Afrika Kusini imeghadhabishwa na mtandao wa Rwanda uliomuita waziri wake “kahaba”

Afrika Kusini imeghadhabishwa na mtandao wa Rwanda uliomuita waziri wake “kahaba”

Like
648
0
Tuesday, 11 December 2018
Global News

Afrika Kusini imemuita balozi wa Rwanda mjini Pretoria baada ya mtandao unaoipendelea serikali nchini Rwanda kumita “kahaba” waziri mmoja wa serikali ya Afrika Kusini.

Lindiwe Sisulu, waziri wa masuala ya uhusiano wa kimataifa nchini Afrika Kusini amekosolewa kwenye Twitter na afisa wa cheo cha juu wa Rwanda.

Msemaji wake aliiambia BBC kuwa matamshi hayo hayatakubaliwa na lazima yakome.

Bi Sisulu hivi majuzi alikutana na mtoro na mkosoaji wa Rais wa Rwanda, na kuzua mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Aliuambia mkutano wa wandishi wa habari mwezi ulipita kuwa alikutana na mkuu wa zamani wa majeshi nchini Rwanda Faustin Kayumba Nyamwasa, mjini Johannesburg.

Alisema alishangazwa kusikia kuwa Bw Nyamwasa ambaye amebuni chama chake nchini Afrika Kusini alikuwa na nia ya kuzungumzia mapatano na serikali yake ya zamani.

Bwana Nyamwasa amekuwa akiishi uhamishoni nchini Afrika Kusini tangu mwaka 2010 baada ya kutofautiana na rais wa Rwanda Paul Kagame.

Naibu waziri wa nchi za kigeni nchini Rwanda Olivier Nduhungirehe, alikosoa mkutano huo kwenye mtandao wa Twitter.

Alisema ikiwa afisa yeyote wa Afrika Kusini anataka kuzungumza na mhalifu ambaye alikuwa anaongoza vuguvugu yuko huru kufanya hivyo lakini kamwe asiishirikishe Rwanda.

Taarifa moja kwenye mtando wa habari unaoipendelea serikali ilikuwa na kichwa kilichomtaja Bi Sisulu kama “kahaba”.

Msemaji wa Bi Sisulu, Ndivhuwo Mabaya, alisema balozi wa Rwanda huko Pretoria ameambiwa kuwa matamshi kama hayo hayatakubaliwa.

Alisema balozi wa Afrika Kusini mjini Kigali, George Twala, ameitwa kwenda Prerotia kwa mashauriano.

Shambulizi la bunduki

Mwaka 2014 Afrika Kusini iliwafukuza wanadiplomasia watatu wa Rwanda kufuatia shambulizi dhidi ya nyumba ya Bw Nyamwasa mjini Johannesburg. Rwanda ilijiubu kwa kuwatimua wanadiplomasia 6 wa Afrika Kusini.

Bw Nyamwasa alinusurika karibu mara mbili jaribio la kuuawa akiwa uhamishoni.

Wanaume wanne walikutwa na hatia mwaka 2014 na mahakama ya Afrika Kusini kwa shambulizi hilo la bunduki lililomuacha na majeraha ya tumbo. Bw Nyamawasa alilitaja shambulizi hilo kuwa lilichochewa kisiasa.

Uhusiano kati ya Afrika Kusini na Rwanda pia ulidhoofika baada ya aliyekuwa mkuu wa ujasusi kanali Patrick Karegeya, kuuawa katika hoteli yake mjini Johannesburg mwaka 2014.

Muda mfupi baada ya kuuliwa, Bw Kagame alisema: “Huwezi kuhujumu Rwanda na hukose kuadhibiwa. Yeyote hata wale ambao bado wako hai watavuna. Kila mtu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *