CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA, kimesema ripoti za CAG ambazo zimeanika ufisadi katika maeneo yaliyokaguliwa ikiwemo Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, mashirika ya umma na miradi ya maendeleo, kwa mara nyingine zimedhihirisha wazi kile ambacho CHADEMA imekuwa ikisema kwa muda mrefu kwamba ufisadi huo unaoendelea kulitafuna taifa na kuwafanya Watanzania wazidi kuwa maskini.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na chama hicho kupitia kwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumaini Makene, Chadema kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ufisadi uliofanyika kwenye matumizi ya fedha za umma kama ilivyobainishwa kwenye ripoti za ukaguzi wa fedha kwa mwaka 2013/2014 zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali –CAG.