Category: Local News

  • Mahakama Kuu yawaita Zitto na Spika Ndugai

    Mahakama Kuu yawaita Zitto na Spika Ndugai

    Mahakama Kuu ya Tanzania, imetoa wito kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kufika mahakamani hapo leo, kesi ya Kikatiba kuhusu madaraka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) itakapotajwa.

    Zitto akishirikiana na mwanasheria wake, Fatma Karume alifungua kesi hiyo iliyosajiliwa kwa namba 01/2019, akiiomba Mahakama kutoa tafsiri ya Ibara ya 143(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

    Alifungua kesi hiyo akipinga hatua ya Spika Ndugai kumuita CAG, Profesa Mussa Assad ili ahojiwe na Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kuhusu kauli yake aliyoitoa akiwa nchini Marekani katika mahojiano na chombo cha habari cha Umoja wa Mataifa, kuwa “kama Bunge halifanyii kazi ripoti zangu, huo ni udhaifu wa Bunge.”

    Januari 21, CAG aliitikia wito wa Spika Ndugai na kuhojiwa na Kamati hiyo ya Bunge ambayo ilisema kuwa utaratibu mwingine unaendelea baada ya mahojiano hayo.

    Kesi hiyo inatajwa leo huku ikiwa imepangiwa jopo la majaji watatu, Jaji Firmin Matogolo, Dkt. Benhajj Masoud na Elinaza Luvanda.

  • Serikali  yaapa kuwanasa wauaji, yadai yamechochewa na ushirikina

    Serikali yaapa kuwanasa wauaji, yadai yamechochewa na ushirikina

    Serikali ya  imeahidi kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuhusika katika mauaji ya watoto mkoani Njombe.

    Waziri Kangi Lugola amesema tayari serikali imepata majina ya wote waliohusika katika mauaji ya watoto Njombe.

    Watoto sita, wakiwemo watatu wa familia moja wenye umri chini ya miaka 10 wamepatikana wakiwa wamefariki katika mazingira ya kutatanisha mkoani humo.

    Akizungumza Bungeni leo, Waziri wa Mambo ya Ndani nchi, Kangi Lugola amesema tayari wameshabaini baadhi ya wale waliohusika na mauaji hayo na hatua kali zitachukuliwa.

    “Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mauaji hayo yametokana na imani za kishirikina…n tayari tumeshawabaini baadhi ya wale ambao wameshiriki. Nawataka watu waache kuichezea serikali. Tutaanza na mkoa wa Njombe,” ameonya Lugola.

    Lugola hata hivyo hakusema ni watu wangapi mpaka sasa wametiwa mbaroni kutokana na mauaji hayo.

    Vurugu Njombe

    Siku ya Jumanne, polisi mkoani Njombe walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi walioandamana katika baadhi ya mitaa wakimtaka mtu anayedaiwa kuwa ni mtekaji wa watoto mkoani humo.

    Umoja wa Mataifa (UN) umetoa tamko kuhusu mauaji hayo ikisema inaungana na serikali ya kulaani ‘unyama’ huo waliofanyiwa watoto.

    Tamko lililotolewa na UN leo Jumanne Januari 29, 2019 limekemea mauaji hayo ikieleza kuwa hayakubaliki na kubainisha kuwa watoto wana haki ya msingi ya kulindwa kutokana na vurugu ili waweze kufurahia na kupata mahitaji yao muhimu.

    “Umoja wa mataifa unaungana na Serikali  kupinga vitendo hivyo vibaya. Kama UN tupo tayari kusaidia Serikali katika jitihada zao za kukabiliana na tatizo hilo,” inaeleza taarifa hiyo ikimnukuu mratibu mkazi wa UN hapa nchini, Alvaro Rodriguez.

    “Zaidi ya hayo tunatoa wito kwa wadau wote kuungana pamoja kuhakikisha kunakuwa na usalama wa watoto kuanzia katika makazi, shule na maeneo mengine miongoni mwa jamii.”

    Watoto wanapitia katika aina nyingi za unyanyasaji katika maeneo mengi duniani, “Hili linatakiwa likome,” amesema mwakilishi wa Unicef nchini , Maniza Zaman.

