MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa wilaya hiyo kutokubali kuuza maeneo ya ufukwe wa Bahari ya Hindi kwa kiasi kidogo cha fedha kwani thamani ya maeneo hayo ni kubwa.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ametoa rai hiyo wakati akiongea kwa nyakati tofauti na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho katika matawi ya Raha leo na Ufukoni yaliyopo katika kata ya Rahaleo wilayani humo.
Mama Salma Kikwete amesema hivi sasa kuna wageni wengi ambao wanaenda kwa wananchi na kununua maeneo ya ufukweni kwa bei ya chini lakini endapo wamiliki wa maeneo hayo watakuwa na subira watayauza kwa bei kubwa kwa kipindi cha miaka michache ijayo.