CHAMA cha Wananchi -CUF kimetishia kutofanyika kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa endapo Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa TAMISEMI haitabadilisha utaratibu waliouweka wa upigaji kura.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam Naibu Katibu Mkuu Bara Magdalena Sakaya amesema kuwa chama hicho hakitakubali kuona wagombea wao wanaenguliwa kulingana na mwongozo na kanuni za uchaguzi zilizopo ambazo tayari waliitaka TAMISEMI kuzirekebisha kwani zina mapungufu kwa wagombea na hata wapiga kura.
Sakaya amesema kuwa miongoni mwa mapungufu yaliyomo ni katika kifungu cha 9 na cha 10 cha fomu ya wagombea ambacho kinawataka kila mgombea kujaza nembo ya chama cha siasa na nembo ya halmashauri jambo ambalo amesema halieleweki katika utekelezaji wake.