo (GPS).

    Alisema badala yake Serikali ipunguze vizuizi na vituo ambavyo havina ulazima wa mabasi kuingia ikiwa hayana abiria ili kuokoa muda.

    Katika hatua nyingine, Meneja wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo, Imani Kasagala amesema kuwa kuna viashiria kuwa mwaka huu kutakuwa na abiria wengi zaidi ya mwaka jana kwani katika theluthi ya kwanza ya kipindi hiki cha sikukuu tayari idadi imeanza kuwa kubwa, tofauti na mwaka jana ambapo idadi kubwa ilianza kuonekana katika theluthi ya pili.

  • William Ole toa neno Simanjiro, asisitiza ushirikiano

    William Ole toa neno Simanjiro, asisitiza ushirikiano

    Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha ameitaka Serikali ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara kuhakikisha inahusisha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA katika ujenzi wa Chuo cha VETA Simanjiro ili miundombinu ya chuo hicho iweze kujengwa kwa utaratibu na viwango vinavyohitajika.

    Ametoa agizo hilo Mkoani Manyara wakati akikagua eneo ambalo Serikali ya Wilaya hiyo inategemea kujenga Chuo cha Veta kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Hiari ECLAT.

    Amesema kuwa ni vizuri Mamlaka husika zikahusishwa katika ujenzi wa Chuo hicho tangu hatua za awali na kumtaka Mkurugenzi wa VETA kanda  na yule wa Mkoa kufika katika eneo la Emboreet ambako mradi utajengwa kwa lengo la kuongea na wananchi pamoja na wafadhili wa mradi huo ili wazo ambalo limeanza liweze kutekelezwa kwa utaratibu unaostahili.

    “Ninyi Halmashauri mnataka kujenga chuo cha Ufundi ni wazo zuri lakini ni lazima kijengwe kwa utaratibu sio kiholela kwa sababu vilianza kuibuka vyuo ambavyo mtu anakuwa na jengo moja anasajili kinaitwa chuo, kuna viwango na masharti ambayo ni lazima yatimizwe kabla chuo kuruhusiwa kufanya kazi, fuateni taratibu hizo ili muweze kuanzisha chuo cha Ufundi,” amesema Ole Nasha.

    Aidha, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeweka mkazo mkubwa katika Elimu ya Ufundi kwa kuwa kuna vijana wengi wanaomaliza shule wanaishia kutokuwa na ajira kwa kuwa hawana maarifa yanayowasaidia

  • Biashara ya kubadili fedha za kigeni kudhibitiwa

    Biashara ya kubadili fedha za kigeni kudhibitiwa

    Mamlaka nchini zimeazimia kuendeleza kampeni ya kudhibiti biashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni nchini ili “kuzuia kuyumba kwa sekta ya fedha”.

    Mwezi uliopita, Benki kuu (BoT) iliyafunga zaidi ya maduka 100 ya kubadili fedha jijini Arusha kwa kutokukidhi masharti ikiwemo kutokuwa na leseni halali za biashara.

    Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Gavana wa BoT Profesa Florens Luoga amesema operesheni hiyo haitakoma, na huenda mji mkuu wa kibiashara Dar es Salaam ukafuata baada ya Arusha.

    “Hatuhitaji maduka 100 ya kubadilisha fedha Dar es Salaam, kwani kuna benki za kutosha. Tunahitaji maduka ya fedha kwenye sehemu muhimu kama kwenye mahoteli ya kitalii na mipakani,” amesema Luoga kwenye mkutano wa Rais John Magufuli na Wakuu wa Mikoa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na viongozi wengine waandamizi wa serikali.

    “Udhibiti utaendelea kuwa mkali. Hii ni moja ya hatua zitakazoendelea, kanuni ambazo zilikuwepo ziliongeza udanganyifu na maduka yakazidi kuongezeka kiholela,” ameongeza Luoga.

    Katika operesheni iliyofanyika Arusha mwezi uliopita BoT ilitumia askari kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

    Kutumika kwa askari wa JWTZ kwenye msako huo kulishtua watu wengi na ikamlazimu Luoga kutoa ufafanuzi baadaye.

    Kwa mujibu wa Luoga BoT ilitumia wanajeshi “kufuatia askari wengi wa Jeshi la Polisi kuwa katika usimamizi wa mitihani ya kidato cha pili,” na taasisi yake ilihusisha askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wasio na silaha ili kuongeza nguvu katika kufanikisha zoezi hilo.

    Kabla ya operesheni hiyo ya kushtukiza, kulishafanyika operesheni nyengine mbili za awali na maofisa wa BoT ambazo hazikuzaa matunda.

    Wakati msako wa Arusha ukifanyika, thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani ilikuwa imeshuka maradufu na kufikia Sh2,300 kwa dola moja. Mara ya mwisho kwa kiwango hicho kufikiwa ilikuwa Julai 2015 na BoT ililazimika kuchukua hatua mahususi kukabiliana na anguko hilo.

    Kwa mujibu wa tovuti ya BoT dola moja ya Marekani kwa hii leo Sesemba kumi imekuwa ikibadilishwa kwa shilingi 2,290.

    Wiki mbili zilizopita, BoT ilizipiga marufuku benki tano kuendesha biashara ya sarafu za kigeni kwa muda wa mwezi mmoja kwa kukiuka sharia.

    Benki ya Barclays Tanzania, Exim Bank, UBA Bank, BancABC na Azania Bank zote zilipigwa marufuku ya kuendesha biashara hiyo Novemba 23 kwa kukiuka sheria za biashara, kwa mujibu wa Alexander Ng’winamila, mkurugenzi wa masoko ya fedha katika benki kuu.

    “Benki zilizopigwa marufuku aidha zilifanya biashara nje ya viwango vya masoko au hazikuwasilisha kwa Benki Kuu rrekodi za biashara zao, suala ambalo ni kinyume na sheria,” Ng’winamila aliliambia shirika la Reuters.

  • Serikali yalipa zaidi ya shil. bilioni 83 kwa wakulima wa Korosho

    Serikali yalipa zaidi ya shil. bilioni 83 kwa wakulima wa Korosho

    Serikali imesema kuwa mpaka sasa imelipa zaidi ya shilingi bilioni 83 kwa wakulima wa Korosho katika mikoa ya Lindi, Mtwara, pamoja na Ruvuma huku zaidi ya wakulima 82,835 kutoka mikoa hiyo wakiwa wamepatiwa fedha zao.

    Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ambapo amesema kuwa Jumla ya fedha iliyolipwa kwa wakulima hao ambao tayari wamefanyiwa uhakiki katika Mkoa wa Mtwara pekee ni 50,835, Lindi wakulima 22,131 na Mkoa wa Ruvuma ambao takribani wakulima 9,445 wamelipwa.

    Ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa wabanguaji wadogo wa korosho wa mikoa mitano ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Morogoro, ambapo amesema jumla ya vyama 328 vimefanyiwa uhakiki kati ya vyama 504 vilivyopo katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma, jumla ya vyama 319 vimekwishalipwa.

    Aidha, amesema kuwa kikao hicho kina lengo la kujadiliana na kukubaliana utaratibu uliopangwa na serikali katika ubanguaji wa korosho mwaka 2018/2019 kwa kuelekeza ubanguaji kufanyika nchini ili kuwanufaisha wananchi katika ajira hiyo.

    “Tumeiona changamoto ya mitaji kwa wabanguaji wadogo nchini sambamba na wabanguaji wakubwa hivyo ili serikali iwarahisishie upatikanaji wa mitaji tumeamua kuwapa kazi nyinyi wenyewe,” amesema Japhet Hasunga.

    Hata hivyo, ameongeza kuwa suala la uhakiki limejikita zaidi kubaini udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wahujumu wa biashara ya korosho.

  • MKURUGENZI WA BOT TAWI LA DODOMA AFUNGUA SEMINA YA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MASUALA YA UCHUMI NA FEDHA JIJINI DODOMA

    MKURUGENZI WA BOT TAWI LA DODOMA AFUNGUA SEMINA YA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MASUALA YA UCHUMI NA FEDHA JIJINI DODOMA

    Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania tawi la Dodoma Bw. Richard Wambali aliyemwakilisha Dkt. Yamungu Kayandabila  Naibu Gavana anayeshughulikia Uchumi na Fedha akifungua  semina ya siku tano ya  waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kuhusu masuala ya uchumi na fedha inayofanyika kwenye ukumbi wa (BOT) jijini Dodoma.

    Katika semina hiyo wanahabari watapata ufafanuzi wa masuala  yanayoshughulikiwa  na benki hiyo pamoja na  mabenki ya biashara ya kifedha nchini Tanzania kwa kufuata sheria kanuni na taratibu zinazosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Bi Zamaradi Kawawa na kushoto ni Bi. Zalia Mbeo Meneja Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki (BOT).

    Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Bi Zamaradi Kawawa akizungumza katika semina hiyo inayofanyika kwenye tawi la Tenki Kuu jijini Dodoma katikati ni Mkurugenzi wa Benki Kuu Tawil la Dodoma Bw. Richard Wambali na kulia ni Bi. Zalia Mbeo Meneja Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki (BOT).
    Kaimu Meneja wa Idara ya Uhusiano na Itifaki, BoT, Bi. Vicky Msina akitoa maelezo ya utangulizi wa semina hiyo kabla ya kufunguliwa rasmi na Mkurugenzi wa Benki Kuu Tawi la Dodoma Bw. Richard Wambali.
    Dkt. Suleiman Missango, Meneja Msaidizi-Idara ya Utafiti, Kurugenzi ya Sera za Uchumi na Utafiti, BoT akiwa na watoa mada wengine kutoka benki kuu tayari kwa kutoa mada katika semina hiyo.
    Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika semina hiyo
    Kaimu Meneja wa Idara ya Uhusiano na Itifaki, BoT, Bi. Vicky Msina akiwa pamoja na wanahabari wanaohudhuria semina hiyo.

  • Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Tanzania

    Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Tanzania

    Rais Dkt. John Pombe Magufuli akutana na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia kanda ya Afrika Dkt. Hafez Ghanem ambaye ametangaza kuwa Benki ya Dunia imeridhia kutoa Dola za Marekani milioni 300 kwa ajili ya mradi wa kuongeza ubora wa elimu ya Sekondari.
    Katika Mazungumzo hayo:
    Benki ya Dunia imeridhia kutoa Dola za Marekani Milioni 300 sawa na shilingi Bilioni 680.5 kwa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuongeza ubora wa elimu ya sekondari unaokusudiwa kujenga vyumba vya madarasa, mabweni, maabara, nyumba za watumishi na kununua vifaa vya kufundishia.
    Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Hafez Ghanem aliyekutana na Mhe. Rais Magufuli tarehe 16 Novemba, 2018 Ikulu Jijini Dar es Salaam amesema pamoja na kuridhia kutoa fedha za mradi huo, Benki hiyo inaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 5.2 sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 13 na kwamba miradi hiyo inatekelezwa kutokana na uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania.

    Dkt. Hafez Ghanem amesema katika mazungumzo hayo wamejadili juu ya maendeleo ya miradi hiyo na kazi nzuri ambayo inafanywa na Tanzania kuimarisha uchumi, na pia amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa matokeo mazuri ya mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha huduma za kijamii.
    Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano na uhusiano mzuri na Tanzania na ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kukuza uhusiano huo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika kwa miradi iliyokusudiwa.
    “Namshukuru Dkt. Hafez Ghanem na Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Tanzania, hizo Dola Milioni 300 ambazo baadhi ya watu wasiotutakia mema walisema zimefyekelewa mbali, anasema zitaletwa, na pia Benki ya Dunia imetoa Dola Bilioni 5.2 ambazo zinafadhili miradi mbalimbali ya elimu, nishati, barabara, kilimo, afya na maji, ni miradi mikubwa na mingi.
    “Kwa hiyo amekuja kututhibitishia kuwa Benki ya Dunia haitatuacha” amesema Mhe. Rais Magufuli.

    cc;Ikulu