Adhabu iliyotangazwa kwa watakaokamatwa wametupa takataka hovyo Jijini Dodoma

Adhabu iliyotangazwa kwa watakaokamatwa wametupa takataka hovyo Jijini Dodoma

Like
777
0
Monday, 30 April 2018
Local News

Siku tatu baada ya Rais Dkt Magufuli kuipandisha hadhi Manispaa ya Dodoma kuwa Jiji, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amesema kuwa, mtu yeyote atakayekamatwa akitupa takataka hovyo, atakamatwa na kutozwa faini ya TZS 50 milioni, ikiwa ni kwa mujibu wa sheria ndogo za usafi.

Mkurugenzi Kunambi ameyasema hayo jana Aprili 29 wakati akizungumza na wafanya usafi ndani ya jiji hilo ambapo alizundua mchakato wa kuwapati kadi za matibabu (bima za afya) ambazo wataweza kuzitumia wao na wategemezi wao wanne. Katika mkutano huo, alitoa kadi 10 kama kuonesha kuanza kwa mchakato huo.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Binilith Satano Mahenge alisema kuwa, baada ya Rais Dkt Magufuli kupandisha hadhi manispaa hiyo, zawadi ya kwanza watakayotoa kwake, ni kuhakikisha kuwa jiji hilo linakuwa safi muda wote. Amesema jiji hilo lazima liwe mfano kutokana na shughuli zinazofanyika hapo, na watu wengine waje kujifunza kutoka kwao.

Katika hatua za wali, RC Mahenge ametoa fedha TZS 1 milioni kwa ajili ya kununulia vifaa vya usafi na kuagiza pia kuwekwe sehemu za kutupia takataka ili wale watakaokamatwa wakiwa wametupa takataka wasipate utetezi wa kusema, hakukuwa na eneo maalumu la kuweka takataka zao.

Pia, amemuagiza mkurugenzi wa jiji hilo, kuwatumia Askari Mgambo ili kuhakikisha kuwa wanawakamata wale wote wanaotupa taka hovyo kuanzia Mei 20 mwaka huu, na kuwatoza faini kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs), na wafanye hivyo bila kumuonea mtu haya.

Amesema, mtu akikamatwa kwa mara ya kwanza na mara ya pili atatozwa faini, lakini akikamatwa kwa mara ya tatu, watatoa jina au majina yao kwenye magazeti kuonesha wao ndio wanaongoza kwa uchafuzi wa jiji.

Katika hatua nyingine, RC Mahenge amempongeza mkurugenzi kufuatia mchakato huo wa kutoa bima za afya kwa wafanya usafi, na kusema kwamba, kutokana na mazingira wanayofanyia kazi, zitakuwa msaada mkubwa sana kwao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *