BODI YA LIGI MSITIKISE MASIKIO KAMA MSIMU ULIOPITA,KOMAENI NA MIUNDOMBINU YA VIWANJA KABLA YA LIGI KUANZA

BODI YA LIGI MSITIKISE MASIKIO KAMA MSIMU ULIOPITA,KOMAENI NA MIUNDOMBINU YA VIWANJA KABLA YA LIGI KUANZA

Like
234
0
Monday, 03 August 2015
Slider

Na Omary Katanga

Michuano ya ligi kuu bara inataraji kuanza kutimua vumbi septemba 12 kwa msimu wa mwaka 2015/2016,na safari hii ikishirikisha jumla ya timu 16 zikiwemo 4 zilizopanda daraja kutoka ligi daraja la kwanza.

Timu hizo 4 ni pamoja na African Sports ya Tanga,Majimaji ya Songea,Mwadui FC ya Shinyanga na Toto Africans ya Mwanza, zinazotarajiwa kuonesha ushindani mkubwa kama ilivyokuwa kwa Mbeya City msimu wa mwaka 2013/2014.

Ongezeko hilo la timu linaongeza pia idadi ya mechi zitakazochezwa kwa msimu mzima na kupelekea viwanja kutumika kwa muda mwingi,kwahiyo kama havitakuwa madhubuti katika matayarisho yake basi tujiandae kushuhudia mabadiliko ya mara kwa mara ya ratiba kutokana na ubovu wa viwanja.

Mpaka sasa viwanja vinavyoonekana kuwa na angalau na bora wa kuridhisha kiasi,ni pamoja na Mwadui Shinyanga ,Jamhuri Morogoro,CCM Kirumba Mwanza,Sokoine Mbeya na Nangwanda Sijaona Mtwara,achilia mbali viwanja vya Taifa na Azam Complex vyenye ubora wa hali ya juu.

Kwa wakati huu ambapo vilabu vinajitayarisha kuanza kivumbi hicho,upande wa bodi ya ligi nao unatakiwa kuharakisha ukaguzi wa viwanja mbalimbali vitakavyotumika,ili kuondoa malalamiko kama yaliyojitokeza katika msimu uliopita.

 

Pamoja na miundombinu ya uwanjani,angalieni pia vyumba vya kubadilishia nguo vinavyoripotiwa wakati mwingine kupuliziwa dawa inayolegeza viungo vya wachezaji pamoja na kudhibiti vitendo vya kushirikina.

Mbali na bodi ya ligi kutilia mkazo katika uboreshwaji wa miundombinu ya viwanja, pia msisahau kuandaa waamuzi wenye uwezo wa kuchezesha kwa kufuata sheria zote 17 za soka na kanuni za ligi zilizowekwa ili kutenda haki kwa klabu.

Tumekuwa tukishuhudia na kusikia malalamiko ya mara kwa mara toka kwa viongozi,makocha na hata wachezaji kwamba mwamuzi Fulani amefanya vitendo vya kuudhi katika maamuzi yake,na kupelekea aidha mchezo kuvurugika au kukatiwa rufaa ambazo hata hivyo majibu yake hayainufaishi klabu iliyotendewa makosa.

Kwakuwa bodi ndiyo yenye dhamana ya kusimamia na kuendesha ligi,inapaswa pia kuchukua maamuzi magumu ya kuwafungia maisha waamuzi wa aina hiyo ambao wanaingia uwanjani wakiwa na matokeo mfukoni,na wakati mwingine wakijikuta wakichezea kichapo kutoka kwa wachezaji wenye hasira kali baada ya kufanya figisu figisu.

Nimalizie kwa kuzitakia maandalizi mazuri pamoja na usajili wenye kuzingatia weledi wa kiufundi klabu zote zitakazoshiriki ligi msimu huu,ili kuwepo na ushindani wa kweli na hatimaye tanzania iwe na timu imara ya taifa yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kusakata kabumbu.

Mwisho.

 

 

 

Comments are closed.