  • Mauaji ya watoto tishio mjini Njombe, wananchi waiangukia serikali

    Mauaji ya watoto tishio mjini Njombe, wananchi waiangukia serikali

    Wananchi Mjini Njombe wameiomba Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kudhibiti vitendo vya mauaji ya watoto wenye umri kati ya miaka 4-9 ambavyo vinatajwa kuongezeka tangu mwezi disemba mwaka jana na kuendelea kutishia hali ya usalama mjini humo.

    Wananchi hao wametoa rai hiyo baada ya mwili wa mtoto mwingine wa jinsia ya kiume kuokotwa kando ya msitu wa asili wa Nundu ulioko nje kidogo ya mji wa Njombe.

    “Ni kweli kuna mtoto mwingine amekutwa amefariki pale msituni, tulipofika pale tulitoa taarifa kwa polisi wa kituo cha Uwemba na walivyokuja ni kweli walishuhudia mwili wa mtoto na wakauchukua na kuupeleka mochwari,”amesema Winfrid Mbangala mwenyekiti wa kijiji cha Nundu

    Aidha, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe Dkt. Barnaba Baraka amekiri kuupokea mwili wa mtoto huyo na kueleza kuwa bado unafanyiwa uchunguzi huku jeshi la polisi mkoani humo likieleza kuwa taarifa ya tukio hilo bado haijakamilika.

  • Kabati akabidhi viungo bandia kwa walemavu Iringa

    Kabati akabidhi viungo bandia kwa walemavu Iringa

    Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati kupitia programu ya ‘Peoples Empowerment Foundation’ chini ya Kampuni ya Camal Group amefanikisha kuwakabidhi viungo bandia walemavu 10 wa miguu kutoka wilaya tofauti za mkoa huo ambao walikosa msaada na kulazimika kuishi wakiwa na upungufu wa viungo vya mwili.
     
    Hayo yamesemwa na Mratibu wa Ofisi ya Mbunge huyo ambapo amesema kuwa Mh. Ritta Kabati alifanya ziara ya kikazi katika mkoa wa Iringa na kubaini uwepo wa walemavu zaidi ya 110 wa viungo mbalimbali vya mwili.
     
    Mratibu huyo wa Mbunge Kabati amesema kuwa zoezi la kuwakabidhi walemavu hao viungo bandia lilifanyika January 20 mwaka huu Jijini Dar es laam na lilidhaminiwa na kampuni ya Camal Group na Mgeni rasmi katika shughuli hiyo alikuwa naibu waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Kazi Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Stela Ikupa.
     
    “Mbunge alifanya ziara katika mkoa wa Iringa ndipo alipobaini uwepo wa hawa hatu wenye mahitaji maalumu tuliwapata watu zaidi ya 110 kutoka wilaya tofauti za mkoa wa Iringa lakini leo tumekuja na wahitaji 10 wa viungo vya miguu ambao wanakabidhiwa viungo hivi,”amesema Mgongo
     
    Kwa upande wao baadhi ya wahitaji waliopata viungo hivyo bandia wamemshukuru Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Iringa, Ritta Kabati kwa kufanikisha kuwatafutia viungo hivyo kisha kuwasafirisha kutoka Iringa hadi Dar es laam kuwakabidhi viungo ambavyo vitawasaidia kuishi na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.
    Katika hatua nyingine Ofisi ya Mbunge huyo imetoa shukrani kwa Mkurugenzi wa manispaa ya Iringa kwa kutoa ushirikiano wakutosha ikiwemo kuwasafirisha wahitaji hao hadi Dar es laam kufanikisha jambo hilo na kuwaomba wadau wengine mkoani humo kujitokeza kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu.
  • Mafao yamponza mstaafu auawa na ‘House boy’

    Mafao yamponza mstaafu auawa na ‘House boy’

    Vijana wengi wamekuwa na tamaa ya kupata fedha nyingi na kwa haraka zaidi hali ambayo inawapelekea kufanya matendo yanayohatarisha maisha ya watu wengine ikiwemo kujichukulia hatua mkononi kupoteza maisha ya watu wengine.

    Vijana wengi wamekuwa wakipita njia za mkato kusaka pesa hali ambayo inawagharimu sana, kufuatia tabia hiyo kijana mmoja ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa ndani ‘House boy’ inasemekana ameyachukua maisha ya mwajiri wake ambaye alikuwa ni mstaafu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Tunsume Sakajinga ambaye ameuawa vibaya kwa kupigwa na kitu kizito kichwani kisha kuchomwa na mkasi ambao uliachwa shingoni mwake.

    Taarifa za mashuhuda wa tukio hilo ambao ni majirani wa mstaafu huyo ni kwamba kijana huyo aliamua kufanya tukio hilo la kinyama akiwa na lengo la kuchukua fedha za mafao ambazo alihisi mwajiri wake amezificha ndani kwani siku chache mara baada ya kustaafu, mama huyo amekuwa akifuatilia mafao yake.

    Polisi Mkoa wa kipolisi Temeke, Emmanuel Lukula amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na bado taarifa za kiuchunguzi zaidi zinaendelea hasa kubaini nani hasa alihusika na mauaji hayo kwani bado haijathibitikwa kisheria kuwa kijana huyo amehusika na mauaji hayo.

    Aidha kaka wa marehemu, Kisa Mwankusye amesema kuwa bado wanasubiri uchunguzi ukamilike na kukabidhiwa mwili kwa ajili ya mazishi ambayo yamepangwa kufanyika katika kijiji cha Kasanga, Rungwe mkoani Mbeya.

    Majirani na watu wa karibu wa nyumba hiyo wamesema kuwa mama huyo alikuwa anaishi vizuri na kijana huyo ambaye alikuwa akisaidia kazi za nyumbani na hawajawahi kusikia malumbano ya aina yeyote kati ya wawili hao zaidi tu kijana huyo alikuwa mnyenyekevu na mwenye kutimiza majukumu yake ya hapo nyumbani.

    Marehemu Tunsume Sakajinga aliishi na kijana huyo kwa muda wa miaka mitatu mpaka mauti kumkuta.

    Roho ya marehemu Tunsume Sakajinga ipumzike kwa amani.

     

  • Rais Magufuli astopisha bomoa bomoa makazi holela

    Rais Magufuli astopisha bomoa bomoa makazi holela

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ameendelea kusisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano ni Serikali inayojali wananchi wake hivyo kuanzia sasa amesitisha zoezi zima la kubomoa makazi ya watu yaliyojengwa bila kufuata mpango mji.

    Rais ameelekeza kuwa nyumba hizo zisibomolewe kwa kuwa hayakuwa makosa yao kujenga katika maeneo hayo na kuelekeza kuwa watu wote wasio na hati miliki za ardhi kufanyiwa urasimishaji wa makazi yao.

    ”Serikali ya awamu ya tano kuanzia sasa haitabomoa tena nyumba za wananchi waliojenga maeneo ya makazi yasiyo rasmi badala yake itarasimisha makazi holela” Amesema Rais Mgufuli.

    Hayo yamekaziwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo na Makazi, William Lukuvi alipokuwa wilayani Simanjiro mkoani Manyara akifanya ziara yake ya kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi kwa wakazi wa mji huo, ambapo amewataka wananchi wote wachangamkie fursa hiyo iliyotolewa na Rais.

    “Serikali ya awamu ya tano inajali sana wananchi wake kwakuwa zamani wananchi ambao hawakujenga kwa kufuata mipango miji wangebomolewa nyumba zao, lakini kwa sasa imeanzisha mpango kurasimisha makazi holela na kuwapatia hati wananchi wote waishio mijini ili waishi katika makazi rasmi”, amesema Lukuvi.

    Pamoja na hayo Lukuvi amewataka wananchi wote waishio mijini kuwa wazalendo kwa kurasimisha maeneo yao waweze kujipatia hati na ili walipe kodi ya pango la ardhi jambo ambalo litaiongezea Serikali mapato

     

  • Maporomoko ya Mto Ruhuji kuanza kuzalisha umeme

    Maporomoko ya Mto Ruhuji kuanza kuzalisha umeme

    Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ameruhusu kuanza mchakato wa ujenzi wa mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Ruhuji mkoani Njombe utakaozalisha megawati 358, kwa lengo la kuwa na hazina kubwa ya nishati ya umeme ambao utauzwa katika nchi jirani ikiwemo Zambia, Kenya na Uganda.
     
    Ameyasema wakati akiwasha umeme katika vijiji vinne vinavyopitiwa na ujenzi wa mradi wa umeme wa Makambako -Songea ikiwa na pamoja na kijiji cha Ngalanga, Lyamkena, Ilembela na Magoda wilayani Njombe, ambapo amesema kuwa jitihada kubwa na maamuzi magumu yanayochukuliwa na serikali ya awamu ya tano katika ujenzi wa miradi mikubwa ya umeme zina lengo la kuwa na kiwango kikubwa cha nishati ambayo itaweza kuuzwa nchi jirani zenye uhitaji.
     
    Amesema kuwa serikali imepanga ifikapo mwaka 2020 vijiji vyote elfu 12 vya Tanzania viwe vimewashwa umeme na hivyo kufungua milango kwa watalaamu binafsi wenye ujuzi wa kuzalisha umeme kuanza kutumia ujuzi wao kuanzisha miradi kwa manufaa ya taifa.
     
    “Tayari serikali yetu ina mpango wa kuanzisha mradi mkubwa wa umeme katika maporomoko ya mto Ruhuji hapa Njombe, hizi ni jitihada kubwa zinazofanywa na raisi wetu Dkt. John Pombe Magufuli na sisi kama wizara ya nishati tupo pamoja naye katika kuhakikisha mipango hii inafanikiwa kwa haraka,”amesema Mgalu.
     
    Naye mbunge wa jimbo la Njombe Mjini kupitia CCM, Edward Mwalongo amesema kuwa kila mwananchi anapaswa kutumia fursa hiyo kujisajili kwa gharama nafuu kabla gharama halisi hazijaongezwa huku akisikitishwa na wanaobeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kusogeza huduma kwa wananchi.
     
    Kwa upande wao wananchi wa vijiji hivyo ambavyo vimepata umeme kupitia mpango wa REA wamesema kuwa ujio wa nishati ya umeme katika vijiji vyao utakuza uchumi kwa kasi kwa kuwa kumekuwa na viwanda na mashine ambazo wakati mwingine zinashindwa kufanya kazi kwa kuwa zinatumia mafuta.
    Zaidi ya vijiji 120 vinavyopitiwa mradi mkubwa wa Makambako -Songea vipo kwenye mpango wa kuwashwa umeme ikiwa ni utekelezaji wa mpan
  • Mngereza aeleza alivyochangamkia mchongo wa TACIP, ‘inaongeza thamani’

    Mngereza aeleza alivyochangamkia mchongo wa TACIP, ‘inaongeza thamani’

    Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza amejivunia kujiandikisha kwenye Mradi wa Utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi Tanzania (TACIP), ambao amedai umemuongezea thamani kama msanii.

    Akizungumza na Dar24 katika mahojiano maalum, Mngereza ameeleza kuwa akiwa kama msanii wa sanaa ya ufundi pamoja na muziki, mbali na kuwa Katibu Mtendaji, ameamua kuchangamkia fursa ya TACIP kwani inaongeza thamani ya msanii na kumfanya aheshimike kwa kumtambulisha.

    “Mimi ninazungumza kama Katibu Mtendaji, lakini nikiuvua ukatibu mtendaji mimi ni msanii. Nimesomea sanaa ya uchoraji na sanaa ya muziki, nilishafanya shughuli za kuchonga… lakini hapa tunazungumzia sanaa ya ufundi,” alisema Mnengereza.

    “Ukitambulika hadhi yako inapanda, kwa sababu hadhi ya mtu, utambulisho wa mtu ni kitu cha msingi sana. Kwa sababu usipokuwa na utambulisho mtu anaweza kukudharaudharau tu. Lakini kumbe uchoraji, uchongaji, ususi, uchoraji ni kazi ya hali ya juu sana. Mimi nimeona fursa…. ndio nimejiandikisha (TACIP),” aliongeza.

    Kadhalika, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Pili Ngarambe ambaye alizindua utekelezaji wa mradi wa TACIP katika halmashauri hiyo alisema kuwa mradi huo ni fursa ya kipekee kwa wasanii.

    Alisema kuwa mradi huo unaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli ambaye hivi karibuni amewapa wafanyabiashara wadogo vitambulisho ili waweze kutambulika na kuwa rasmi, kwani kuwa tambua wasanii ni wakuwaongezea heshima na kuwapa fursa zaidi.

    Aliipongeza kampuni ya DataVision International kwa kuanzisha na kuratibu mradi huo unaolenga kuwapa fursa nyingi ikiwa ni pamoja na sifa za kukopesheka kwa kutumia kitambulisho cha TACIP.

    TACIP ni mradi wa utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi nchini ambao umeanzishwa na kampuni ya kizawa ya Data Vision International iliyoko jijini Dar es Salaam, inayojishughulisha na Teknlolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Tafiti na Mafunzo, ambapo wanatekeleza mradi huo kwa kushirikiana na Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA). Mlezi wa mradi huo ni Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda.

  • Mbunge alalamikia malipo kidogo ya Korosho

    Mbunge alalamikia malipo kidogo ya Korosho

    Mbunge wa Jimbo la Tandahimba kupitia tiketi ya CUF, Katani S Katani amelalamikia hatua ya serikali kulipa kiasi kidogo cha fedha kwenye vyama ushirika ambavyo viko kwenye jimbo lake linalokadiriwa kuwa zaidi ya vyama 128.

    Kwa mujibu wa Mbunge Katani, mpaka sasa hakuna mkulima ambaye anamiliki magunia zaidi ya 16 ambaye ameshalipwa kutokana na utaratibu wa serikali, kulipa wenye idadi ya magunia 15.

    “Kwa mfano mimi kwangu, kumefanyika uhakiki lakini fedha iliyolipwa haizidi bilioni 6, na hii fedha imelipwa kwa chama kimoja tu wakati kwangu mimi kuna vyama zaidi ya 126, kwahiyo serikali imejificha kwenye uhakiki lakini kumbe haina fedha za kutosha,” amesema Katani.

     

    Hivi karibuni Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema kuwa mpaka sasa zaidi ya wakulima 130,163 wamelipwa jumla ya shilingi bilioni 133 kwenye zao la korosho.

    Katika Mkoa wa Lindi tayari wakulima 41,564 wamekwishalipwa, ambapo ni kiasi cha Bilioni 42 huku katika mkoa wa Ruvuma wakulima 11,463 wamekwishalipwa kiasi cha Bilioni 10.

    Aidha, Hasunga alisema kuwa katika mkoa wa Pwani Milioni 101,091,960 zimekwishalipwa kwa wakulima 81 huku akisisitiza kuwa vyama vilivyohakikiwa ni 461 na vilivyolipwa ni 451, ambapo jumla ya Kilo 40,381,798 zimenunuliwa na serikali.

    Serikali iliamua kujikita kwenye ununuaji wa zao la korosho kufuatia kuibuka kwa sintofahamu baina ya wafanyabiashara na wakulima juu bei ya elekezi zao hilo hali ambayo ilipekea kusitishwa kwa minada miwili.

     

  • RC Wangabo atoa tahadhari ya magonjwa ya mlipuko kwa waathirika wa mvua kali Rukwa

    RC Wangabo atoa tahadhari ya magonjwa ya mlipuko kwa waathirika wa mvua kali Rukwa

    Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amezitahadharisha Kaya ambazo bado hazijaweza kurudi katika makazi yao kutokana na nyumba zao kuezuliwa na upepo na mvua kali na kuwafanya kuishi kwa mikusanyiko katika majengo ya serikali juu ya usafi wa mazingira ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko kutokana na uchache wa vyoo katika maeneo hayo.

    Amesema hayo baada ya kuwatembelea waathirika wa mvua na upepo mkali waliohifadhiwa katika kituo cha kilimo kilichopo katika kijiji cha Kipeta, Kata ya Kipeta Wilayani Sumbawanga na kuwapatia misaada ya bati bando moja, gunia la maharage kilo 100, turubai moja, unga wa mahindi tani moja mahindi kilo 200.

    Amesema kuwa ili kuhakikisha mlipuko huo hautokei ni vyema waathirika hao wakajibana kwa ndugu ambao nyumba zao hazikuathirka na kusisitiza kuwa kujisitiri katika majengo ya Serikali ni kwa dharura tu huku wakiendelea kutafuta ufumbuzi wa misaada kwa wadau mbalimbali wa ndani na nje ya mkoa ili kuweza kuzisaidia familia hizo kurudi kwenye makazi yao ya kudumu.

    “Tusingependa wandelee kukaa pale, kuna atahari nyingine ya magonjwa ya mlipuko kuwaweka watu zaidi ya 200 sehemu kama ile, miundombinu ya vyoo haitoshi, kwahiyo pale ni pa muda mfupi, jamani wale watu si wana ndugu? Hatuwezi kubanana banana huko, naiachia Halmashauri ndio maana nikasema Mkurugenzi ashuke huku ayaangalie yote haya,” Amesisitiza.

    Katika hatua nyingine amewatahadharisha wale waliopo katika kamati za maafa ngazi ya kata kuwa makini na misaada hiyo na kuacha fikra ya kuitumia misaada hiyo kwa maslahi yao binafsi na kusisitiza kuwa yeyote atakayejihusisha na tabia hiyo atawajibika kwake.

    Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dkt. Khalfan Haule alitoa taarifa fupi juu ya walichokifanya baada ya maafa kutokea na kusema kuwa maafa hayo yaliathiri vijiji vinne na kitongoji kimoja katika wilaya ya sumbawanga.

    “Katika Wilaya yetu maafa haya pia yalitokea kwenye vijiji kama vinne pale (kijiji cha) Muze, kule (Kijiji cha) Msia tumepata taarifa shule ya msingi ya Msia yote imeanguka lakini pia katika kijiji cha Mpwapwa na kule Tunko na kwenye kata hii kuna vijiji viwili na kitongoji cha Kituku,” Alisema

    Usiku wa tarehe 8 kuamkia tarehe 9.12.2018 Mvua iliyoambatana na upepo mkali iliweza kuharibu nyumba 336 na kujeruhi watu 49 na kusababisha kifo cha mtu mmoja katika kijiji cha Kipeta na Kilyamatundu vilivyopo kata ya kipeta, katika bonde la ziwa Rukwa, wilayani Sumbawanga.

     

     

  • Polisi wanawake wapongezwa jijini Arusha

    Polisi wanawake wapongezwa jijini Arusha

    Polisi wanawake mkoa wa Arusha kupitia Mtandao wao (TPF NET) wamepongezwa kutokana na utendaji bora wa kazi zao za kila siku hasa katika suala zima la kudumisha nidhamu na kufanya kazi kwa uaminifu.
     
    Pongezi hizo zimetolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Ramadhani Ng’anzi wakati wa kuhitimisha maazimisho ya Siku 16 za kupinga Ukatili yaliyoanza rasmi Novemba, 25 mwaka huu.
     
    Amesem kuwa askari wa kike wamekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wananchi lakini pia kudumisha nidhamu kwa kiwango cha hali ya juu katika utendaji wao wa kazi.
     
    “Natoa pongezi kwa viongozi wenu wa TPF NET kwa kuwasimamia vyema na kuwaweka kwenye mstari mnyoofu na wale ambao walikuwa na dalili za kwenda kinyume na kazi walirudishwa kwenye njia kuu,”Amesema Kamanda Ng’anzi.
     
    Aidha, amesema kuwa ubora wao wa utendaji kazi umekuwa kivutio kwa baadhi ya taasisi na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali mkoani hapo ambapo wamekuwa wakifanya kazi pamoja nao hasa katika Madawati ya Kijinsia na Watoto kupitia harakati za kupinga ukatili na unyanyasaji na kuahidi kujenga ofisi kubwa ya Dawati mkoa itakayotoa nafasi ya faragha kwa wateja.