Biashara ya kubadili fedha za kigeni kudhibitiwa

Biashara ya kubadili fedha za kigeni kudhibitiwa

Like
1671
0
Monday, 10 December 2018
Local News

Mamlaka nchini zimeazimia kuendeleza kampeni ya kudhibiti biashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni nchini ili “kuzuia kuyumba kwa sekta ya fedha”.

Mwezi uliopita, Benki kuu (BoT) iliyafunga zaidi ya maduka 100 ya kubadili fedha jijini Arusha kwa kutokukidhi masharti ikiwemo kutokuwa na leseni halali za biashara.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Gavana wa BoT Profesa Florens Luoga amesema operesheni hiyo haitakoma, na huenda mji mkuu wa kibiashara Dar es Salaam ukafuata baada ya Arusha.

“Hatuhitaji maduka 100 ya kubadilisha fedha Dar es Salaam, kwani kuna benki za kutosha. Tunahitaji maduka ya fedha kwenye sehemu muhimu kama kwenye mahoteli ya kitalii na mipakani,” amesema Luoga kwenye mkutano wa Rais John Magufuli na Wakuu wa Mikoa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na viongozi wengine waandamizi wa serikali.

“Udhibiti utaendelea kuwa mkali. Hii ni moja ya hatua zitakazoendelea, kanuni ambazo zilikuwepo ziliongeza udanganyifu na maduka yakazidi kuongezeka kiholela,” ameongeza Luoga.

Katika operesheni iliyofanyika Arusha mwezi uliopita BoT ilitumia askari kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kutumika kwa askari wa JWTZ kwenye msako huo kulishtua watu wengi na ikamlazimu Luoga kutoa ufafanuzi baadaye.

Kwa mujibu wa Luoga BoT ilitumia wanajeshi “kufuatia askari wengi wa Jeshi la Polisi kuwa katika usimamizi wa mitihani ya kidato cha pili,” na taasisi yake ilihusisha askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wasio na silaha ili kuongeza nguvu katika kufanikisha zoezi hilo.

Kabla ya operesheni hiyo ya kushtukiza, kulishafanyika operesheni nyengine mbili za awali na maofisa wa BoT ambazo hazikuzaa matunda.

Wakati msako wa Arusha ukifanyika, thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani ilikuwa imeshuka maradufu na kufikia Sh2,300 kwa dola moja. Mara ya mwisho kwa kiwango hicho kufikiwa ilikuwa Julai 2015 na BoT ililazimika kuchukua hatua mahususi kukabiliana na anguko hilo.

Kwa mujibu wa tovuti ya BoT dola moja ya Marekani kwa hii leo Sesemba kumi imekuwa ikibadilishwa kwa shilingi 2,290.

Wiki mbili zilizopita, BoT ilizipiga marufuku benki tano kuendesha biashara ya sarafu za kigeni kwa muda wa mwezi mmoja kwa kukiuka sharia.

Benki ya Barclays Tanzania, Exim Bank, UBA Bank, BancABC na Azania Bank zote zilipigwa marufuku ya kuendesha biashara hiyo Novemba 23 kwa kukiuka sheria za biashara, kwa mujibu wa Alexander Ng’winamila, mkurugenzi wa masoko ya fedha katika benki kuu.

“Benki zilizopigwa marufuku aidha zilifanya biashara nje ya viwango vya masoko au hazikuwasilisha kwa Benki Kuu rrekodi za biashara zao, suala ambalo ni kinyume na sheria,” Ng’winamila aliliambia shirika la Reuters.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *