China imeionya Marekani kuwa iko tayari na ina uwezo wa kulinda maslahi yake, wakati ambapo mgogoro wa kibiashara ukifukuta kati ya nchi hizo mbili. Shirika la habari la China-Xinhua, limeripoti kuwa Naibu Waziri Mkuu wa China Liu He amempigia simu Waziri wa Fedha wa Marekani, Steven Mnuchin na kufikisha ujumbe huo. Liu pia amesema uchunguzi wa miezi saba uliofanywa na Marekani kuhusu shughuli za kibiashara za China, unakiuka sheria za kimataifa za biashara. Mazungumzo hayo ya simu kati ya Liu na Mnuchin yamefanyika baada ya wiki moja ya uhusiano wa kibiashara kati ya Marekani na China kukumbwa na wasiwasi mkubwa. Mnamo Alhamisi, Marekani ilitangaza mipango ya kuongeza kodi ya dola bilioni 60 kwa bidhaa za China kufuatia madai ya biashara isiyokuwa na usawa pamoja na wizi. China ililipiza kisasi kwa kutangaza ushuru wa dola bilioni 3 kwa bidhaa za Marekani.