JESHI la polisi kanda maalum ya Dar es salaam limefanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa watatu kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa afisa wa polisi ELIBARIK PALANGO yaliyotokea nyumbani kwakwe Yombo kilakala tarehe 4 mwezi huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam leo Naibu kamishna wa polisi kanda maalum Dar es salaam SIMON SIRRO amesema kuwa watuhumiwa hao ambao ni madereva bodaboda wamekamatwa baada ya jeshi kufanya msako mkali katika jiji la Dar es salaam.
Aidha Kamishna SIRRO amewataja watuhumiwa hao kuwa ni pamoja na SALIM KATIBU mwenye umri wa miaka 32 mkazi wa tabata , ISMAIL SAID miaka 36 mkazi wa yombo makangarawe na PIRIMINI HAULEMI miaka 25 mkazi wa yombo makangarawe.
Wakati huo huo jeshi la polisi katika oparesheni yake endelevu limefanikiwa kukamata watuhumiwa wawili wakiwa na bunduki aina ya SMG ikiwa na risasi nane.
Vilevile jeshi linawashikilia watuhumiwa watatu kwa kukutwa na vipande vinne vya meno yanayodhaniwa kuwa ya tembo lakini pia limewatia mbaroni watuhumiwa watano wakiwa na sare za jeshi la wananchi Tanzania kinyume na sheria.