WATU wawili raia wa Australia waliopatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevywa wamehamishwa kutoka jela mjini Bali nchini Indonesia leo na kupelekwa katika kisiwa kimoja nchini humo ambako watauwawa kwa kupigwa risasi.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari nchini Australia, hatua hiyo ya adhabu ya kifo kwa Myuran Sukumaran na Andrew Chan imeongeza wasiwasi wa kidiplomasia, huku kukiwa na maombi ya msamaha kwa watu hao wawili kutoka Australia, na imeiweka Indonesia katika hali ya kuonekana kuwa inatumia adhabu ya kifo kwa raia wa kigeni.
Chan na Sukumaran walihukumiwa mwaka 2005 kama viongozi wakuu wa genge linalojulikana kama Bali Nine, ambao walikamatwa katika uwanja wa ndege wa Denpasar kwa kujaribu kusafirisha kilo 8 za mihadarati kwenda Australia.