IMEELEZWA kuwa asillimia 70 ya wagonjwa wa saratani hupoteza maisha katika nchi zinazoendelea na katika Bara la Afrika lenye watu zaidi ya milioni 804 asilimia 12.4 wanapata saratani kabla ya kufikia umri wa miaka 75 na asilimia 90 wanapata ugonjwa huo wakiwa na umri chini ya miaka 40.
Hayo yamesemwa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta wakati akifungua mkutano wa tisa wa Jukwaa la wake wa marais wa Afrika la kutokomeza magonjwa ya saratani za mfumo wa uzazi ambazo ni mlango wa kizazi, matiti na tezi dume unaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa-KICC– mjini Nairobi.
Rais Kenyatta amesema Ripoti ya saratani iliyotolewa mwaka 2014 na Shirika la Kimataifa la kutafiti ugonjwa huo kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani –WHO– ilionesha kuwa takwimu mpya za saratani zinaongezeka kila mwaka na kwa upande wa Afrika vifo vingi vinatokana na saratani ya mlango wa kizazi.