Uchaguzi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) wa nafasi ya urais unatarajiwa kufanyika April 14, 2018, na wakili wa kujitegemea Fatma Karume amesema Jumamosi ana baraka zote za Rais wa chama hicho Tundu Lissu.
Tundu Lissu, ambaye ni mwanasheria na mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) muda wake wa uongozi utapomalizika.
Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimesema kuwa Lissu aliye kwenye matibabu nchini Ubelgiji, hatagombea tena baada ya kumaliza mwaka mmoja wa uongozi wake.
Kutokana na shambulizi la risasi Septemba 7 lililofanywa na watu wasiojulikana, mwaka jana, na kusababisha awe katika matibabu nje ya nchi kwa muda mrefu, Lissu atakuwa ametumikia nafasi yake kama Rais wa TLS kwa miezi sita pekee.
Fatma ambaye pia ni mtoto wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, ameliambia gazeti la Mtanzania kuwa mwanzoni hakuwa tayari kugombea urais wa TLS lakini baadaye akashawishiwa na mawakili vijana akakubali.
“Yalikuwa maamuzi magumu sana kwa sababu sikutaka kugombea, nilikuwa naombwa na vijana kwamba Fatma chukuwa fomu ugombee tutakuchagua nikasema hapana nina majukumu mengi.
“Nakumbuka ilipofika Alhamisi kuna kijana mmoja akanifuata akaniambia nakuomba uchukue fomu nikamwambia siko interested kwa sababu nilikuwa nataka nijipunguzie majukumu.
“Sasa baadaye nilivyojiuliza kujipunguzia huku majukumu ina maana nafikiria watu au mimi mwenyewe nikasema huu utakuwa ubinafsi…baada ya kutafakari nikamtumia message yule kijana kwamba achukue fomu ajaze na sehemu ya wadhamini halafu aniletee nisaini.