Mkali wa Nigeria, Ludemilade Martin Alejo maarufu kama YCEE, anatarajiwa kutua bongo, Jumapili hii.
Mkali huyu anatarajiwa kuja Tanzania kwa dhumuni la kuutangaza zaidi muziki wake akiwa na ngoma kama Omo Alhaji, Jagabana’ na nyinginezo.
Ziara hiyo itaambatana na mkutano wa waandishi wa habari siku ya Jumatatu, ikifuatiwa na ziara ya kutembelea vituo mbalimbali vya habari kuanzia Agosti 29 mpaka tarehe Septemba 1.
Pamoja na hayo amesema kuwa, anayo shauku kubwa juu ya ziara yake kwani hii ni mara yake ya kwanza hapa nchini.”Nina hamu sana ya kukutana na mashabiki wangu wa Tanzania, kwa sababu upendo wanaonipa kupitia mitandao ya kijamii ni wa ajabu na nina furaha sana ya kukutana na watu wapya” alisema.
Baada ya ziara yake nchini Tanzania, YCEE ataenda nchini Afrika Kusini kuendelea na ziara yake ya kukuza na kutangaza muziki wake, na anatarajia kuachia orodha ya nyimbo mpya baadaye mwaka huu utakaofahamika kwa jina la ‘The First Wave’.
Msanii pia ni miongoni mwa wasanii wanaopenda kusaidia jamii kwa kuwafikia vijana wa kiafrika katika masuala ya maendeleo na michezo. Katika ziara yake hapa nchini, YCEE atatoa msaada wa fedha kwa kituo cha masuala ya umaskini na ukosefu wa upatikanaji wa elimu kwa watoto wa mitaani Kigamboni.
Kigamboni Community Center (KCC) ni kituo kinachoshughulika na masuala ya kutokomeza umaskini, huku kikijikita katika kutoa elimu ya chekechea na msingi kwa watoto ambao wako mbali na upatikanaji wa elimu.
KCC pia hutoa fursa nyingine za kujifunza kwa vijana wa Kigamboni, na pia hutoa elimu ya jamii, madarasa ya kuendeleza vipaji na mafunzo ya ufundi stadi. YCEE ameamua kuunga mkono kituo hiki kwa kwa sababu ya kujitolea kwao kukuza vipaji na kujenga upatikanaji wa elimu kwa jamii.
YCEE alipata umaarufu kimataifa mara baada ya kuteuliwa kushiriki katika mchakato wa ‘Revelation of
the Year’ katika tuzo za muziki za MTV Africa Music Awards 2015 , na kuteuliwa tena katika tuzo za
‘Best Artist in African Pop’ mwaka 2015 kwenye tuzo za 'All Africa Music Awards'. Pia alifanikiwa
kuibuka mshindi wa tuzo za ‘Rookie of the year’ kwenye The Headies mwaka huu.
Kwa sasa YCEE yupo chini ya lebo ya Tinny Entertainment, ambapo anaendelea kukuza muziki wake
kibiashara kupitia wimbo wake mpya 'Sun mi' ambao ni remix ya ' Condo ' akishirikiana na Khuli
Chana wa Afrika Kusini, KiD X , sambamba na DJ Consequence aliyeshirikiana nae hivi karibuni
katika wimbo mwingine ' In Benz '