WIZARA ya maendeleo ya mifugo na uvuvi nchini imewasilisha rasmi makadilio ya matumizi yake katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2015 hadi 2016 yanayokadiliwa kuwa ni zaidi ya bilioni 68 kwa lengo la kuboresha na kuimarisha utendaji kazi kwa maendeleo ya Taifa.
Akiwasilisha makadilio hayo Waziri wa wizara hiyo dokta TITUS KAMAN amesema kuwa endapo fedha hizo zitapitishwa, zitaisaidia Wizara katika utekelezaji wa shughuli muhimu kwa kipindi cha mwaka mzima kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Katika hatua nyingine kamati ya kudumu ya Bunge ya kilimo, ufugaji na maji kupitia kwa mwakilishi wake ambaye ni mbunge wa viti maalum dokta CHRISTINE ISHENGOMA imeishauri serikali kuwekeza zaidi katika uvuvi ili kuleta manufaa zaidi kwa wananchi.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Wawi kupitia chama cha Cuf mheshimiwa HAMAD RASHID amesema kuwa ni vyema serikali ikashirikiana na sekta binafsi pamoja na kutumia bandari zilizopo ili kuhakikisha watanzania wananufaika kupitia uvuvi.
Katika hatua nyingine, Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera, uratibu na bunge mheshimiwa JENISTA MHAGAMA ameomba muongozo wa mwenyekiti kwa kudai kuwa mwasilishaji wa maoni ya kambi ya upinzani mheshimiwa MKIWA KIMWANGA amewasilisha hoja zisizo za ukweli juu ya hotuba iliyotolewa na Waziri mkuu kuhusu makadilio ya bajeti ya ofisi hiyo.