Fifa nayo yaishukia Gor Mahia

Fifa nayo yaishukia Gor Mahia

Like
394
0
Monday, 12 May 2014
Slider

NI taabu tupu kwenye ngome ya Gor Mahia kwani baada ya kuandamwa na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) kwa kutokulipa ushuru wa Sh118 milioni, sasa iko hatarini kufungiwa na Fifa kusajili wachezaji.

Kwa wiki chache zilizopita, mambo hayajawa mazuri kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Kenya ambao wamefilisika na kwa sasa wanawategemea mashabiki wao kutoa mchango ili kuwanusuru na janga la kifedha.

Huku hayo yakizidi kuwaumiza kichwa, Fifa ambalo ni shirikisho la kimataifa la vyama vya soka, imetishia kuwashushia rungu hilo baada ya klabu hiyo kukikuka kanuni katika kumsajili, Patrick Oboya, kutoka klabu ya Vietnamese.

Habari zilizopatikana zinasema shirikisho hilo limenusa mchezo mchafu unaodaiwa kufanywa Gor kutokufuata kanuni zinazotakiwa kumnunua mchezaji huyo na sasa limeitaka klabu hiyo kujieleza kinagaubaga jinsi gani walivyomsajili Oboya.

“Tunataka Gor Mahia itueleze kwa mapana na marefu ni utaratibu upi walioufuata hadi kumpata mchezaji huyo. Oboya amekuwa akishiriki mechi bila ya kuwa na cheti cha kimataifa cha uhamisho na hilo ni kosa kubwa,” taarifa kutoka Fifa imeeleza.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ambrose Rachier amekiri kupokea barua ya Fifa kuhusu usajili wa Oboya na amesema katika hatua za awali wamemwomba mchezaji huyo aketi pembeni kidogo mpaka mzozo huo utakapotatuliwa.

Ofisa Mkuu wa uhamisho wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa, naye amethibitisha nao kuwa na nakala ya barua hiyo, lakini analitetea shirikisho lisilaumiwe.

Kwa kawaida Fifa huwa inazifungia usajili klabu zinazofanya faulo katika suala hilo. Pia huenda Gor Mahia ikapokonywa pointi za mechi ambazo Oboya alicheza kama itathibitika kanuni zilikiukwa katika usajili wake.

Kabla ya kujiunga na Gor mwanzoni mwa msimu huu, Oboya alikuwa akiichezea Thanh Hoa inayoshiriki Ligi Kuu Vietnam ambako mkataba wake ulisitishwa. Alikwenda Vietnam akitokea Ligi ya Slovakia ambako aliichezea klabu ya MFK Ruzomberok.

source mwanaspoti

Comments are closed.