HOSPITALI za Mkoa wa Dar es Salaam zimebainika zilikuwa na wagonjwa wengi ambao walikufa kutokana na malaria, Ukimwi , ajali, maambukizi ya bakteria kwenye damu, upungufu wa damu, saratani na kifua kikuu(TB) ukifuatiwa na mkoa wa Morogoro.
Imefahamika malaria na upungufu wa damu ulichangia vifo vingi kwenye kundi la watoto chini ya miaka mitano na vifo kutokana na Ukimwi na Kifua Kikuu viliathiri zaidi kundi la watu wazima, vifo vinavyotokana na ajali viliathiri zaidi kundi kubwa la vijana wakati saratani ziliathiri makundi ya umri wote.
Hayo yameelezwa jana jijini Dar es Salaam na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu(NIMR) wakati ikielezea matokeo ya utafiti wa vifoo vinavyotokea katika hospitali za Tanzania. Imeelezwa na NIMR taarifa za vifo ni moja ya vyanzo muhimu vya takwimu katika kupanga mipango na kuandaa sera ya afya ambapo uchambuzi wa takwimu katika makundi ya magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukiza na kundi la ajali na majeraha ulionesha tofati kubwa kati ya mikoa na mikoa.
Utafiti huo umebaini mikoa ya Pwani, Geita na Katavi imeonekana kuathirika zaidi na magonjwa ya kuambukiza na utapia mlo. Wakati vifo kutokana na ajali na majeraha viliathiri zaidi mikoa ya Rukwa, Tabora, Singida na Kigoma. Kundi la magonjwa yasiyoambukiza limeathiri zaidi mikoa ya Ruvuma, Manyara, Dar es Salaam na Mwanza.
“Kati ya mwaka 2006 na mwaka 2015, mikoa ya Kanda ya Kati (Dodoma, Singida, Manyara) mikoa ya kaskazini (Arusha na Kilimanjaro) ndiyo iliyobeba mzigo mkubwa wa vifo vilivyosababishwa na maradhi ya mifumo ya kupumua, upungufu wa damu uliathiri zaidi mikoa ya Dodoma, Simiyu na Mtwara,”imesema. Imeeleza utafiti umeanisha changamoto katika ukusanyaji, uchanganuzi na matumizi ya takwimu katika hospitali zilizopo nchini na kumekuwa na matumizi hafifu ya majina rasmi ya magonjwa kwa kutumia mwongozo wa kimataifa.
“Vyanzo vikuu vya vifo hospitalini nchini Tanzania ni pamoja na malaria, maradhi yanayoathiri mfumo wa kupumua, Ukimwi, upungufu wa damu na magonjwa ya moyo. “Kumekuwa na ongezeko kubwa la vifo vya watoto wachanga na magonjwa ya mfumo wa kupumua katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.