Rais Dkt. John Pombe Magufuli akutana na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia kanda ya Afrika Dkt. Hafez Ghanem ambaye ametangaza kuwa Benki ya Dunia imeridhia kutoa Dola za Marekani milioni 300 kwa ajili ya mradi wa kuongeza ubora wa elimu ya Sekondari.
Katika Mazungumzo hayo:
Benki ya Dunia imeridhia kutoa Dola za Marekani Milioni 300 sawa na shilingi Bilioni 680.5 kwa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuongeza ubora wa elimu ya sekondari unaokusudiwa kujenga vyumba vya madarasa, mabweni, maabara, nyumba za watumishi na kununua vifaa vya kufundishia.
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Hafez Ghanem aliyekutana na Mhe. Rais Magufuli tarehe 16 Novemba, 2018 Ikulu Jijini Dar es Salaam amesema pamoja na kuridhia kutoa fedha za mradi huo, Benki hiyo inaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 5.2 sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 13 na kwamba miradi hiyo inatekelezwa kutokana na uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania.
Dkt. Hafez Ghanem amesema katika mazungumzo hayo wamejadili juu ya maendeleo ya miradi hiyo na kazi nzuri ambayo inafanywa na Tanzania kuimarisha uchumi, na pia amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa matokeo mazuri ya mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha huduma za kijamii.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano na uhusiano mzuri na Tanzania na ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kukuza uhusiano huo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika kwa miradi iliyokusudiwa.
“Namshukuru Dkt. Hafez Ghanem na Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Tanzania, hizo Dola Milioni 300 ambazo baadhi ya watu wasiotutakia mema walisema zimefyekelewa mbali, anasema zitaletwa, na pia Benki ya Dunia imetoa Dola Bilioni 5.2 ambazo zinafadhili miradi mbalimbali ya elimu, nishati, barabara, kilimo, afya na maji, ni miradi mikubwa na mingi.
“Kwa hiyo amekuja kututhibitishia kuwa Benki ya Dunia haitatuacha” amesema Mhe. Rais Magufuli.
cc;Ikulu