WAFADHILI wa Kimataifa wameanza mkutano wao leo mjini Berlin, Ujerumani, unaolenga kukusanya dola bilioni 10 kwa ajili ya Mfuko wa Mabadiliko ya Tabia Nchi, ambapo Mataifa 22 duniani yanatazamiwa kuhudhuria mkutano huo.
Lengo la mfuko ulioanzishwa na Umoja wa Mataifa ni kuzisadia nchi masikini ili kupunguza utoaji wa hewa chafu na kujitayarisha na athari za kupanda kwa joto ulimwenguni.
Mkuu wa Kitengo cha Mabadiliko ya Tabia Nchi cha Umoja wa Mataifa, Christiana Figueres, ametoa wito kwamba angalau mtaji wa dola bilioni 10 uwe umeshapatikana kufikia mwishoni mwa mwaka huu kwa ajili ya mfuko huo.