RIO2016: WANARIADHA WA KENYA WAISHI KWENYE MAZINGIRA MAGUMU BAADA YA OLIMPIKI

RIO2016: WANARIADHA WA KENYA WAISHI KWENYE MAZINGIRA MAGUMU BAADA YA OLIMPIKI

Like
241
0
Thursday, 25 August 2016
Slider

Wanariadha wa Kenya wamekuwa wakiishi kwenye makazi ambayo hayawafurahishi timu hiyo baada ya kumalizika kwa Michezo ya Olimpiki mjini Rio, mmoja wa wanariadha hao amelalamika.

Mkimbiaji wa mbio za Marathon, Wesley Korir, ambaye pia ni mbunge, amepakia picha za hoteli anayosema ni duni kwenye mitandao ya Twitter na Facebook akilalamika.

“Timu iliyoongoza Afrika na timu ya pili dunia nzima katika riadha, na hivi ndivyo tunavyotunzwa ,” ameandika.

Amelinganisha mazingira ya eneo wanamoishi na mtaa wa mabanda.

Wanariadha hao walilazimika kuondoka eneo la kifahari waliomoishi wanamichezo wakati wa michezo hiyo, ambalo hufahamika kama Kijiji cha Olimpiki, baada ya eneo hilo kufungwa kufuatia kumalizika kwa michezo.

Kwenye mtandao wake wa Twitter, alisema: “Na hivi ndivyo mambo yanavyoendelea Rio #TeamKenyaa @UKenyatta haya ndiyo makazi ya timu ya kenya kwa usiku wa leo!!”

Bw Korir amekuwa akijibu maswali kuhusu ni nani ambaye bado yuko nchini Brazil

Alipoulizwa ni kwa nini anadhani timu ya wanariadha bado iko mjini Rio, alisema huenda wasimamizi wa Olimpiki Kenya walisubiri kuwanunulia wachezaji tiketi nafuu, na ndipo wakaamua kuwaweka muda zaidi Rio.

Mbunge huyo wa Kenya ametoa wito uchunguzi ufanyike kuhusu usimamizi wa timu ya Kenya wakati wa michezo na baada ya michezo baada ya kutokea kwa hitilafu mbali mbali, ikiwemo kutonunuliwa kwa tiketi ya mwanamichezo maarufu mshindi wa dunia katika mchezo wa kurusha mkuki Julius Yego.

Comments are closed.