Marekani imesema italegeza masharti ya vikwazo dhidi ya Iran kwa nchi nane huku waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiisifu hatua ya Marekani na kulitaja tukio hilo kuwa la kihistoria.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ameziorodhesha China, India, Italia, Ugiriki, Japan, Korea Kusini, Taiwan na Uturuki kuwa nchi ambazo zitapewa ahueni ya muda ya kuagiza mafuta ya Iran na kuepuka kuadhibiwa kwa kukiuka vikwazo vilivyowekewa nchi hiyo. Pompeo amesema Marekani haitachoka kuishinikiza Iran.
Maafisa wa Iran wamesema hawatiwi wasiwasi na vikwazo ambavyo vimeanza kutekelezwa leo na kuapa kuvikiuka.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameitaja leo kuwa siku ya kihistoria kufuatia hatua hiyo ya Marekani ya kuiwekea Iran ambaye ni hasimu wa tangu jadi wa Israel vikwazo akiongeza kuwa, vikwazo hivyo vitaifanya Iran kupunguza ubabe katika kanda ya Mashariki ya Kati.
Vikwazo hivyo vinanuia kupunguza kwa kiasi kikubwa uuzaji wa mafuta ya Iran, biashara ambayo tayari imeshaathirika kwani nchi hiyo imepunguza uuzaji wa karibu mapipa milioni moja ya mafuta tangu mwezi Mei na hivyo kuathiri uchumi wake.
Hatua hiyo ya Marekani inayotajwa na utawala wa Rais Donald Trump kuwa vikwazo vikali zaidi dhidi ya Iran inafuatia uamuzi wa Marekani mwezi Mei mwaka huu kujiondoa kutoka makubaliano ya kimataifa kuhusu mpango wa kinyuklia.
Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert amesema nchi yake inaamini inaweza kuendelea kudumisha mahusiano ya kibiashara na Iran na inaangalia namna ya kuzilinda kampuni ambazo zimeathirika na kuanza kutekelezwa kwa vikwazo hivyo ambavyo Marekani inaamini vitaizuia Iran kutengeza silaha za kinyuklia na kupunguza ushawishi wake katika kanda ya Mashariki ya Kati.
Vikwazo hivyo vinaathirii benki 50 na asasi nyingine za kifedha, zaidi ya watu 200, vyombo vya usafiri wa majini na shirika la ndege.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif amesema kitendo cha Marekani ni cha uchokozi na ni vita vya kiuchumi lakini amesisitiza havifanikiwa. Umoja wa Ulaya umesema unaendelea kuunga mkono makubaliano ya kinyuklia yaliyofikiwa kati ya nchi zenye nguvu duniani na Iran na wanapinga kurejeshwa kwa vikwazo dhidi ya taifa hilo, msimamo ambao pia unapingwa na China. Iran kwa upande wake imesema kwa hatua hiyo ya Marekani hakuna jipya, kwani vikwazo vyake tayari vimekuwepo.