Category: Global News

  • Bosi ashtakiwa kwa ‘Kujamba’ ofisini

    Bosi ashtakiwa kwa ‘Kujamba’ ofisini

    Mfanyakazi mmoja nchini Australia amefungua mashtaka kwenye mahakama ya rufaa ya nchi hiyo akidai bosi wake alikuwa akimbughudhi ofisini kwa kujamba sana.

    Awali, mahakama moja ya chini ilifikia uamuzi kuwa hakukuwa na bughudha yeyote katika suala hilo.

    Hata hivyo, David Hingst anadai kuwa bosi wake wa zamani Greg Short alikuwa “akinyanyuka na kumjambia” karibu mara sita kwa siku.

    Mwaka jana mashtaka dhidi ya kampuni yake ya zamani na kudai dola milioni 1.28 yalitupiliwa mbali na Mahakama Kuu ya Victoria iliyohukumu kuwa hakukuwa na bughudha.

    Bwana Hingst mwenye miaka 56, amedai kuwa mashuzi hayo yamemsababishia “msongo mkubwa”.

    Aalikuwa akijamba na kwenda zake

    Hingst, ambaye alikuwa afisa utawala katika mji wa Melbourne, ameishtaki kampuni ya Construction Engineering mwaka 2017 lakini kesi hiyo ilitupwa Aprili 2018.

    Amekata rufaa dhidi ya uamuzi huo na Jumatatu, Novemba 25 alisikilizwa na Mahakama ya Rufaa.

    “Nilikuwa nikikaa kwenye chumba kidogo ambacho hakina madirisha, alikuwa akiingia na kujamba nyuma yangu na kisha kwenda zake. Alikuwa akifanya hivyo mara tano mpaka sita kwa siku,” Hingst ameliambia Shirika la Habari la nchi hiyo, Australian Associated Press (APP).

    Katika kesi ya awali mwaka jana, bwana Short alidai kuwa hakumbuki kujamba akiwa karibu na Hingst lakini “yawezekana ilitokea mara moja ama mbili hivi, yawezekana.”

    Hata hivyo, alikanusha kuwa alifanya vitendo hivyo “kwa madhumuni ya kumkera na kumbughudhi” Hingst.

    Hingst alikuwa akimuita Short “Bwana Mnukaji” na alikuwa akipuliza uturi kila aliposogea karibu yake, korti iliambiwa.

    Kwa mujibu wa mitandao ya Australia, Hingst amedai kuwa, tabia ya Short ilikuwa ni sehemu ya mpango wa kumng’oa kazini na muda aliofanya kazi na Construction Engineering kulimsababishia majeraha ya kiakili. Pia amedai kuwa Short alikuwa akimkejeli kutokana na ufanisi wake na kumpachika jina la “bwege”.

    Hingst amesema kesi yake ya kwanza haikuamuliwa kwa usawa, kudai jaji alimbagua.

    Mahakama ya Rufaa itatoa hukumu yake Ijumaa, Machi 29.

     

  • Trump ‘hakusuka njama na Urusi’ kushinda uchaguzi

    Trump ‘hakusuka njama na Urusi’ kushinda uchaguzi

    Kampeni iliyoendeswa na rais wa Marekani Donald Trump ‘haikushirikiana na Urusi wakati wa uchaguzi wa 2016, kwa mujibu wa muhtasari wa ripoti ya ya mwanasheria mahususi Robert Mueller iliyowasilishwa kwenye bunge la Congress ,Jumapili.

    Muhtasari wa ripoti haukuelezea ikiwa Bwana Trump alizuia utekelezwaji wa sheria – lakini pia haikumuhusisha rais na madai hayo.

    Ripoti hiyo iliwekwa kwa muhtasari kwa ajili ya Congresi na Mwanasheria Mkuu, William Barr.

    Trump alituma ujumbe wa twitter kujibu muhtasari wa ripoti yake akisema: ” hakuna ushirikiano, hakuna kuzuia sheria.”

    Rais Trump, ambaye mara kwa mara aliuelezea uchunguzi kama ”uwindaji wa kichawi”, alisema Jumapili kwamba “ni aibu kwamba nchi ililazimika kupitia hili”, akiuelezea uchunguzi dhidi yake kuwa “kuangushwa kwa jambo lililo kinyume cha sheria “.

    Ripoti hiyo inakamilisha uchunguzi wa miaka miwili wa Bwana Mueller, ambapo wakati wa uchunguzi huu washirika wa karibu wa rais walishitakiwa, na wakati mwingine hata kufungwa.

    “Japo ripoti hii haionyeshi kuwa rais alifanya uhalifu, haimuweki huru ,”Bwana Mueller aliandika katika ripoti yake.

    Kile kilichomo kwatika muhtasari wa ripoti

    Barua ya muhtasari wa ripoti hiyo ya Bwana Barr inaainisha matokeo ya uchunguzi unaohusiana na juhudi za Urusi za kushawishi matokeo ya uchaguzi wa 2016.

    Bwana Barr alihitimisha ripoti yake kwa kusema: “Mchunguzi maalum hakumpata Trump, mtu yeyote wa Marekani au afisa wa kampeni ya Trump na hatia ya kushirikiana au kwa kufahamu kuratibu ushirikiano wowote na Urusi .”

