MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya umesema hautawavumilia watumishi wa hospitali ya Mkoa wa Kagera wanaojihusisha na vitendo vya kughushi nyaraka za kuchukulia dawa katika maduka ya dawa na kuusababishia Mfuko kulipa fedha ambazo hazijatumika kihalali.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Michael Mhando ameyasema hayo mkoani humo wakati akizungumza na uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Kagera kabla ya uzinduzi wa mpango wa Madaktari Bingwa ili kusaidia kutoa huduma kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
Mhando amesema kuwa Mfuko huo una jukumu la kulinda fedha za wanachama wake na kuhakikisha zinatumika kwa matumizi sahihi hivyo hawapo tayari kuendelea kuvumilia watoa huduma wasio waaminifu.