Category: Sports

  • SIMBA YAANZISHA GAZETI LAKE

    SIMBA YAANZISHA GAZETI LAKE

    Uongozi wa klabu ya Simba umetangaza kuanzisha gazeti lake ambalo litatambulishwa kesho katika tamasha la Simba Day.

    Hatua hiyo imekuja mara baada ya uongozi huo kueleza kumekuwa na magazeti baadhi mtaani yamekuwa yakitumia jina la Simba na kujipatia faida ambayo ilipaswa kuwa inaenda klabuni.

    Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, amesema gazeti hilo litakuwa linaitwa SIMBA NGUVU MOJA, litakuwa linatoka mara kila wiki siku ya Jumamosi.

    Manara amesema gazeti hilo litakuwa linauzwa siku ya Jumamosi na gharama yake itakuwa kiasi cha shilingi za kitanzania 500 pekee.

    Utambulisho wa gazeti hilo utafanyika kesho ambapo Simba itakuwa inakipiga na Asante Kotoko kutoka Ghana ukiwa ni mchezo maalum wa kukitambulisha kikosi cha timu hiyo kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

  • SIMBA YAINGIA MKATABA WA MILIONI 250 NA MO ENERGY

    SIMBA YAINGIA MKATABA WA MILIONI 250 NA MO ENERGY

    Uongozi wa klabu ya Simba umetangaza kuingia mkataba wa mwaka na Kampuni ya Utengenezaji vinywaji ya A One Products kupitia kinywaji cha Mo Energy Drink.

    Mkataba huo utakuwa na thamani ya fedha za kitanzania, shilingi milioni 250.

    Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Mwasala Masoud, amesema fedha hizo zitahusika na Simba kwa ajili ya shughuli mbalimbali ndani ya klabu hiyo.

    Mwasala ameeleza kuwa kinywaji cha Mo Energy kitakuwa kinaiwakilisha kampuni ya A One kutokana na utengenezaji wa bidhaa zake ambazo inazalisha.

    Aidha, Mwasala ameeleza kuwa mkataba huo unaweza ukaongezwa tena baada ya kufikia ukingoni baada ya miezi 12 ijayo kumalizkika.

    Baada ya A One na Simba kusaini mkataba huo, Kaimu wa Rais wa klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again, amesema fedha hizo ambazo ni milioni 250 zitaenda katika mradi wa ujezi wa Uwanja Bunju.

    Ikumbukwe Simba walianzisha mradi wa ujenzi wa Uwanja huo lakini baadaye ukaja ukasimama kutokana na sakata la viongozi wa klabu akiwemo Rais Evans Aveva kushitakiwa mahakami.

  • KOCHA ALIYEIPA UBINGWA WA AFRIKA NIGERIA, ASAINI MIAKA MIWILI TAIFA STARS

    KOCHA ALIYEIPA UBINGWA WA AFRIKA NIGERIA, ASAINI MIAKA MIWILI TAIFA STARS

    Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia amemtangaza kocha Emmanuel Amunike kutoka Nigeria kuwa kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars”.

    Kocha huyo amefikia mwafaka na TFF ya kusaini kandarasi ya miaka miwili kuinoa Taifa Stars inayodhaminiwa na bia ya Serengeti.

    Amunike aliwahi kutamba na kikosi cha Nigeria akicheza kama winga wa kushoto na pia alifanikiwa kuifundisha timu ya taifa hilo mwaka 1993 mpaka 2001.

    Mchezaji huyo mstaafu alikiongoza kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria katika mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 1994 kilichowafunga Bulgaria mabao 3-0 katika hatua ya makundi na pia kupoteza dhidi ya Italy kwa mabao 2-1 kwenye 16 bora.

    Aidha Amunike anakumbukwa kwa kuisaidia Nigeria kutwaa taji la Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1994 huko Tunisia na baada ya mashindano hayo aliweza kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa Afrika.

  • ALIKIBA AANZA KAZI COASTAL UNION

    ALIKIBA AANZA KAZI COASTAL UNION

    Mshambuliaji mpya wa klabu ya Costal Union ya Tanga, Ali Kiba, ameanza kujinoa na wachezaji wa kikosi hicho huko Tanga tayari kwa msimu mpya wa ligi utakaoanza Agosti 22 2018.

    Kiba ambaye pia ni Msanii wa Kimataifa kupitia Muziki wa kizazi kipya, ameanza kambi hiyo baada ya kujiunga na Coastal akisaini mkataba wa mwaka mmoja.
    Nyota huyo amekuwa gumzo kubwa ndani ya jiji la Tanga na kwa mashabiki na wanachama wa Costal kutokana na usajili wa Kiba ambao haukutarajiwa na wengi.
    Ikumbukwe Kiba amekuwa na umaarufu mkubwa zaidi katika tasnia ya muziki tofauti na mpira, japo ana kipaji kikubwa cha kusakata kambumbu.
    Caostal wameanza kujifua tayari kwa maandalizi ya msimu mpya ambao utakuwa na idadi ya timu 20 kutoka 16 ilivyokuwa kwa 2017/18.
  • Cameroon imethibitisha kufanya mazungumzo na meneja wa zamani wa England -Eriksson

    Cameroon imethibitisha kufanya mazungumzo na meneja wa zamani wa England -Eriksson

    Cameroon imethibitisha kufanya mazungumzo na kocha wa zamani wa England Sven-Goran Eriksson kuchukua usukani wa kuifunza timu ya taifa hilo Indomitable Lions.

    Eriksson mwenye umri wa miaka , 70, raia wa Sweden alikuwa na mazungumzo mazuri na maafisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Cameroon (Fecafoot) mjini Yaoundé wiki iliyopita waliokuwa wakitaka kuziba pengo lililoachwa baada ya kuondoka kwa Hugo Broos.

    “Baada ya kukaa saa 72, Sven-Goran Eriksson aliondoka Yaoundé Jumamosi tarehe 28 July 2018,” Fecafool lilieleza kwenye ukurasa wake wa Twitter.

    ” Meneja huyo raia wa Sweden alikuwa amekaribishwa na Cameroon kwa mazungumzo juu ya kuajiriwa kwa kocha mkuu wa timu kuu ya taifa – the Indomitable Lions.

    ” Baada ya kumpa mtihani wa kazi Sven-Goran Eriksson na kuzingatia mapendekezo mengine yaliyopo, Fecafoot litafichua chaguo lake la kocha wa kudumu wa timu yetu ya taifa lilieleza shirikisho hilo la mpira wa miguu la Cameroon.

    Haki miliki ya picha Getty Images
    Image caption Aliyekuwa kocha wa timu ya Indomitable Lions Hugo Broos, aliondoka mwezi Februari mwaka huu baada ya mkataba wake kuisha

    Eriksson, ambae alikuwa meneja wa England kati ya mwaka 2001 na 2006, na kuifikisha timu hiyo hadi michuano ya robo fainali ya Kombe la Dunia mara mbili, alikuwa mmoja wa watu 77 ambao maombi yao ya kazi yalifichuliwa mwezi Aprili.

    BBC inafahamu kuwa Eriksson, ambaye awali alikuwa mkufunzi wa klabu za England Manchester City na Leicester City, atalipwa CFA 50 million (€71,000) kila mwezi na atafanya kazi na kocha msaidizi raia wa Cameroon na ataishi nchini humo.

    Vyombo vya habari nchini Cameroon pia vimewahusisha Waholanzi Clarence Seedorf na Patrick Kluivert na kazi hiyo. 

    Awali Eriksson alizifunza timu za Mexico na akafanikiwa kuipeleka led Ivory Coast katika Kombe la Dunia la 2010 nchini Afrika Kusini kabla ya kuwa meneja wa timu ya Uchina ya Guangzhou Evergrande mnamo 2013.

    Akiwa Uchina pia alipata fursa ya kuzifunza timu za Shanghai SIPG na Shenzhen, kabla ya kuondoka hukomwezi June 2017.

    Pia amekuwa akihusishwa na Iraq kama kocha.

    Kazi ya kocha wa timu ya Cameroon ilikuwa wazi mwezi Februari wakati aliekuwa kocha wa timu Indomitable Lions Hugo Broos, alipoondoka baada ya mkataba wake kuisha.

  • UONGOZI WA SIMBA UMEFUGUKA KUHUSU UCHAGUZI WAKE

    UONGOZI WA SIMBA UMEFUGUKA KUHUSU UCHAGUZI WAKE

    Uongozi wa klabu ya Simba umefunguka na kusema kuwa haushinikizwi kufanya uchaguzi wake na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zikiwa zimesalia siku kadhaa kuelekea mchakato wake kuanza.

    Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, amesema wao kama Simba walikuwa wanasubiria katiba yao mpya isajiliwa na serikali hivyo mchakato wa uchaguzi ulisimama kwa muda kuisubiria.

    Manara ameeleza kuwa wao kama Simba hawawezi kushinikiwa kufanya uchaguzi huo na TFF na badala yake watakutana Agosti 31 kuanza mchakato kamili wa kuunda Kamati ya Uchaguzi.

    Hivi karibuni, Rais wa TFF, Wallace Karia aliwapa Simba siku 75 kwa ajili ya kuanza mchakato huo baada ya kupokea barua inayoeleza kuwa klabu hiyo inapaswa kufanya uchaguzi mwingine baada ya viongozi waliopo madarakani kumaliza muda wao.

    Simba imekuwa ikiongozwa na Kaimu Rais, Salim Abdallah ‘Try Again’ ambaye amekaimu nafasi hiyo kutoka kwa Evans Aveva mbaye yuko mahakamani kutokana na makosa ya matumizi mabaya ya fedha.

  • UONGOZI YANGA WAWEKA HADHARANI VIINGILIO VYA MCHEZO DHIDI YA GOR MAHIA

    UONGOZI YANGA WAWEKA HADHARANI VIINGILIO VYA MCHEZO DHIDI YA GOR MAHIA

    Uongozi wa klabu Yanga umetangaza viingilio vya mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya Gor Mahia FC utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Julai 29 2018.

    Kueleka mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika, Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten, amesema kuwa kiingilio cha chini kabisa kitakuwa ni shilingi 3000 pekee ambacho ni kwa jukwaa la mzunguko.

    Katika jukwaa la VIP A kiingilio kitakuwa ni Tshs 10,000 huku VIP B na C kikiwa ni 7,000 pekee.

    Yanga inaenda kucheza mchezo huo ikiwa inashika mkia kunako kundi D ikiwa na alama moja pekee iliyoipata baada ya suluhu tasa dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa Dar.

    Yanga inakutana na Gor Mahia ambayo iliwapa kichapo cha maana kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza jijini Nairobi kwenye Uwanja wa Moi Kasarani wa jumla ya mabao 4-0.

  • BAADA YA MKWASA NA SANGA KUACHIA NGAZI, UONGOZI YANGA WATOA TAMKO JUU YA WATAKAORITHI NAFASI ZAO

    BAADA YA MKWASA NA SANGA KUACHIA NGAZI, UONGOZI YANGA WATOA TAMKO JUU YA WATAKAORITHI NAFASI ZAO

    Baada ya viongozi wa Yanga kuzidi kuachia ngazi akiwemo Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo jana, Clement Sanga kutangaza kujiuzulu wadhifa wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika, ameitisha kikao na wahabari leo.

    Nyika ameitisha kikao hicho kuzungumzia mustakabali mzima wa Yanga juu ya kujaza nafasi za viongozi wake walioachia ngazi namna utakavyokuwa.

    Ikumbukwe Yanga imekuwa haina Mwenyekiti kwa muda mrefu tangu kujiuzulu kwa Yusuf Manji akidai anahitaji kupumzika kutokana na kukabiliwa na majukumu mengi binafsi.

    Baada ya Manji, wajumbe kadhaa wa Kamati ya Utendaji akiwemo Salum Mkemi na Khalfan Hamis nao wameachia ngazi kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri baina yao na uongozi wa juu wa klabu.

    Kutokana na kujizulu kwao, uongozi wa Yanga kupitia kwa Nyika utaeleza kiunagaubaga leo hatma ya nafasi zao ikiwemo suala la uchaguzi wa kujaza nafasi ya Mwenyikiti pamoja na ile ya Katibu Mkuu.

  • MAKAMU MWENYEKITI WA YANGA CLEMENT SANGA AJIUZULU NAFASI YAKE

    MAKAMU MWENYEKITI WA YANGA CLEMENT SANGA AJIUZULU NAFASI YAKE

    Makamu Mwenyekiti wa Yanga Clement  Sanga amejiuzulu nafasi yake katika klabu hiyo kuanzia leo hii.

    Amesisitiza kuendelea kuwa mwanachama na kuisaidia klabu ya Yanga katika kila hali.

    Kwa upande wa hela zinazozungumziwa za Milioni 240 za kutoka CAF, Sanga amesema Yanga imekuwa na changamoto nyingi sana katika upande wa fedha na wamekuwa wana madeni makubwa ambayo wanakatwa katika mapato ya mlangoni ikiwemo Deni la Ardhi na madeni mengine pia.

  • Mesut Ozil ajiengua timu ya taifa ya Ujerumani

    Mesut Ozil ajiengua timu ya taifa ya Ujerumani

    Kiungo mshambuliaji wa Arsenal Mesut Ozil amesema hataki tena kuiwakilisha Ujerumani katika michuano ya kimataifa.

    Katika taarifa ndefu iliyotolewa na Ozil mwenye miaka 29, imesema kufanyiwa vitendo visivyo vya kiungwana na chama cha soka cha Ujerumani DFB, kumemfanya asitake tena kuivaa jezi yao.

    Ameongeza kuwa amekuwa akilaumiwa sana kwa Ujerumani kufanya vibaya katika michuano ya kombe la dunia.

    Mwezi May, Ozil alilalamikiwa vikali na mashabiki pamoja na chama cha soka cha Ujerumani kwa kupiga picha na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alipokua mjini London.

    Ozil alihudhuria katika hafla hiyo akiwa na kiungo mwenzake anayechezea Manchester City Ilkay Gundogan.

    Ozil na Gundogan wote wana asili na uraia wa Uturuki.

    Ozil amesema yeye na Gundogan walizungumzia masuala ya soka walipokutana na Rais Erdogan.

    Picha hizo zilitolewa na chama tawala nchini Uturuki AK kuelekea kampeni za Urais ambazo Erdogan alishinda.

    Wanasiasa wengi nchini Ujerumani walihoji kitendo hicho wakati ambao taifa hilo lenye nguvu zaidi ya kiuchumi barani Ulaya likiilaumu Uturuki kwa kukiuka haki za binaadam na kutofuata misingi ya demokrasia.

    Ozil amesema ”lisingekua jambo la busara kushindwa kupiga picha na Rais wa nchi ya asili yangu, hata babu zangu wa kale na kale wasingependezwa”.

    Ameongeza kuwa yeye na familia yake wamekua wakipokea simu za vitisho, barua pepe za matusi na hata jumbe za kukatisha tamaa katika mitandao ya kijamii.

    Akiwa na kikosi cha Ujerumani amecheza mara 92, akifunga magoli 23 na kuchangia mengine 33, huku akishinda kombe la dunia mwaka 2014.

  • SIMBA YAMTAMBULISHA KOCHA MPYA KUTOKA UBELGIJI

    SIMBA YAMTAMBULISHA KOCHA MPYA KUTOKA UBELGIJI

    Uongozi wa klabu ya Simba umemtangaza rasmi kocha wao mpya, Mbelgiji Patrick Aussems, tayari kuanza kazi ya kuiandaa timu kuelekea mashindano ya Ligi Kuu Bara.

    Simba wameingia makubaliano ya mkataba wa mwaka mmoja na Aussems akiwa anachukua mikoba ya Mfaransa, Pierre Lechantre ambaye alimaliza muda wake.

    Hatua hiyo imekuja mara baada ya mabosi wa Simba kugoma kumuongezea mkataba Lechantre ambaye alipewa timu kwa muda wa miezi sita pekee na baada ya kumalizika wakaacha naye.

    Aussems amesaini mkataba huo mbele ya Makamu Rais wa klabu hiyo, Salim Abdallah maarufu kama Try Again, sambamba na Kaimu Makamu wa Urais, Idd Kajuna pamoja na Waandishi wa Habari.

    Kocha huyo amewahi kuzinoa timu kadhaa za Afrika ikiwemo AC Leopards ya Congo, KSA Cameroon ya Cameroon, ES Troyes AC ya Ufaransa na zingine zilizopo  je ya Afrika.

    Simba wamefikia hatua ya kumpa mkataba wa mwaka mmoja baada ya kuridhishwa na CV zake hivyo kuona anastahili kukinoa kikosi hicho ambacho kimeshiriki michuano ya SportPesa Super CUP na KAGAME bila ya Kocha Mkuu.

    Wakati Aussems akimwaga wino, kikosi cha Simba kinatarajiwa kusafiri kuelekea nchini Uturuki kwa ajili ya kambi ya wiki mbili kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa ligi unaotaraji kuanza Agosti 22.