Asa Mwaipopo na wakuu wa kampuni ya madini washtakiwa kwa uhalifu wa kiuchumi

Asa Mwaipopo na wakuu wa kampuni ya madini washtakiwa kwa uhalifu wa kiuchumi

Like
893
0
Wednesday, 24 October 2018
Local News

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya uchimbaji madini Tanzania Acacia Mining, Asa Mwaipopo amefikishwa mahakamani hii leo kwa mashtaka ya uhalifu wa kiuchumi.

Mwaipopo mwenye umri wa miaka 55 alikamatwa hapo jana mjini Dar es salaam.

Anajiunga na wengine sita ambao wanazuiwa tangu wiki iliyopita kwa makosa hayo akiwemo Deogratias Mwanyika aliyekuwa makamu wa rais wa kampuni ya Barrick Gold na mkurugenzi wa mawasiliano wa kampuni ya Bulyanhulu mine, na Alex lugendo mwenye umri wa miaka 41 ambao tayari wako rumande.

Wanakabiliwa na mashtaka yakiwemo biashara haramu ya fedha, udanganyifu, na ukwepaji kulipa kodi.

Mwaipopo alifikishwa mbele ya mahakama ya hakimu mkaazi ya Kisutu hii leo ambapo alishtakiwa kwa kupanga njama na maafisa wengine ndani na nje ya Tanzania na kughushi nyaraka kukwepa kulipa kodi.

Acacia imekuwa katika mgogoro na serikali ya Tanzania, tangu serikali izuie usafirishwaji wa makinikia ya kampuni hiyo nje ya nchi.

Serikali ya Tanzania pia imekuwa ikiishutumu kampuni ya Acacia kwa kukwepa kulipa kodi inayostahili, tuhuma ambazo kampuni hiyo mpaka sasa imekuwa ikizikanusha.

Rais John Magufuli na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, Prof John Thornton katika mkutano wa nyuma

Kwa mujibu wa Reuters, Acacia Mining ilithibitisha siku ya Jumatano wiki iliyopita kwamba mfanyakazi wao na aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni hiyo, walizuiliwa na taasisi ya kupambana rushwa Tanzania, ikiwa ni wiki moja baada ya kampuni hiyo kusema mfanyakazi mwingine ameachiwa kwa dhamana baada ya kushtakiwa kwa rushwa.

Acacia, ambayo ni kampuni kubwa ya uchimbaji madini Tanzania imekuwa katika mzozo wa muda mrefu na serikali ambayo inaituhumu kampuni hiyo kwa kukwepa kulipa kodi. Acacia imekana kufanya makosa yoyote.

Kampuni hiyo inamilikiwa na kampuni iliyopo Canada Barrick Gold.

Mvutano wa Acacia Mining na serikali ?

Serikali ya imeishutumu Acacia kwa kufanya kazi ya uchimbaji nchini Tanzania kinyume cha sheria na kusema kuwa makampuni ya uchimbaji madini yamekuwa yakikwepa kulipa kodi.

Kutokana na tuhuma hizo kutoka kwa serikali, thamani ya hisa za kampuni ya Acacia ilishuka.

Uchunguzi ulioamriwa kufanyika mwezi Machi mwaka jana ulibaini kuwa Kampuni ya uchimbaji Acacia imekuwa ikifanya kazi kinyume cha sheria.

Mwenyekiti wa kamati ya wachumi na wanasheria Nehemiah Osoro iliyofanya uchunguzi huo alieleza.

Kamati ilifanya uchunguzi kuhusu usafirishaji wa madini kwa kipindi cha miaka 19.

Hisa za Kampuni ya Acacia ambayo inamilikiwa na Barrick Gold Corparation zilianguka kwa kiasi cha asilimia 15.

Acacia imejitetea kuwa inafanya biashara zake kwa viwango vya juu na inafanya kazi kwa kufuata sheria za Tanzania ikiwemo kulipa kodi zote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *