Shamima Begum, aliyejiunga na kundi la wapiganaji wa Islamic State nchini Syria akiwa na miaka 15, atapoteza uraia wake Uingereza.
Duru kutoka serikalini zilisema inawezekana kumvua uraia msichana huyo mwenye umri wa miaka 19 raia wa Uingereza kwasababu ana nafasi ya kupata uraia wa nchi nyingine.
Wakili wa familia yake, kwa uamuzi huo na wanatathmini ‘njia zote kisheria’ kukabiliana na hatua hiyo.
Begum, aliyeondoka London mnamo 2015, alisema anataka kurudi nyumbani.
Alipatikana katika kambi ya wakimbizi nchini Syria wiki iliyopita baada ya kuondoka Baghuz, inaarifiwa – ngome ya wapiganaji wa IS – na kwamba alijifungua mtoto wa kiume mwishoni mwa juma.
Katika mahojiano na BBC Jumatatu, Begum amesema hakutaka kuwa ‘sura ya wasichana’ wa IS na kwamba anachotaka sasa ni kumlea mtoto wake kwa umakini nchini Uingereza.
Inaaminika ana asili ya Bangladeshi lakini alipoulizwa na BBC, ameeleza kwamba hana pasipoti ya Bangladesh na kwamba hajawahi kwenda katika nchi hiyo.
Lakini vipi kuhusu mwanawe aliyemzaa? mtoto aliyezaliwa na mzazi aliye na uraia wa Uingereza kabla ya kupokonywa uraia, bado anatizamwa kuwa raia wa Uingereza.
Wakati inawezekana kimsingi kumpokonya mtoto uraia , maafisa watahitaji kupima sawa haki zao dhidi ya tishio walilonalo.
Islamic State limepoteza sehemu kubwa ya maeneo ambayo yalidhibiti , lakini kati ya wapiganaji 1000 na 1500 inaaminika wamesalia katika eneo la kilomita 50 kwa mraba karibu na mpaka wa Syria na Iraq.