Manchester United mnamo Jumapili walithibitisha kumnunua kipa wa Argentina Sergio Romero kwa mkataba wa miaka mitatu.
Mlindalango huyo wa miaka 28 atajaza pengo lililoachwa na Victor Valdes, aliyetimuliwa Old Trafford baad aya kudaiwa kukataa kucheza na timu ya akiba ya United.
“Kuchezea timu kubwa zaidi duniani kwangu ni kutimia kwa ndoto,” alisema Romero kupitia taarifa kwenye tovuti ya klabu hiyo.
“Louis van Gaal ni meneja mzuri sana na nasubiri sana kuanza kibarua hiki mpya na cha kusisimua kwenye maisha yangu ya uchezaji.”
Romero alianza kucheza ligi kuu ya Argentina ya Primera Division akiwa na klabu ya Racing mwaka 2007.
Tangu wakati huo, amechezea taifa lake mara kadha na alikuwa kwenye kikosi cha Argentina Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil ambako walimaliza nambari mbili nyuma ya Ujerumani.
Tayari anafamu mbinu za meneja wa sasa wa Manchester United Van Gaal, kwani alikuwa kocha Romero alipokuwa katika klabu ya Uholanzi ya AZ Alkmaar.
“Alikuwa kipa mchanga nilipokuwa AZ Alkmaar na ninafurahia kwamba anajiunga na Manchester United,” Van Gaal alisema kwenye tovuti ya klabu hiyo.
“Atafaa sana timu na nasubiri kuanza kufanya kazi naye tena.”