Madini mapya yamegunduliwa nchini Tanzania, katika eneo lenye madini ya kipekee la Manyara, na kupewa jina Merelaniite.
Jina hilo limetokana na eneo ambalo madini hayo yalipatikana, Merelani (Mererani) katika milima ya Lelatema katika wilaya ya Simanjiro katika eneo la Manyara.
Eneo hilo linafahamika sana kwa madini ya Tanzanite.
Madini hayo yaligunduliwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kiteknolojia cha Michigan cha Marekani, makavazi ya historia asilia ya London, chuo kikuu cha Di Firenze cha Italia na makavazi ya historia asilia ya Smithsonian ya Washington.
Wataalamu sita waliofanya uchunguzi, kwenye makala iliyochapishwa kwenye jarida la Minerals (Madini) wanasema madini hayo yana vipande vinavyofanana na sharubu vya rangi ya kijivu vya urefu wa milimita moja hivi, ingawa kuna baadhi vyenye urefu wa hadi mililita 12.
Kipenyo cha vipande hivyo ni mikrometa kadha.
Madini hayo yanakaribiana na madini ya zoisite (aina ya tanzanite), prehnite, stilbite, chabazite, tremolite, diopside, quartz, calcite, graphite, alabandite na wurtzite.
“Madini haya mapya yametambuliwa na taasisi inayoyapa majina madini, IMA CNMNC (2016-042), na kupewa jina linalotokana na eneo yalipogunduliwa kwa heshima ya wachimba migodi wa eneo hilo wa zamani, wanaoishi na wanaofanya kazi,” makala ya wataalamu hayo inasema.
“Wilaya ya Merelani imekuwa maarufu tangu mwishoni mwa miaka ya 1960 kutokana na aina ya madini ya thamani ya rangi ya samawati kwa jina zoisite yafahamikayo kama tanzanite, lakini ni eneo muhimu sana kwa wanaotafuta madini ya kipekee na ni eneo la kusisimua sana kutafuta madini mapya,” John Jaszczak, mwanafizikia katika Chuo Kikuu cha Kiteknolojia cha Michigan, na aliyeongoza katika kuandika makala kuhusu ugunduzi wa madini hayo anasema.
Madini hayo yalitambuliwa mara ya kwanza mwaka 2012 na Simon Harrison na Michael Wise, bila wataalamu hao kuyafahamu vyema, pale walipogundua vitu vilivyoonekana kama nyaya ndogo zilizokuwa zimedunga na kuingia ndani ya vipande vya madini ya chabazite.
Baadaye uchunguzi zaidi ulifanywa na ikagunduliwa kwamba yalikuwa madini tofauti.