    Sehemu ya pili ya barua hiyo ilizungumzia suala la kuzuwia utendaji wa sheria . Muhtasari wa Bwana Barr unasema ripoti wa mchunguzi mkuu “Hatimae haimuweki katika nafasi ya kushtakiwa “.

    Uchunguzi wa Robert Mueller umechukua takribani miaka miwili

    “Kwa hiyo baraza la uchunguzi halikutoa hitimisho – kwa njia moja au nyingine- juu ya ikiwa mienendo iliyochunguzwa ilikuwa ni ya kuzuwia utendaji wa kisheria ,”ilielezea barua hiyo.

    Bwana Barr anasema kuwa ushahidi haukutosha “kubaini kwamba rais alitenda kosa la kuzuwia utendaji wa washeria “.

    Bwana Barr alikamilisha barua yake kwa Congresi kwa kusema kuwa atafichua mengi zaidi katika ripoti kamili , lakini akasema baadhi ya yanazuwiwa kutangazwa.

    “Kutokana na masharti hayo , mpango wa mchakato wa ripoti hiyo utategemea kwa upande mmoja juu ya namna wizara ya mambo ya nje itakavyoweza haraka kubaini yaliyopendekezwa na jopo kuu la mahakama ambayo kw amujibu wa sheria hayapaswi kutangazwa kwa umma ,” aliandika.

    ” Nimeomba msaada wa mchunguzi mkuu katika kutambua taarifa zote zilizomo kwenye ripoti haraka iwezekanavyo .”

    Walichosema wanasiasa wa marekani kuhusu Muhutasari wa ripoti

    Mjumbe wa Congresi Jerry Nadler, ambaye ni mwenyekiti wa tume ya sheria wa Democratic katika bunge la wawailishi, alisisitiza kuwa mwanasheria mkuu hakusema moja kw amoja kwamba Trump alizuwia utendaji wa sheria .

    “Barr anasema kwamba rais huenda alizuwia uutekelezwaji wa sheria, lakini kupatikana na hatia hiyo , ‘serikali itahitaji kutoa ushahidi wa kutosha kwamba mtu alifanya hivyo kwa kukusudia, au kuhusika katika mwenendo wa kuzuwia utekelezwaji wa sheria’.”

    Seneta wa Democratic Richard Blumenthal, ambaye ni mjumbe wa kamati ya Seneti ya sheria, alisema kwamba japo ushahidi ulikosa wa “kushtakiwa kwa uhalifu wa kushirikiana “, bado maswali yanabakia juu ya ikiwa Bwana Trump alihusika.

    Katika taarifa ya pamoja , Spika wa bunge kutoka chama cha Democratic Nancy Pelosi na kiongozi wa wabunge wa Democratic katika seneti Chuck Schumer walisema barua ya Bwana Barr ” inaibua maswali mengi kama inavyoyajibu” na wakatoa wito wa ripoti kamili kutolewa.

    “kwa rais kusema yuko huru kabisa inakwenda kinyume kabisa na maneno ya Bwana Mueller na maneno yake hayapaswa kuchukuliwa kuwa ni ya kuaminika ,” ilisema taarifa yao.

    Afisa habari wa ikulu ya White House Sarah Sanders alielezea matokeo ya uchunguzi huo kuwa “ya kumuweka huru kwa jumla rais”.

    Wakili wa Trump, Rudy Giuliani, alisema ripoti “ilikuwa bora kuliko nilivyotarajia “. Nae Seneta wa Republican Mitt Romney aliafiki “habari njema “, akituma ujumbe wake wa twitter kwamba ”Ni wakati wa taifa kusonga mbele “.

  • Basi la shule latekwa na kuteketezwa kwa moto

    Basi la shule latekwa na kuteketezwa kwa moto

    Basi lililokuwa limebeba watoto wa shule wapatao 51 lilitekwa na dereva wake na kisha kutiwa moto karibu na Milan nchini Italia.

    Watoto hao wa shule, baadhi yao walifungwa kamba, waliokolewa baada ya kuvunjwa vioo vywa basi hilo upande wa nyuma na hakuna hata mmoja aliyejeruhiwa vibaya.Watu kumi na wanne waliathiriwa na moshi uliotokana na kuteketea kwa basi hilo.

    Dereva wa basi hilo alikuwa na umri wa miaka arobaini na saba mwenye uraia wa nchini Italia ingawa ana asili ya kutoka nchini Senegal, inaarifiwa kwamba ametiwa nguvuni.

    Dereva huyo alisikika akitamba, akiwaambia waliokuwemo katika basi hilo kwamba hakuna hata mtu mmoja atakaye nusurika.Ulikuwa ni muujiza, vinginevyo yangekuwa ni mauaji ya halaiki, alinukuliwa akisema hayo mwendesha mashtaa mkuu wa mjini Milan, Francesco Greco.

