Abdul Nondo ashinda kesi ya ‘kujiteka’

Abdul Nondo ashinda kesi ya ‘kujiteka’

Like
841
0
Monday, 05 November 2018
Local News

Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imemuachia huru Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi  (TSNP), Abdul Nondo.

Nondo ameshinda kesi aliyofunguliwa na upande wa jamuhuri toka mwezi Machi mwaka huu.

Katika kesi hiyo, Nondo alikuwa anakabiliwa na mashtaka mawili, la kwanza kutoa taarifa ya uongo kwa ofisa wa polisi wa kituo Mafinga akidai alitekwa na watu wasiojulikana.

Katika shtaka la pili, Nondo alidaiwa kutoa taarifa za uongo mtandaoni kuwa yupo katika hatari.

Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu Liad Chamchama na Nondo aliwasilisha utetezi wake Septemba 18 na 19.

Akizungumza na BBC wakili wa Nondo Jebra Kambole amesema upande wa utetezi wamepokea hukumu hiyo kwa mikono miwili na kuishukuru mahakama kwa kusimama katika haki.

“Mahakama imetenda haki katika kipindi hiki kigumu sana, hili limetufanya kuendelea kuwa na Imani thabiti juu ya taasisi ya mahakama,” amesema Jebra.

Nondo ambaye ni mwanafunzi wa Sayansi ya Siasa na Utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisimamishwa masomo toka alipofunguliwa kesi hiyo, huku uongozi wa chuo ukisema angeendelea na masomo baada ya kumalizika kwa kesi yake.

“Tunashukuru kesi imeisha kwa ushindi kwetu, sasa mwananfunzi (Nondo) arejee shule amalize masomo yake,” amesema Jebra.

Hakimu Chamchama katika maelezo yake amesema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha pasi na shaka tuhuma zilizokuwa zinamkabili Nondo.

Mwezi Machi mwaka huu, Nondo ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali juu ya maslahi ya wanafunzi alituma ujumbe mfupi kwa watu wake wa karibu akisema kuwa yupo hatarini.

Baada ya kutoweka, uongozi wa TSNP ikatoa taaaarifa ya chama hicho cha wanafunzi inasema Bw Nondo amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana.

Wakati mmoja, anadaiwa kukamatwa na askari wa jeshi la polisi eneo la Milimani City na kutuhumiwa kwamba “analeta uchochezi wa baadhi ya wanafunzi waliokosa mikopo ya elimu ya juu kuandamana.”

“Mara kadhaa kumekwua na makundi ya watu asiowatambua na wenye nguo za kiraia wakijitambulisha kama watu wa usalama ambao wamekuwa wakimfuatilia na kumpa vitisho hivyo,” taarifa hiyo ilisema.

Baada ya siku moja alipatikana akiwa hajitambui wilayani Mafinga mkoani Iringa na kudai kuwa alitekwa na kutelekezwa na watu wasiojulikana.

Hata hivyo, madai hao yalipingwa vikali na polisi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo Mwigulu Nchemba amabye alidai mwanafunzi huyo “alijiteka”. Baada ya kushikiliwa kwa siku kadhaa mjini Iringa na jijini Dar es Salaam, hatimaye alifunguliwa mashtaka ambayo ameyashinda hii leo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *