Kiungo wa Yanga thabani kamusoko anataka nguvu ya mashabiki wa timu yao siku ya Jumamosi wakati Yanga itakapokuwa inacheza nyumbani dhidi ya Wolaitta Dicha mchezo wa mtoano kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya kombe la shirikisho Afrika.
Kamusoko amesema kipindi hiki ambacho timu ipo kwenye wakati mgumu wachezaji wanahitaji zaidi sapoti ya mashabiki kuliko kitu kingine.
“Timu inapokuwa haifanyi viruri ndiyo inahitaji sapoti kubwa ya mashabiki kwa hiyo nawaomba mashabiki waje kwa wingi kuisapoti timu yao kwa sababu bila wao inakuwa ngumu kwa wachezaji. Kwa sasa timu ipo katika kipindi kigumu na ndiyo hali ya mpira, timu haiwezi ikawa inashinda kila siku”-Thabani Kamusoko amezungumza na Yahaya Mohamed ‘Mkazuzu’ mjini Morogoro.
Mchezaji huyo raia wa Zimbabwe amesema mchezo wa jumamosi utakuwa mgumu hivyo wanahitaji kuwaheshimu wapinzani wao kwa hatua waliyofika.
Mashindano ya Caf magumu kwa sababu ukiona timu imefika hatua ambayo ikicheza mechi mbili ikishinda inaweza kuingia hatua ya makundi sio ya kuichukulia poa, Caf ni mashindano makubwa sana. Sisi tumejiandaa vizuri, tunajua timu tunayokutana nayo iko vipi tumefanya mazoezi kwa ajili ya mechi ya Jumamosi ili tuingie tena hatua ya makundi.
Amesema pia kwa sasa anapambana kuhakikisha anarejea kwenye kiwango chake baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha.
“Majeraha sio mazuri, ukikaa muda mrefu bila kucheza mpira huwezi kurudi mara moja kwa hiyo unarudi taratibu hadi ifike kipindi wewe mwenyewe unaona umekaa sawa. Nimerejea lakini najitahidi nirudi kwenye kiwango changu naamini taratibu nitakuwa poa.”