RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa linalochunguza jinsi dunia inavyoweza kujikinga na majanga ya magonjwa ya milipuko katika miaka ijayo, Dokta Jakaya Mrisho Kikwete, amewasili mjini Geneva, Uswisi, kwa ajili ya kuendesha vikao vya Jopo hilo.
Vikao hivyo vitakuwa ni awamu ya pili kwa Jopo ambalo liliteuliwa Mwezi Aprili, mwaka huu, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , Ban Ki Moon.
Wajibu mkuu wa Jopo hilo ni kutoa mapendekezo ya kuimarisha mifumo ya kitaifa na kimataifa, ili kuweza kuzuia ama kudhibiti kwa uhakika zaidi majanga ya magonjwa ya milipuko kufuatia balaa la Ebola katika nchi za Liberia, Sierra Leone na Guinea ambalo limeua maelfu ya watu.