Mgawanyiko wazuka ndani ya upinzani nchini DRC

Mgawanyiko wazuka ndani ya upinzani nchini DRC

Like
518
0
Tuesday, 13 November 2018
Global News

Vigogo wa vyama vikuu, kikiwemo kile cha UDPS, wametupilia mbali chaguo la viongozi wao hapo jana mjini Geneva, Uswisi, huku wafuasi wa vyama hivyo wakielezea huzuni yao kuhusu uteuzi wa Martin Fayulu.

Upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umegawanyika baada ya kuteuliwa kwa Martin Fayulu kuwa mgombea pekee wa urais kwenye uchaguzi ujao wa Desemba 23. Vigogo wa vyama vikuu, kikiwemo kile cha UDPS, wametupilia mbali chaguo la viongozi wao hapo jana mjini Geneva, Uswisi, huku wafuasi wa vyama hivyo wakielezea huzuni yao kuhusu uteuzi huo, licha ya mashirika ya kiraia kuipongeza hatua ya upinzani ya kuweka mgombea mmoja kwenye uchaguzi wa rais.

Kwenye makao makuu ya chama cha UDPS mtaani Limete, DW iliwakuta wafuasi hawa wakijadili uteuzi huo wa Martin Fayulu kuwa mgombea wa upinzani. Taarifa hiyo imezusha mshangao kuona kwamba kiongozi wao Felix Tshisekedi hakuteuliwa kuwa mgombea pekee wa upinzani. Jean –Yves Kamale, mfuasi wa chama cha UDPS amesema ni vigumu kuamini walichofikia viongozi saba wa upinzani huko Geneva. Ameendelea kusema:

“Nimehuzunishwa sana, nimehuzunishwa sana kuona kwamba Kamerhe, Bemba, Matungulu, Felix, Katumbi na Muzito kuteuwa Martin Fayulu kuwa mgombea wetu… nini Fayulu anaweza kuchangia kwenye upinzani? Hana ngome yyote…Ukienda kwenye jimbo jirani la Kongo-Central nani anamjuwa Fayulu?”

Vigogo wa UDPS wapinga uteuzi wa Fayulu

Vigogo wa chama cha UDPS waliobaki hapa mjini Kinshasa pia wametupilia mbali uteuzi wa Fayulu. Huku akiahidi mkutano wa chama baadaye leo, naibu katibu mkuu wa chama hicho, Augustin Kabuya, amesema kwamba chaguo hilo haliwezi kukubalika hata kidogo na wafuasi wao.

Kwenye chama cha kingine cha upinzani cha UNC cha Vital Kamerhe tafauti imezuka baina ya viongozi wake.

Msemaji wa chama hicho hicho, Jolino Makelele, amepongeza uteuzi wa mgombea mmoja, lakini mkuu wa tawi la vijana, Billy Kambale, amesema kwa vyovyote vile Kamerhe atagombea kiti cha urais.

Lambert Mende, msemaji wa mgombea wa chama tawala Ramazani Shadary alikataa kutoa maoni yake kuhusu uteuzi huo, lakini ameiambia DW kwamba wapigaji kura ndio watakaotoa uamzi wa mwisho kwa wagombea.

Mashirika ya kiraia yapongeza suala la upinzani kuwa na mgombea mmoja

Hata hivyo, baadhi ya mashirika ya kiraia nchini yamepongeza uteuzi huo wa mgombea mmoja wa upinzani. Kiongozi wa shirika la haki za bindamu ACCES A LA JUSTICE, Georges Kapiamba, amesema kwamba upinzani umefikia hatua ya kistoria.

“Ni habari nzuri kwa sababu upinzani umeonesha kwamba unaweza kukubaliana na kuteuwa mgombea mmoja. Tunaipongeza hatua hiyo ya viongozi wa upinzani inayoonesha kukomaa kwao kisiasa.”

Martin Fayulu mwenye umri wa miaka 62 alijiunga na siasa mwaka 2006 alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Kinshasa, na baadaye kachaguliwa mbunge wa taifa mwaka 2011. Kabla ya hapo, Fayulu alikuwa mfanyabiashara. Fayulu ni miongoni mwa wapinzani waliokuwa mstari wa mbele kupinga kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais mwaka 2016.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *