BANDARI TANGA KUHUDUMIA SHEHENA YA NCHI SABA KWA KUTUMIA MPAKA MMOJA

BANDARI TANGA KUHUDUMIA SHEHENA YA NCHI SABA KWA KUTUMIA MPAKA MMOJA

Like
1179
0
Wednesday, 12 December 2018
Local News

Bandari ya Tanga inaelezwa kuwa bandari ya kipekee na ya aina yake barani Afrika inayoweza kuhudumia nchi saba kwa kutumia mpaka mmoja.

Hayo yameelezwa na Meneja wa bandari hiyo, Percival Salama, ofisini kwake jijini Tanga wakati akizungunza na waandishi wa habari kuhusu maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika kuhakikisha wanaongeza ufanisi wa bandari hiyo.

Meneja wa bandari hiyo, Percival Salama,akizungumza na Waandishi wa habari juu ya mipango ya kuboresha bandari ya Tanga na mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitatu ya Rais Magufuli.

Amesema mbali na kuwa na uwezo wa kuhudumia nchi saba bandari ya Tanga kijografia ina sifa ya kuwa bandari pekee ya asili kutokana na kuwa na kina cha maji cha asili cha kuanzia mita tano hadi 30 huku ikizungukwa na visiwa vya asili ambavyo husaidia kupunguza nguvu ya mawimbi.

“Serikali ya awamu ya tano kwa kuona upekee wa bandari ya Tanga iliamua kutoa fedha za kuwekeza katika miradi ya uboreshaji ili kuongeza ufanisi,” amesema.

Salama alifafanua kuwa maboresho makubwa ya bandari hiyo ambayo kwa sasa inaongoza kuwa bandari inayohudumia mizigo kwa kasi Afrika Mashariki, yamefanyika katika nyanja ya ukatabati na ununuzi wa mitambo mipya, ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhia mizigo, na uboreshaji wa mifumo ya teknolojka ya habari na maaasiliano.

Amesema kwa upande wa mitambo tayari imeshaanza kuwasili ambapo kati ya mitambo 20 iliyonunuliwa mitano imeshawasili bandarini hapo na wanatarajia kupikea mingine miwili siku chache zijazo na kwamba hadi kufikia Julai mwakani mitambo yote
itakuwa imewasili.

Alitaja mitambo iliyowasili kuwa ni mashine mbili za kupakia na kushusha makontena yenye uwezo wa kubeba tani 45 kila moja, mashine moja ya kupakia na kushusha mizigo kwenye majahazi na yadi ya uwezo wa tani 30, Fork lift moja ya tani 16 pamoja boti moja ya doria.

Aliongeza kuwa katika uboreshaji wa  miundombinu ya kuhifadhia mizigo Disemba 3 mwaka huu wameanza mradi wa uboreshaji wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia shehena yenye mita za mraba 13,000, mnara wa kuongozea meli, uwekaji sakafu na sehemu ya kulia chakula na kwamba utakamilika Machi 2020.

Aidha alisema serikali kwa kupitia TPA imenunua mdaki unaotembea (mobile scanner) ambao umerahisisha zoezi la uondoshaji mizigo bandarini ambao unaweza kuhudumia makasha 80 hadi 100 kwa saa.

“Kutokana na kuwa na mdaki huu sasa hivi mzigo ukitoka kwenye meli unaingizwa moja kwa moja kwenye mdaki kukaguliwa na kisha unaenda kuhifadhiwa tayari kwa mteja kuja kuchukua baada tu ya kukamilisha nyaraka zake za uondoshaji,” amesema Salama.

Amesema kutokana na maboresho hayo ufanisi umeongezeka kwa kiasi kikubwa ambapo wamefanikiwa kuongeza shehena za mizigo baada ya kuvutia wateja waliokimbia baada ya kutetereka.

“Mfano ni kampuni ya A to Z ya Arusha ambayo tulipotetereka walituhama lakini sasa wamerudi na inapitisha mizigo yake hapa takribani tani 91 kwa mwezi na tuna hakika hadi kufikia 2020/21 tutakuwa tumewarudisha wateja wote waliohama,” amesema Salama.

Alisema Bandari ya Tanga ambayo ina lango kubwa kuliko bandari yeyote Afrika Mashariki la mita 1200, inatarajia kuhudumia shehena ya mizigo tani 1,267,000 kwa mwaka 2018/2019 ikilinganishwa na tani 646,718 za mwaka 2017/2018.

“Mteja anakuja anakaa siku tano anatoa mzigo, kesho hawezi kuja tena lakini sisi hapa mtu akija kuchukua mzigo anaondoka siku hiyo hiyo na meli ikija hapa haisubirishwi kwenye eneo la bahari kama kwenye bandari zingine bali inaingia moja kwa moja kushusha au kupakia mzigo,” alisema Salama.

Alifafanua kuwa ucheleweshaji wa meli bandarini ni moja ya vikwazo kwa wenye meli kwani anapochelewa anapigwa penati ambapo kwa siku moja ni dola 20,000 hivyo anaongeza gharama za uendeshaji.

“Sisi hapa mara nyingi tunawahisha meli kabla hata ya muda wa makubaliano ambapo tumekuwa tukipata zawadi mara kwa mara,” aliongeza.

Awali meli ya tani 40,000 ilikuwa ikihudumiwa kati ya siku sita hadi nane lakini kutokana na maboresho yaliyofanywa bandarini hapo hivi sasa inahudumiwa kwa siku mbili.

“Bandari chakula chake ni mzigo hivyo, jitihada zetu ni kupunguza muda wa kuhudumia na wateja wanaangalia ubora wa huduma na kazi kubwa iliyofanyika katika bandari yetu ni kuboresha eneo la vifaa kwa sababu shida kubwa ilikuwa kwenye mitambo
iliyosababisha uondoshwaji wa mizigo kuchukua muda mrefu,” alisema.

Kuhusu mapato alisema kwa mwaka 2018/2019 bandari hiyo imepangiwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 25 hivyo wameweka nguvu kubwa kuboresha miundombinu na kununua mitambo ya kisasa kufanikisha malengo hayo.

Akizungumzia kuhusu miradi mikubwa iliyopangwa kufanyika Salama alisema tayari wameanza kufanyia kazi agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuchimba na kuongeza kina cha bandari hiyo hadi kufikia kina cha mita 15.

Alisema tayari wamefanya utafiti wa aina ya udongo uliopo ambapo kazi oliyofanywa na kampuni ya BIKO ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Tumegundua kuwa taarifa zilizokuwepo kwa miaka mingi kuwa kuna jiwe si za kweli na kwamba kilichopo ni mchanga na udongo aina ya mfinyanzi na sasa tunatarajia kufanya usanifu na kumtafuta mhandisi mshauri ili tuanze kuchimba,” alisema.

Mradi mwingine ni wa ujenzi wa matanki ya kuhifadhia mafuta kutokana na kuwepo kwa mradi wa bomba la maguta kutoka Ohima Uganda hadi bandarini hapo eneo la Chongoleani litajengwa gati ya mafuta itakayowezesha meli kubwa za kubeba tani 100,000 hadi 250,000.

“Kwa kuweza kupokea meli za aina hii bandari ya Tanga itakua ndio yenye uwezo wa kupokea meli kubwa kuliko bandari yeyote Afrika na huku ni kuelekea kuwa Hub ya ukanda wa Mashariki na kati,” alisema Salama.

Alisema bandari ya Tanga ina fursa kubwa ya kufanyiwa upanuzi kutokana na kuwa na ghuba nne zenye eneo la maji la mita za mraba milioni 35.

“Eneo hili ni sawa na bandari 12 za nchi jirani hivyo unaweza kuona fursa iliyopo kwenye bandari yetu ya Tanga,” aliongeza.

Akizungumza kuhusu changamoto katika bandari hiyo alisema ni uwepo wa bandari bubu ambazokwa mujibu wa tathmini wamebaini uwepo wa bandari bubu 48 kwenye wilaya nne, 12 zikiwa wilaya ya Mkinga, 20 Tanga mjini, moja Muheza, na 15 wilaya ya Pangani.

Alisema uwepo wa bandari bubu unaikosesha mapato serikali pamkna na kuhatarisha usalama wa nchi.

“Bandari ni mipaka ya nchi hivyo kuwepo kwa uingizaji na uondoshaji wa mizigo usiosimamiwa ni kuhatarisha usalama wa nchi kwasababu wanaweza kuingiza bidhaa zisizo ruhusiwa ikiwemo silaha,” alisema.

Hata hivyo alisema wamefanikiwa kwa kiasi fulani kudhibiti bandari hizo baada ya kutoa elimu kwa wananchi na kufanya doria za mara kwa mara kwa kutumia boti yetu ambayo ni mpya.

Alisema tayari wameanza kuona mafanikio ya udhibiti wa bandari bubu ambapo mapato yanayotokana na majahazi yameongezeka kutoka Sh
milioni 26 kwa mwezi hadi Sh milioni 63 kwa bandari ya Tanga na kutoka Sh milioni 2.5 hadi Sh milioni 8 hadi 9 kwa bandari ya Pangani huku lengo likiwa ni kufikia Sh milioni 12.

Aidha alitoa wito kwa wananchi kutumia bandari rasmi ambazo ni Tanga na Pangani kwasababu ni gharama za chini kabisa kuliko bandari bubu ambazo wanaweza kukamatwa na mali zao kutaifishwa.

Alisema katika mpango wa kutaka kurasimisha bandari hizo zipo bandari nne ambazo zinaweza kurasimishwa ambazo ni Mkwaja, Kipungwi, Kikombe na Moha.

Bandari ya Tanga ikonekana kwa juu kama ilivyopigwa na Mpiga picha wetu alipotemblea Bandari hiyo

Mdaki mpya wa kukagua mizigo uliopo katika Bandari ya Tanga

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *