SERIKALI imeliagiza Shirika la Reli Tanzania (TRL), kupitia upya mikataba ya ununuzi wa vichwa vya treni na mabehewa ili kubaini kasoro zilizojitokeza na kuchukua hatua stahiki kabla ya maboresho ya reli ya Tanga-Moshi na Arusha.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa agizo hilo mkoani Kigoma wakati akikagua miundombinu ya reli na kusissitiza nia ya serikali kufufua reli ya kanda ya kaskazini ili kuimarisha huduma ya uchukuzi katika mikoa hiyo.
Prof. Mbarawa amesema Serikali imedhamiria kuliongezea nguvu TRL ambapo baadhi ya mitambo kutoka Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) itakabidhiwa kwa shirika hilo na hivyo kulitaka kuwa na mpango madhubuti wa kufanya biashara na kurudisha hadhi ya usafiri wa reli hapa nchini.