MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, SAID MECKY SADICK kwa kushirikiana na Meya wa Manispaa ya Kinondoni, YUSUPH MWENDA wameanza kutekeleza agizo lililotolewa na Rais JAKAYA KIKWETE la kuondoa maji katika makazi ya watu kwenye maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo yaliyosababishwa na mvua zilizokuwa zikinyesha jijini hivi karibuni.
Rais KIKWETE alitoa agizo hilo wiki iliyopita wakati alipofanya ziara katika maeneo ya Namanga, Nyaishozi, Dawasco na Basihaya kuangalia athari za mafuriko zilizosabaisha wananchi kuyakimbia makazi yao.
Akizungumza wakati wa zoezi la kuanza kuyaondoa maji katika maeneo hayo mwishoni mwa wiki Dar es Salaam, SADICK amesema maji yaliyojaa katika maeneo ya Basihaya na Nyaishozi yanatolewa kwa pampu na kuelekezwa katika Bwawa la Dawasco ambako yatatolewa na kuelekezwa kwenye mtaro mkubwa ambao umeanza kuchimbwa kwa ajili ya kuelekezwa baharini.