WATU 60 wameuawa katika shambulizi la bomu la kujitoa mhanga nchini Pakistan karibu na mpaka na India, ikiwa ni shambulizi baya zaidi la kigaidi kuwahi kutokea nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.
Makundi kadhaa, likiwemo la Taliban, yamedai kuhusika na shambulizi hilo ambalo liliwajeruhi zaidi ya watu 120, lililotokea karibu na kivuko pekee cha mpaka kati ya Pakistan na India cha Wagah mashariki ya mji wa mashariki mwa Pakistan, Lahore.
Shambulizi hilo lilitokea baada ya kukamilika sherehe maalumu za kijeshi za kushusha bendera ambazo huwavutia maelfu ya watazamaji kila siku na ni maarufu kwa watalii.
Pakistan inakumbwa na uasi wa ndani unaofanywa na kundi la Taliban ambao umesababisha mauaji ya maelfu ya watu katika miaka ya karibuni.