MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta Mohamed Gharib Bilal leo amezindua rasmi Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano pamoja na kufungua Kituo cha kisasa cha kimataifa cha mawasiliano ya Intaneti kitakachojulikana kwa jina la IP-POP ikiwa ni jitihada za Serikali kuboresha na kuimarisha sekta ya TEHAMA nchini kwa kuboresha na kuongeza miundombinu itakayosaidia kutoa huduma bora katika Sekta ya mawasiliano.
Akizungumza katika hafla hiyo Dokta Bilal amesema kuwa miundombinu hiyo ya mawasiliano ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa na nchi jirani zisizopakana na bahari. Hivyo miundo mbinu hiyo ni muhimu sana hasa katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya maendeleo ya Mwaka 2025 na malengo ya Milenia MDGs ya mwaka 2000-2015 kuhusu kupambana na umaskini.