JESHI la Burkina Faso limeapa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa baada ya kuimarisha udhibiti wake katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Vikosi vya usalama hapo jana vimefyatua mabomu ya kutoa machozi na risasi angani ili kuwatawanya waandamanaji wanaopinga hatua ya jeshi kutwaa madaraka baada ya Rais Blaise Compaore kujiuzulu.
Majeshi yaliingia katika uwanja maarufu wa Place de la Nation mjini Ouagadougou na kuchukua udhibiti wa makao makuu ya televisheni ya taifa katika hatua ya kuonyesha ubabe, licha ya wito kutoka kwa jamii ya kimataifa na waandamanaji wa kutaka nchi hiyo irejeshwe katika utawala wa kiraia.