Rais wa Uganda Museveni anakanusha kwamba Bobi Wine amejeruhiwa

Rais wa Uganda Museveni anakanusha kwamba Bobi Wine amejeruhiwa

Like
549
0
Monday, 20 August 2018
Local News

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amekanusha kwamba mbunge wa upinzani Bobi Wine amejeruhiwa.

Katika taarifa yake ya kwanza kuhusu afya ya mbunge huyo aliyekamatwa na vikosi vya usalama nchini, Museveni amevishutumu vyombo vya habari kwa kile alichokitaja ni kueneza habari zisizo za kweli kuhusu suala hilo.

Kulingana na ripoti mbalimbali za vyombo vya habari mbunge huyo ambaye pia ni msanii, Robert Kyagulanyi ana matatizo ya figo ambayo yanahitaji kutibiwa ipasavyo na madaktari bingwa waliobobea katika kutiba sehemu nyeti kama hizo za ndani ya mwili.

“Vyombo vya kueneza habari zisizo za kweli vimekuwa vikitangaza kwamba mjukuu wetu, asiye na nidhamu Bobi Wine, ni mgonjwa mahututi, hawezi kuzungumza na mengineyo.

“Wamekuwa wakisema kuwa huenda maafisa wa usalama wamemjeruhi vibaya Bobi Wine kwasababu ya namna walivyokabiliana na wabunge wakati wakiwakamata.

“Nimeamua kuwasiliana na madaktari wa jeshi, kwasababu ya nidhamu ya jeshi, madaktari wa UPDF daima wanachukua tahadhari katika hali kama hizi. Tayari Bobi Wine alionekana na madaktari Arua, Gulu na Kampala. Hakuwa na majeraha ya kichwa, kifua au mifupa kuvunjika, wameniarifu,” ilisema taarifa ya rais.

Kadhalika Museveni alilaumu watu maalum ambao alieleza kuwa ni wa nje wanaotafuta kuingilia siasa za nchi hiyo.

Chama cha wafanyakazi wa afya nchini Uganda kinasema mahali wanapohifadhiwa wabunge wa upinzani na vyombo vya usalama akiwemo Bobi Wine ni ya hatari na inaweza kuwasababishia vifo.

Viongozi wa chama hicho wamesema madaktari wa Jeshi la UPDF hawana ujuzi wa kutosha kuwafanyia matibabu wabunge hao wanaodaiwa kujeruhiwa vibaya na maafisa wa usalama.

Wameelezea kuwa wako tayari kushirikiana na UPDf kuwashughulikia wabunge hao na washukiwa wengine kufuatia ghasia hizo.

Daktari Edward Ekwaro Ebuku, rais wa chama cha wafanyakazi wa afya Uganda ameeleza, ‘Ugonjwa wa figo unatakiwa uangalizi wa dharura, jeshi la Uganda limemficha huyu Bobi Wine, isitoshe walimkataza Daktari wa familia kumtibu’.

‘Sasa hivi hatujui hali yake ikoje. Lakini tunafikiria wamemficha kwasababu hali yake ni mbaya zaidi’.

Wataalamu wa afya wanafafanua kuwa mtu akiwa na matatizo kwenye figo ni rahisi sana sehemu zingine kama maini na ubongo wake kuathirika iwapo hatua za dharura hazichukuliwi kumtibu.

Wameongezea kuwa mbunge Francis Zake ambaye ni miongoni mwa waliokamatwa yuko katika hali mahututi na anahitaji kuhamishwa kutoka hospitali moja hadi nyingine kupata matibabu ya hali ya juu.

Wamejitolea kushirikiana na UPDF kutoa matibabu ili kuyanusuru maisha ya wahanga wote wa ghasia waliojeruhiwa na waliomo katika hali mbaya.

‘Hatujapata ruhusa kuingia kambi za jeshi pahali hawa wabunge wa Uganda, tutamuandikia mkuu wa jeshi rais Yoweri Kaguta Museveni ili atupe ruhusa twende tumsaidie huyu mheshimiwa Robert Kyagulanyi’ amesema Ebuku.

Hapo jana mtu mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi na wengine watano kupata majeraha wakati polisi ilipokuwa ikizima maandamano ya wakaazi wa Manispaa ya Mityana magharibi mwa Kampala.

Vurugu hizo ziliibuka baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa mbunge wa upinzani Francis Zaake amekufa baada ya kupigwa na maafisa wa usalama anakoshikiliwa yeye na wenzake.

Waganda walioko nje wameendelea kutuma ujumbe wa kuishtumu serikali kwa vitendo vyake vya kuwanyanyasa wanasiasa wa upinzani na raia kwenye mitandao ya kijamii.

Katika mji wa Toronto nchini Canada maandamano makubwa yalifanyika kwenye barabara za mji huo siku ya Jumamosi huku raia wengine nao walituma kanda binafsi za video kutoka Afrika Kusini na Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *