Timu Ya Arsenal ya nchini Uingereza jana usiku iliweza kufuzu kucheza mashindano ya kombe la UEFA kwa msimu wa 17 mfululizo kwa timu za Ulaya baada ya kuichapa timu ya Besiktas ya Uturuki kwa bao 1-0.
Katika mchezo wa awali wiki mbili zilizopita timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana na hivyo kusubiri uamuzi wa nani atavuka katika mechi ya pili ya marudiano ambayo ilichezwa jana usiku. Alikuwa ni mchezaji mpya wa timu ya Arsenal aliyejiunga msumu huu akitokea timu ya FC Barcelona Alex Sanchez, ambaye ndiye aliyeiwezesha Arsenal kusonga mbele baada ya kuipatia timu yake bao hilo pekee la ushindi kwa timu yake katika dakika ya 46 ya kipindi cha kwanza.
Arsenal ilipata nafasi ya kumaliza mchezo huo mapema lakini washambuliaji wake Santi Cazorla na Alex Chamberlain walipoteza nafasi nyingi za wazi walizopata.
Timu ya Arsenal ilipata pigo la kupungukiwa na mchezaji mmoja uwanjani, zikiwa zimesalia dakika 15 kabla ya kumalizika kwa mchezo, baada ya mchezaji wake Mathieu De Buchy kutolewa nje ya mchezo kwa kadi mbili za njano na kufanikiwa kupambana wakilinda ushindi wao kiduchu hadi mwisho wa mchezo.
Timu nyingine zilizofuzu pamoja na Arsenal katika kinyang’anyiro cha kufuzu jana usiku ni pamoja na Atletico Bilbao 3-1 dhidi ya Napoli, Bayer 04 Leverkusen 4-0 dhidi ya FC Copenhagen, Ludogorets Razgrad 1-0 dhidi ya Steau Bucharest na Malmo FF – 3-0 dhidi ya Fc Red Bull Salzburg.