    Mwalimu mmoja wapo alikuwa ndani ya basi wakati tukio hilo likitekelezwa, alimuelezea mtuhumiwa huyo kuwa alikuwa na silika ya hasira mara kwa mara na kubwa hasa ni juu ya sera za wahamiaji nchini Italia .Taarifa zingine zinaarifu kuwa dereva huyo alisikika akibwata sitisheni mauaji katika bahari ya Mediterranean”.

    ukio hilo lilikuwaje?

    Makundi mawili ya wanafunzi waliokuwa wakisindikizwa na waalimu wao , walikuwa wameyatoka mazingira ya shuleni iitwayo Vailati di Crema , wakielekea kwenye mazoezi lakini baadaye gari ikachukua muelekeo tofauti na safari yao na kuelekezwa kwenye barabara kuu ya mkoa na kufuata njia inayoelekea katika uwanja wa ndege wa Milan Linate, ripoti za mashuhuda zinaarifu .

    Suala hilo liling’amuliwa dakika arobaini baadaye , wakati dereva alipowaelekezea abiria wake kisu huku akizungumza, mvulana mmoja aliwapigia wazazi wake kwa siri, ambao nao waliwafahamisha polisi juu ya tukio hilo.

    Ilichukua muda kidogo kabla polisi hawajalifikia basi lililotekwa na kujaribu kulifanya lisimame,na mara basi hilo lilianza kubamiza gari la polisi kabla ya kupunguza mwendo na kusimama kabisa.

    Taarifa kutoka nchini Italia zinaarifu kuwa mafuta ya petroli yalinyunyizwa kulizunguuka basi hilo la shule , lakini polisi walitumia mbinu ya kuvunja mairisha ya nyuma ya basi hilo na hivyo kuwaruhusu abiria kushuka kwa haraka kabla basi hilo halijalipuka moto.

    Waendesha mashitaka wa Milan waliarifu kuwa wanafanya uchunguzi wa kina kuchunguza ikiwa kulikuwa na nia zozote mbaya ikiwa ni pamoja na ugaidi.Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia, Matteo Salvini, alizungumza kwa hasira kwamba dereva huyo alikuwa na rekodi ya uhalifu.

    Msimamo mkali wa Italia kwa wahamiaji

    Tangu alipoingia madarakani mwezi wa sita mwaka jana, uongozi wa Italia wa chama cha mrengo kulia na harakati za umoja wa Wanawake wenye hadhi ya nyota tano wameanzisha harakati zenye msimamo mkali wa kupambana na uhamiaji nchini humo.

    Harakati hizo zimepamba moto na kuwa za mstari wa mbele dhidi ya wahamiaji wanaovuka Bahari ya Mediteranean kwenda Ulaya, nayo Italia imejaribu kufunga bandari zake kwa kutumia boti.

    Mapema wiki hii, watu karibu hamsini waliokolewa na meli ya wasamaria wema ambapo wahamiaji walikuwa wakisafiri kwenye boti iliyotengenezwa kwa plastiki ikielea katika pwani ya Libya na kuchukuliwa hadi katika pwani ya Sicilia ya Lampedusa.

    Mamlaka nchini Italia iliamuru kukamatwa kwa meli hiyo na kuanzisha uchunguzi juu ya madai ya kuhamia uhamiaji wa siri

    cc;BBCswahili
  • Janga kubwa’ Msumbiji na Zimbabwe kuathiri Afrika mashariki

    Janga kubwa’ Msumbiji na Zimbabwe kuathiri Afrika mashariki

    Kimbunga Idai kimesababisha “janga kubwa” katika mataifa ya kusini mwa Afrika na kuathiri laki kadhaa za watu kama sio mamilioni, Umoja wa mataifa unasema.

    Eneo hilo limekabiliwa na mafuriko katika sehemu nyingi na uharibifu katika nchi za Musmbiji Zimbabwe na Malawi.

    Huku kukiwa na ripoti kwamba takriban angalau watu 400,000 wameachwa bila ya makaazi Msumbiji ya kati, shirika la kimataifa la msalaba mwekundu linaonya kwamba huenda ikachukua siku kadhaa kabla ya athari kamili ya “janga la kibinaadamu” kujulikana dhahiri.

    Maafisa kutoka kitengo cha utabiri wa hali ya hewa nchini Kenya wanaonya kwamba athari ya kimbunga hicho itashuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya Afrika mashariki.

    Benard Chanzu, naibu mkurugenzi katika idara ya utabiri wa hali ya hewa Kenya anasema kimbunga hicho huenda kikaathiri msimu wa mvua kwenye eneo hili.

    ‘Mara nyingi upepo unapovuma, kila mahali huwa unaeleka katika eneo ambapo kunashuhudiwa kimbunga kile, pahali kulipo na hewa nyepesi, upepo unapovuma unakwenda ukielekea kwenye hicho kimbunga.

    ‘Wakati kimbunga kimeelekea kikaja mpaka kikaktua Msumbiji, kilitunyanganya upepo wote kutoka sehemu ya Afrika mashariki, kwa hivyo inanyang’anya uwezekano wa kuwepo mvua katika sehemu hii yetu’ameeleza bwana Chanzu.

    Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi ameliita “janga la kibinaadamu lenye kiwango kikubwa”.

    Amesema Idadi ya watu waliofariki kutokana na kimbunga Idai nchini Msumbiji sasa huenda ikawa ya juu na kufikia watu 1000.

    Kimbunga hicho kilishuka katika mji wa bandari wa Beira siku ya Alhamisi kikiwa na upepo wenye kasi ya hadi kilomita 177 kwa saa, lakini mashirika ya misaada yalifika katika eneo hilo siku ya Jumapili.

    Serikali ya Msumbiji imesema watu 84 wamefariki na wengine takriban 100,000 wanahitaji kuokolewa kwa dharura karibu na mji wa Beira.

    Picha ya kutoka juu ya jimbo hilo imeonyesha kiasi cha 50km ya ardhi imezikwa chini ya maji baada ya mto Buzi kuvunja kingo zake , shirika la misaada la Save The Children limesema.

    Juhudi za uokoaji zinaendeleaje?

    Nchini Msumbiji, mashirika kadhaa ya misaada yanasaidia jitihada za serikali katika kuwatafuta na kuwaokoa watu na katika kutoa misaada ya chakula pia, mtandao wa ReliefWeb unaripoti.

    Shirika la Telecoms Sans Frontiers limetuma maafisa mjini Beira kusaida kuidhinisha mawasiliano – ambayo yamekatizwa kutokana na mafuriko hayo – katika kusaidia kuendeleza operesheni za usaidizi.

  • Watu 1000 wahofiwa kufariki kutokana na kimbuga Msumbiji

    Watu 1000 wahofiwa kufariki kutokana na kimbuga Msumbiji

    Idadi ya watu waliofariki kutokana na kimbunga Idai nchini Msumbiji sasa huenda ikawa ya juu na kufikia watu 1000 rais Filipe Nyusi amesema.

    Bwana Nyusi alisafiri kwa ndege katika maeneo yalioathirika zaidi siku ya Jumatatu. Alielezea kuona miili ikielea juu ya mito.

    Tayari kuna hatari ya maisha ya zaidi ya watoto 100,000 na watu wazima kufuatia kikmbunga hicho huku mito katika maeneo yaliothirika zaidi ikivunja kingo zake , kulingana na shirika la Save the Children.

    Mafuriko yaliofanyika mapema mwezi huu yamezidishwa na kimbunga Idai ambacho kilikumba eneo la kaskazini mwa Msumbiji mnamo tarehe 15 mwezi Machi 2019 na kusababisha unahiribifu mkubwa wa nyumba , shule, hospitali na miundo mbinu.

    Kulingana na serikali ya Msumbiji takriban watu 600,000 wameathiriwa , huku maisha ya zaidi ya watu 1000 yakidaiwa kupotea huku yale ya watu 100,000 yakihitaji msaada wa dharura mjini Beira.

    Kiwango cha janga hilo kinazidi kuongezeka kila dakika na shirika la Save the Children lina wasiwasi mkubwa kuhusu watoto na familia walio katika hatari huku viwango vya mafuriko vikizidi kuongezeka anasema Machel Pouw mkuu wa operesheni ya shirika hilo nchini Msumbiji.

    Save the Children ni mwanachama wa COSACA wakishirikiana na shirika la OXFAM pamoja na lile la CARE na linafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na serikali pamoja na taasisi za usimamizi wa majanga ili kuwasaidia watoto walioathirika

    Kimbunga hicho kilishuka katika mji wa bandari wa Beira siku ya Alhamisi kikiwa na upepo wenye kasi ya hadi kilomita 177 kwa saa , lakini mashirika ya misaada yalifika katika eneo hilo siku ya Jumapili.

    Mfanyikazi mmoja wa Umoja wa mataifa aliambia BBC kwamba kila nyumba mjini Beira- ambapo ni mji wenye makaazi ya watu nusu milioni iliharibiwa.

    Gerald Bourke, kutoka kwa shirika la chakula duniani , alisema: Hakuna nyumba ambayo haikuathiriwa . hakuna Umeme, hakuna mawasiliano.

    Barabara zimejaa magogo ya nyaya za umeme. Paa za nyumba zimeanguka pamoja na nyuta zake. raia wengi wa mji huo wamepoteza makaazi yao.

    Idadi rasmi ya watu waliofariki nchini Msumbiji inadaiwa kuwa watu 84 kufuatia mafuriko na upepo mkali.

    Kimbunga hicho kimewaua takriban watu 180 katika eneo lote la Afrika Kusini.

    Shirika la msalaba mwekundu limeelezea uharibifu huo kuwa mbaya zaidi na wa kutisha. Watu wamelazimika kuokolewa wakiwa juu ya miti , Jamie LeSeur mkuu wa IFRC aliambia BBC.

    Nchini Zimbabwe takriban watu 98 wamefariki huku 217 wakiwa hawajulikani waliko mashariki na kusini serikali imesema.

    Idadi ya watu waliofariki inashirikisha wanafunzi wawili wa shule ya St Charles Lwanga katika wilaya ya Chimanimani, ambao walifariki baaada ya bweni lao kuathiriwa kutokana na mawe yaliosombwa na maji hayo katika mlima.

    Malawi pia nayo iliathiriwa vibaya . Mafuriko nchini humo yaliosababishwa na mvua kabla ya kimbunga hicho kuwasili yalisababisha mauaji ya vifo 122 kulingana na mitandao ya mashirika ya misaada.

    Serikali ya Uingereza inasema kuwa itatoa msaada wa kibinaadamu wenye thamani ya £6m kwa Msumbiji na Malawi.

    Pia imesema kuwa itatuma mahema pamoja na maelefu ya mahema nchini Msumbiji.

    Uharibifu wa Beira ni mkubwa kiasi gani?

    Wengi wa wale wanaojulikana kufariki waliuawa karibu na mji wa Beira , ambao ndio mji mku wa nne kwa ukubwa ukiwa na idadi ya watu isiopungua nusu milioni kulingana na mamlaka.

    Zaidi ya watu 1500 walijeruhiwa na miti pamoja na vifusi vilivyoanguka ikiwemo paa , kulingana na maafisa katika mji mkuu wa Maputo waliozunguzma na BBC.

    ”Karibu kila kitu kimeathiriwa na janga hili” , Alberto Mondlane , gavana wa mkoa wa Sofala unaoshirikisha Beira alisema siku ya Jumapili. Tuna watu wanaotaabika kwa sasa , wengine juu ya miti na wanahitaji sana msaada.

    Barabara inayounganisha Beira na maeneo mengine ya taifa hilo iliharibiwa vibaya, lakini usafiri wa ndege hadi maeneo yalioathirika pakubwa umeanzishwa.

    Rais Filipe Nyusi alikata ziara yake ya Swaziland ili kutembelea maeneo yalioathirika.

    Manusura katika hospitali moja katika wilaya ya Chimanimani walizungumza kuhusu vile mafuriko hayo yalivyoharibu nyumba zao na kuwasomba wapendwa wao.

    ”Hadi sasa sijui ni wapi mwangu yupo” , Jane Chitsuro aliambia shirika la habari la AFP . ”hakuna samani , hakuna nguo ni vifusi na mawe pekee’.

    Nyumba ya Praise Chipore pia nayo iliharibiwa .

    ”Mwanangu alikuwa nami kitandani akasombwa na mafuriko huku mafuriko makubwa yakinisomba mie pia”, alisema.

     

  • Watu 10 wamefariki kutokana na uhaba wa chakula

    Watu 10 wamefariki kutokana na uhaba wa chakula

    Zaidi ya watu 10 wameripotiwa kufariki kutokana na ukame katika kaunti ya Turkana nchini Kenya,

    Wengine zaidi ya 800,000 wakiendelea kuumia kwa makali ya njaa na kiu kwa mujibu wa wizara ya kudhibiti majanga na utumishi wa umma ya kaunti ya Turkana.

    Mariam Loolio ni ajuza mwenye umri was miaka 85. Kwa siku tano anasema hajala chochote

    Serikali ya kaunti hiyo wiki iliyopita ilitoa hakikisho kwamba imeidhinisha mpango wa usaidizi kuwakinga wakaazi kutokana na madhara ya ukame uliopo.

    Katika kijiji cha Kakwanyang’ Turkana ya Kati, mizoga ya wanyama iliyotapakaa, na miti yaliyokauka inaashiria hali inayoshuhudiwa katika eneo hilo kutokana na na ukame.

    Wakaazi wengi katika kijiji hiki hawajatia chakula chochote mdomoni kwa muda wa karibu siku 5 zilizopita.

    Kwa sasa wakaazi hawa wanalazimika kutuliza makali ya njaa kwa kula matunda ya mwituni yajulikanayo kama Mkoma.

    Moru Lomutan ni mzazi wa watoto sita na nilipofika nyumbani kwake nilimkuta akiwa analigonga gonga tunda la Mkoma ili kulifanya liwe laini kwake kutafuna.

    “Najaribu kuligonga hili tunda kwa mawe ili nile kwa sababu sina hata nguvu ya kuliuma mdomoni”

    Katika bwawa la maji, watu walikuwa wamejaa, kina mama na watoto.

    Miale ya jua sio kizuizi kwa wanakijiji hao kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu ili kuweza kujipatia maji.

    Karibu na bwawa hilo mizoga ya mbuzi na kondoo imetapakaa. Wakaazi wanadai kuwa mifugo hao walifariki baada ya kukosa chakula na maji.

    Anna Emaret amepoteza mifugo wake 20. Anasema amekuwa akigawana chakula na mifugo wake, lakini chakula kilipoisha, wakafa.

    “Kondoo wangu wote wamekufa, mbuzi pia wamekufa. Sasa sina mifugo, sina chakula, serikali isipotusaidia, tutakufa tu kama mifugo wetu”

    Mariam Loolio ni ajuza mwenye umri was miaka 85. Kwa siku tano hajala chochote .

    “Nimekaa hapa kungoja serikali ituletee chakula. Munavyoniona mimi ni mzee, tena kipofu. Hakuna jinsi ninavyoweza kutafuta chakula, hakuna kabisa. Kwa hivyo nasubiri tu serikali ije iniokoe ili nisife njaa. Sina namna”

    Nancy Alimlim alimzika kakake siku ya Jumamosi. Anaelezea kwa uchungu huku akibubujikwa na machozi.

    Maji yamekuaka katika visima na mabwawa ya maji

    Ukame umekuwa ukishuhudiwa kwa miaka mingi katika kaunti hii.

    Kila mara ukame unapobisha hodi, maisha ya wakaazi na mifugo wao huwa hatarini.

    Nchini Uganda katika Jimbo la Karamoja karibu na eneo hili la Turkana, Rais Museveni alijenga bwawa ambalo hutumiwa na jamii ya Karamoja ambayo ni jamii ya wafugaji.

    “Kwanini serikali ya Kaunti na ile serikali kuu zisiungane pamoja na kutafutia wananchi suluhisho mwafaka na la kudumu kama ilivyofanywa na Rais Museveni upande ule mwingine?…” anauliza Paul Jaling’a, kiongozi wa vijana katika Kaunti ya Turkana.

    Anna Emaret anasema amekuwa akigawana chakula na mifugo wake, lakini chakula kilipoisha, wakafa.

    “Inapaswa sisi kama vijana tuelimishwe jinsi ya kufuga mifugo kwa manufaa ya biashara. Isiwe tu kwamba tunafuga mifugo kisha kiangazi kikianza, tunarudi kuwa masikini.

    “Kuuza mifugo wakati wa mvua na kuwekeza fedha ili kujinusuru wakati wa kiangazi itasaidia pakubwa katika kuhakikisha kwamba ukame unasalia kuwa historia”.

    baadhi ya maeneo ya mashariki, kaskazini na kaskazini magharibi mwa Kenya ambapo kuna jamii za wafugaji, huenda zikakabiliwa na mzozo wa uhaba wa chakula.

  • Watu 49 wauawa katika shambulio kwenye misikiti New Zealand

    Watu 49 wauawa katika shambulio kwenye misikiti New Zealand

    Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern anasema watu 49 wameuawa na wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa vibaya baada ya kuzuka mashambulio katika misikiti miwili katika mji wa Christchurch, huko New Zealand.

    Waziri mkuu huyo amelitaja shambulio hilo kuwa mojawapo lililotanda ‘kiza kikubwa’ siku ya leo nchini humo.

    Wanaume watatu na mwanamke mmoja wamekamatwa, kamishna wa polisi Mike Bush anasema, lakini ameonya kwamba huenda washukiwa zaidi wapo.

    Inaarifiwa kwamba washambuliaji hao hawakuwa kwenye orodha ya magaidi wanaosakwa lakini ni wazi kwamba wana itikadi kali.

    Waziri mkuu wa Australia Scott Morrison amesema mojawapo ya waliokamatwa ni raia wa Australia.

    Amemtaja mshukiwa wa shambulio hilo kuwa “gaidi mwenye itikadi kali za mrengo wa kulia”.

    Walioshuhudia mkasa huo wameambia vyombo vya habari kwamba walilazimika kutoroka kuokoa maisha yao na waliona watu walioanguka chini wanaovuja damu nje ya mskiti wa Al Noor.

    Polisi inasisitiza kwamba hali bado haijaimarika na wamethibitisha pia kwamba “vilipuzi kadhaa vilivyofungwa kwenye gari vimeharibiwa”.

    Maafisa wameshauri misikiti yote katika mji huo ifungwe mpaka ilani itakapotolea, wakieleza kwamba hili lilikuwa shambulio la vurugu ambalo halikutarajiwa.

    Mohan Ibrahim, ambaye alikuwa katika eneo hilo la msikiti wa Al Noor ameliambia gazeti la Herald: “Awali tuliona ni hitilafu za umeme lakini mara tu, watu wote wakaanza kutoroka.

    “Bado rafiki zangu wamo ndani. Nahofia usalama wa maisha ya rafiki zangu.”

    Nini kilichofanyika katika mskiti?

    Bado haijulikani wazi nini kilichofanyika ndani ya misikti hiyo, taarifa mpaka sasa zimetoka kwa walioshuhudia mkasa na waliozungumza na vyombo vya habari.

    Mashahidi wametaja kuona watu wakiwa wameanguka chini wanavuja damu.

    Inaarifiwa mshambuliaji alilenga sehemu ya maombi ya wanaume, na baadaye kuelekea katika sehemu ya wanawake.

    Watu wamehamishwa pia kutoka msikiti wa pili katika kitongoji cha Linwood na kamishna wa polisi amesema “watu kadhaa wameuawa ” katika maeneo mawili.

     

  • Tshisekedi na Kabila watangaza serikali ya Muungano

    Tshisekedi na Kabila watangaza serikali ya Muungano

    Kiongozi mpya katika Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo, Felix Tshisekedi na mtangulizi wake Joseph Kabila wamesema wameamua kuunda serikali ya muungano kufuatia mazungumzo, shirika la habari la AFP linaripoti.

    Licha ya ushindi wa rais Tshisekedi — kiongozi huyo amejikuta akilazimika kugawanya uongozi tangu uchaguzi huo wa urais.

    Mpaka sasa hajafanikiwa kumteua waziri mkuu kutokana na kwamba muungano wa Kabila – Common Front for Congo (FCC) una uwingi katika bunge la taifa.

    Mkwamo huo umeweka kizuizi kwa maazimio ya Tshisekedi kuigeuza nchi hiyo inayogubikwa kwa rushwa na tuhuma za ukiukaji wa haki za binaadamu.

    Katika taarifa ya pamoja hapo jana Jumatano, Tshisekedi na Kabila wamesema kwamba licha ya “FCC kuwa na uwingi mkubwa bungeni” katika kuidhinisha matakwa yalioelezewa na wapiga kura, FCC na CACH wanaonesha uwajibikaji “wa malengo yao ya pamoja kuongoza pamoja kama sehemu ya serikali ya muungano” linaripoti AFP.

    Taarifa hiyo inafuata ziara ya Tshisekedi nchini Namibia wiki iliyopita ambapo alielezea kukasirishwa kwake kwa kutoweza kuwa na uwingi kuunga mkono chaguo lake la wadhifa wa waziri mkuu.

    Kwa miaka 18 iliyopita, taifa lenye utajiri wa madini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo limeongozwa na mtu mmoja: Joseph Kabila.

    Kwa muda ilionekana kana kwamba Tshishekedi, jina lake halingekuwa kwenye karatasi za kura.

    Kuongezea hilo, wakosoaji wake pia walikuwa wakisema Tshisekedi hajawahi kushikilia wadhifa wowote wa juu au kuwa na uzoefu wa usimamizi.

    Lakini kadri muda ulivyosogea amefanikiwa kupanda cheo, kuanzia mwaka 2008 ambapo alikuwa katibu wa taifa aliyeangazia masuala ya uhusiano wa nje.

    Tshisekedi, ingawa hana uungwaji mkono mkubwa kama wa babake, mwaka jana alisema kwamba akishinda urais ataunda tume ya ukweli, haki na maridhiano na kumuwajibisha Bw Kabila. Lakini alisema atamruhusu kusalia nchini DR Congo.

    Changamoto kubwa ni kuangalia vipi Tchisekedi anaweza kuleta amani na maridhiano kwa taifa hilo hususan eneo la mashariki ambako kumeshuhudia ghasia na umwagikaji damu mkubwa wa raia, na uwepo wa wanamgambo waliojihami wanaotekeleza mashambulio.

    Ni wazi kwamba ni wakati wa kihistoria kwa upinzani wa nchi hiyo, ambao umekuwa kando kando katika siasa za nchi kwa miongo kadhaa.

    Lakini swali kubwa sasa ni je makubaliano haya ya kuunda serikali ya muungano yana uzito kiasi gani katika ushawishi wa kiongozi huyu mkuu, na inaweka wapi matumaini ya raia wa Congo katika swala la mageuzi nchini?

    cc;BBCswahili

  • Auawa na simba aliyemfuga nyumbani kwake

    Auawa na simba aliyemfuga nyumbani kwake

    Mwanamume mmoja ameshambuliwa na simba aliyemfuga nyumbani kwake mashariki mwa Jamhuri ya Czech

    Michal Prasek alimmiliki simba huyo mwenye miaka 9 na simba jike aliyemfuga kwa ajili ya kuzalisha , hatua inayoarifiwa kuzusha wasiwasi kutoka kwa wakaazi.

    Babake Prasek aliupata mwili wake ndani ya kizuizi cha simba huyo na kuambia vyombo vya habari kwamba kilikuwa kimefungwa kwa ndani.

    Wanyama hao waliokuwa wanaishi katika vizuizi tofuati, walipigwa risasi na kuuawa na polisi walioitwa katika eneo hilo.

    Msemaji wa polisi amewaambia waandishi habari kwamba ilikuwa muhimu kwa simba hao kuuliwa ili kumfikia marehemu.

    Prasek, mwenye umri wa miaka 33, alimnunua simba huyo mnamo 2016 na simba jike huyo mwaka jana, na aliwaweka wote katika vizuizi alivyovitengeneza katika ua lake katika kijiji cha Zdechov.

    Awali alikatazwa ruhusa ya kujenga vizuizi hivyo, na alitozwa faini kwa kufuga wanyama hao kinyume na sheria.

    Lakini mvutano wake na maafisa wa utawala ulifikia mkwamo baada ya kukataa kuruhusu mtu yoyote kuingia kwake.

    Ukosefu wa vituo mbadala katika Jamhuri hiyo ya Czech, imemaanisha kwamba haingewezekana wanyama hao kuondolewa kwa lazima.

    Prasek aligonga vichwa vya habari mwaka jana baada ya mwendesha baiskeli kupambana na simba hao wakati Prasek alipokuwa akiwatembeza huku akiwa amewafunga kwenye nyororo.

    Baada ya polisi kuingilia kati, tukio hilo lilitazamwa kama ajali ya trafiki.

    “Tukio la leo huenda likasaidia hatimaye kutatua tatizo hili la muda mrefu,” amesema meya wa Zdechov , Tomas Kocourek.

     

  • Rubani wa naibu rais William Ruto afariki baada ya helikopta kuanguka Kenya

    Rubani wa naibu rais William Ruto afariki baada ya helikopta kuanguka Kenya

    Rubani wa naibu rais William Ruto amefariki katika jali ya ndege baada ya helikopta aliyokuwemo kuanguka nchini Kenya.

    Taarifa katika vyombo vya habari nchini zinaeleza kwamba ndege hiyo ilianguka Jumapili mwendo wa saa mbili usiku katika eneo la Turkana.

    Inaarifiwa kwamba Kapteni Mario Magonga amefariki pamoja na abiria wengine wanne.

    Polisi inasema helikopta hiyo imeanguka katika eneo la Labolo, kisiwa chenye milima ya volcano katikakati ya ziwa Turkana – Central Island National Park kaskazini magharibi mwa Kenya.

    “Taarifa zilizopo zinaashiria kwamba ndege mbili zilitua mapema katika kambi ya Lobolo katika kisiwa hicho kilichopo kwenye mbuga ya kitaifa, hatahivyo moja ndio iliyofanikiwa kutua salama katika eneo hilo,” idara ya polisi imesema katika taarifa yake rasmi.

    Inaarifiwa kwamba vikosi vya usalama vimetumwa katika eneo hilo katika kusaidia kwenye jitihada za kuondosha miili na masalio ya ndege hiyo.

    Kufikia sasa, chanzo cha ajali bado hakijajulikana.

    Kapteni Magonga ni nani?

    Alikuwa rubani wake naibu rais wa Kenya William Samoei Ruto.

    Aliwahi kuwa rubani katika jeshi la Kenya.

    Ni mzawa wa Nyamataro, Kitutu Chache kusini, kaunti ya Kisii – kusini magharibi mwa Kenya.

    Babake ni mwanajeshi mstaafu; Brigedia (rtd) Magonga.

    Alikuwa rubani mkuu wa helikopta za kampuni ya KIDL helicopters – inayotoa huduma za usafiri binafsi katika eneo zima la Afrika mashariki.

    Alikuwa mkufunzi aliyehitimu wa helikopta.

    Alipokea mafunzo kutoka kikosi cha ulinzi Kenya KDF.

    Ana uzoefu wa kuendesha ndege kwa zaidi ya saa 5500 kwenye ndege za injini moja na injini zaidi ya moja.

    Kwa waliofahamu, wanamueleza kuwa rubani aliye na taaluma na uzoefu mkubwa, na aliheshimika pakubwa.

  • Wanawake walio na maumbo makubwa  nchini Uganda wamewasilisha  malalamiko yao kwa  spika wa Bunge

    Wanawake walio na maumbo makubwa nchini Uganda wamewasilisha malalamiko yao kwa spika wa Bunge

    Waandalizi wa shindano la wanawake walio na maumbo makubwa nchini Uganda wamewasilisha malalamiko yao kwa spika wa bunge kufafanua madhumuni yao.

    Wamesema kuwa lengo lao sio kutumia shindano la ‘Miss Curvy Uganda” kuvutia watalii kuja nchini humo.

    ”Haya ni mashindano ya urembo wa wanawake wanene”alisema Annie Mungoma, mkurugenzi mkuu wa mashindano hayo.

    Bi. Mugoma aliongeza kuwa mtazamo wao itaondosha fikra za kimagharibi kuwa urembo unamaanisha mtu kuwa mwembamba.

    ”Tunataka kuwapatia motisha wanawake wenye maumbo makubwa kujiamini kwamba wao pia ni warembo”.

    Siku mbili zilizopita spika wa bunge Rebecca Kadaga aliyepinga vikali mashindano hayo amebadili msimamo wake baada ya kupokea ufafanuzi huo.

    Ameahidi mkono juhudi zao na kutoa ufafanuzi kwa bunge ili kuondoa fikra kwamba mashindano hayo ni ya aibu kwa jinsia ya mwanamke.

    Tangu shindano shindano hilo lilipozinduliwa mapema mwezi huu, wanasiasa,wanaharakati wa haki za wanawake na viongozi wa kidini wamejitokeza na kulishtumu vikali.

    Waziri wa utalii nchini Uganda Godfrey Kiwanda alipendekeza kuwe na onyesho la wanawake wenye maumbo makubwa ili kuvutia wageni zaidi wanaoitembelea nchi hiyo.

    Akizungumza katika uzinduzi wa shindano hilo , waziri huyo alisema kuwa itakuwa “tukio la kipekee ambalo litawaonesha mabanati wakionesha maumbo yao mazuri yaliyo nona”

    Kauli hiyo ilizua mjadala mkali hasa katika mitandao ya kijamii huku baadhi ya watu wakimshutumu bwana Kiwanda kwa kuzungumza juu ya wanawake wanene kama wananyama huku mwanamke mmoja akihoji kama ingewezekana basi wawekwe bustanini ili watazamwe kama wanayama watendewavyo “.

    Licha ya mjadala huo kufikia sasa washiriki 200 kutoka sehemu mbalimbali za Uganda pamoja na nchi jirani ya Rwanda wamejisajili kushiriki shindano la Miss Curvy Uganda linalotarajiwa kufanyika mwezi wa June mwaka huu.

    cc.BBCswahili