Viongozi wa nchi 20 zilizoendelea zaidi kiuchumi wataanza mkutano wa kilele leo mjini Buenos Aires, Argentina, ambao unatarajiwa kugubikwa na mivutano ya kibiashara, pamoja na mzozo mpya kati ya Urusi na Ukraine.
Rais wa Marekani Donald Trump ni miongoni mwa viongozi ambao tayari wametua mjini Buenos Aires, baada ya kufuta mkutano wake na Rais wa Urusi Vladimir Putin, kutokana mzozo mpya kati ya Urusi na Ukraine katika bahari ya Azov. Kuwepo kwa Trump katika mkutano huo kunapokelewa kwa maoni mchanganyiko, kutokana na sera yake ya Marekani kwanza ambayo imeiweka biashara huria duniani katika hali tete.
Kinachosubiriwa kwa shauku ni mkutano kati ya Trump na rais wa China Xi Jinping, ambao unatazamiwa kutuliza au kuzidisha wasiwasi wa kibiashara. Nchi hizo zinazoogoza kiuchumi duniani zimekuwa na mvutano, na kuwekeana na vikwazo vya kiushuru ambavyo vimeathiri sehemu nyingi za dunia.
Trump asema hataki makubaliano na China
Kabla ya kuanza safari yake, Trump alizungumzia uwezekano wa kupata makubaliano ya China, akisisitiza hata hivyo kwamba hana haraka yoyote, kwa sababu Marekani inanufaika na vikwazo ilivyoiwekea China.
”Nadhani tunakaribia kupiga hatua na China, lakini sijui kama nataka kufika hapo, kwa sababu sasa hivi Marekani inaingiza mabilioni na mabilioni yatokanayo na ushuru na kodi, kwa hiyo, kusema kweli sijui. Lakini nawaambia, nadhani China wanataka sana kupata makubaliano, na niko wazi kwa makubaliano, lakini kusema kweli napendezwa na hali inavyoendelea.”
Safari ya Trump kutoka Washington hadi Buenos Aires imeandamana na kiwingu cha kisiasa, kufuatia hatua ya aliyekuwa mwanasheria wake binafsi Michael Cohen kukiri mahakamani, kwamba alilidanganya bunge kuhusu mipango ya kibiashara ya kampuni ya Trump nchini Urusi.
Suali linaloulizwa na wengi ni ikiwa Trump atakutana na Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman, anayeshukiwa kuhusika katika mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi.
Ndege ya Merkel yapata hitilafu
Wakati viongozi wengine wangi wakiwa tayari wamewasili nchini Argentina, wakiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza na Rais wa Ufaransa, Kansela wan Ujerumani Angela Merkel yumkini atakosa sherehe za ufunguzi wa mkutano huo muhimu, kwa sababu ndege yake, Airbus ”Konrad Adenauer” ililazimika kukatisha safari hapo jana ikiwa juu ya anga ya Uholanzi na kutua kwenye uwanja wa Cologne na Bonn, baada ya marubani wa ndege hiyo kubaini hitilafu katika mfumo wa mawasiliano.
Hata hivyo, gazeti la Bild la hapa Ujerumani limewanukuu marubani wa ndege hiyo, wakisema haikuwa katika kitisho chochote cha usalama. Lakini, gazeti jingine la Rheinische Post limeripoti kuwa wachunguzi wataangalia pia uwezekano wa sababu za kihalifu katika masaibu yaliyoikumba ndege hiyo.