Meneja wa Chelsea Jose Mourinho amejipata akishutumiwa vikali baada ya ripoti kuibuka kwamba amemtenga daktari wa mabingwa hao wa Ligi ya Premia Eva Carneiro.
Ripoti kwenye vyombo vya habari Uingereza zinasema Carneiro hatakuwa tena akihudhuria mechi za Chelsea wala vikao vya mazoezi baada ya Mourinho kumzomea yeye na daktari wa viungo Jon Fearn kwa kukimbia uwanjani kumhudumia Eden Hazard dakika za mwisho za mechi ya wikendi iliyopita iliyoisha sare 2-2 nyumbani dhidi ya Swansea City.
Mourinho, aliyesema Carneiro na Fearn walionyesha kutofahamu mchezo, amekashifiwa vikali kutoka kila upande, huku daktari mkuu wa zamani wa Liverpool Peter Brukner akitaja tabia yake kuwa ya “kufedhehesha”.
Kupitia taarifa Alhamisi, Kundi la Madaktari wa Ligi ya Premia lilitaja kushushwa madaraka kwa Carneiro kuwa hatua isiyo ya “haki na inayozidi”.
Waliongeza: “Kwenye kisa hicho kilichoangaziwa sana cha mechi hiyo dhidi ya Swansea, matabibu Chelsea waliitwa wazi uwanjani na refa msimamizi wa mechi kumhudumia mchezaji.
“Kukataa kuingia uwanjani kungekuwa ni kukiuka jukumu lao la utunzaji ambalo huhitajika kutekelezwa na madaktari kwa mgonjwa wao.
“Ni jambo la kusikitisha sana kwamba Dkt Carneiro amelazimishwa kuwekwa kwenye macho ya wanahabari na kubadilishwa kwa majukumu yake, sababu tu ikiwa kwamba alitii maadili ya taaluma yake na kuifanya kazi yake vyema.”
Chelsea na Mourinho bado hawajazungumzia ripoti hizo kwamba majukumu ya Carneiro yamebadilishwa, lakini anatarajiwa kuhutubia wanahabari katika kikao cha kila wiki na wanahabari Ijumaa.