Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege na kumwamuru kurejesha Dola za Marekani 42,543 (Sh68,068,800).
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando alimtia hatiani Ekelege baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi saba wa upande wa mashtaka, vielelezo na ushahidi wa utetezi uliotolewa na mshtakiwa.
Hakimu Mmbando alisema katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulithibitisha mashtaka yote yanayomkabili Ekelege pasipo kuacha shaka na kumhukumu kifungo hicho.
Mmbando alisema viongozi wapo kwa ajili ya kulinda masilahi na rasilimali za nchi ili wananchi waweze kuifurahia keki ya Taifa na siyo kufuata matakwa yao.
Alisema kiongozi kama Ekelege aliaminiwa na kuteuliwa na Rais ili aweze kuiongoza TBS ambayo ni sehemu ya chanzo cha mapato ya nchi, hivyo kuzembea kwake na kusababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha, hapaswi kuonewa huruma ili iwe fundisho kwa viongozi wengine.
Katika shtaka la kwanza la kutumia madaraka yake vibaya kwa kuziondolea asilimia 50 ya ada ya utawala, Kampuni za Jaffar Mohamed Ali na Quality Motors, Ekelege alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela.
Katika shtaka la pili la kuondoa ada za kampuni hizo bila idhini ya Baraza la Utendaji kinyume na utaratibu wa TBS pia alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na katika shtaka la tatu la kusababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha alifungwa tena kifungo kingine cha mwaka mmoja jela.
Hakimu Mmbando alisema vifungo hivyo vitakwenda pamoja, hivyo mshtakiwa huyo atatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela na kurejesha Sh68,068,800 anazodaiwa kulisababishia shirika hilo hasara kwa uzembe.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Janeth Machulya alisema kwa kuzingatia uzito wa mashtaka aliyotenda Ekelege na alivyoshindwa kuitumikia dhamana aliyopewa, anastahili adhabu kali ili iwe fundisho kwa viongozi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Machulya aliiomba mahakama wakati ikifikiria kutoa adhabu kwa Ekelege izingatie sheria ya uhujumu uchumi.
Wakili aliyekuwa akimtetea Ekelege, Majura Magafu aliiomba Mahakama impunguzie adhabu mteja wake kwa kuwa ni kosa lake la kwanza, ana familia ya mke, watoto na wazee wanaomtegemea.
Katika utetezi wake, Ekelege alikana kusababisha hasara kwa kutoa msamaha, akisema hali hiyo ilitokana na udanganyifu uliofanywa na kampuni husika.
Alidai kuwa kampuni hizo zilidanganya na kusababisha kutoa uamuzi mwingine ambao haukuwa sahihi na bodi ya wakurugenzi ya TBS ilipoitishwa iliridhia kuwa msamaha huo haukutolewa kwa makusudi.
Alisema kwa kuwa TBS haikuwa na historia ya kutoa msamaha hiyo na kwa kuwa ilikuwa mara ya kwanza na kampuni hizo hazikuwa na uaminifu, aliiomba Mahakama imwachie huru.
Akijitetea, alisema kampuni ya Jaffar Mohamed Ali ilipata msamaha baada ya kuwasilisha maombi yake ikidai kuwapo kwa ushindani uliotokana na wakala mwenzake, Total Otomotive Services, aliyekuwa akifanya mchezo mchafu wa kuvuta wateja kwa kutokagua viwango vya ubora wa magari yao na kuwapa vyeti vya ubora.
Alidai kuwa menejimenti ya TBS iliijadili na kukubaliana na matatizo hayo na ikatoa msamaha kwa kipindi cha Oktoba 2007 na Machi 2008 na alitakiwa kuanza kulipa tozo na gharama zake ifikapo Aprili Mosi, 2008.